Kanisa linatumikia na kuishi katika uhuru ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi, wakulima
na wanafunzi, alikwenda moja kwa moja hadi kwenye Uwanja wa Michezo wa Campobasso
ambako ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa waamini
kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Campobasso-Boiano, Jumamosi tarehe 5 Julai 2014.
Baba Mtakatifu
Francisko katika mahubiri yake mintarafu Liturujia ya Neno la Mungu amekazia mambo
makuu mawili katika maisha na utume wa Kanisa; kwamba, ni Watu wanaomtumikia Mungu
na wanaishi katika uhuru ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe. Huduma
ya Watu wa Mungu inajionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya Sala, Utangazaji
wa Habari Njema ya Wokovu na kwa njia ya ushuhuda wa upendo na katika mambo haya,
Bikira Maria ni kielelezo na mfano wa kuigwa.
Kanisa katika shule ya Bikira
Maria linajifunza kila siku kuwa ni "Mtumishi wa Bwana" kwa kusoma alama za nyakati
ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa
Kanisa, kwa kutoa kipaumbel cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Huduma ya upendo ni changamoto kwa kila mwamini inayopaswa kumwilishwa
kila siku ya maisha, katika familia, parokiani, sehemu za kazi na kwa majirani.
Huduma
ya upendo ni kielelezo makini cha Uinjilishaji na hapa Kanisa limeendelea kuwa katika
mstari wa mbele kwa kuonesha umama na udugu katika kushirikiana na wahitaji, ili kuwajengea
matumaini zaidi. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini wa Jimbo kuu la Campobasso-Boiano
kwa huduma wanayoifanya kwa kushirikiana na Askofu wao mahalia, changamoto na mwaliko
wa kuendeleza huduma hii ya upendo, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano,
ili kuwahudumia watu wenye mahitaji ya kiroho na kimwili, lakini hasa kwa wasiokuwa
na fursa za ajira, jambo ambalo kwa sasa ni janga la kimataifa linalohitaji mshikamano
wa dhati.
Kazi ni changamoto kubwa inayowawajibisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara
na watunga sera. Hapa utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza
katika mikakati na utekelezaji wake mambo mengine hata kama ni halali yanafuata baadaye.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi katika uhuru wa
kweli unaotolewa na Mwenyezi Mungu ili kushinda ubinafsi na miundo yake yote, ili
kujisadaka kwa moyo wa furaha kama alivyofanya Bikira Maria, kwa kuona na kuguswa
na mahitaji ya wenye shida na mahangaiko zaidi; uhuru unaotekelezwa kwa njia ya upendo
na kumwilishwa katika maisha ya Jumuiya za Kikristo wakati zinapojisadaka kwa ajili
ya huduma kwa jirani, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano.
Baba Mtakatifu
anasema, uhuru wa Mungu unawawezesha waamini kuondokana na hali ya kukosa imani, masikitiko,
woga na utupu katika maisha ya ndani; upweke, majonzi na litania ya malalamiko yasiokuwa
na msingi. Hata katika Jumuiya za Waamini kuna watu wanaotaka kujilinda zaidi kuliko
kujisadaka kwa ajili ya wengine, lakini wakijiachilia mikononi mwa Yesu anaweza kuwaokoa.
Hata katika mapungufu yao kibinadamu na dhambi wanazotenda, bado wanahamasishwa kuwa
na furaha na ujasiri ili kushuhudia imani yao kwa kujenga na kuimarisha umoja na Mwenyezi
Mungu, ili kukabiliana kwa ujasiri mkubwa magumu na vishawishi vya maisha.
Baba
Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Uwanja wa Michezo wa Campobasso kwa kuwaombea waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kutembea katika uhuru wa kweli waliopewa na Mwenyezi Mungu. Bikira Maria aliwezeshe
Kanisa kuwa kweli ni Mama na mkarimu kwa wote; waoneshe upendo na mshikamano kwa wagonjwa
na vijana na kwamba, Bikira Maria, Mama wa uhuru awe ni kielelezo cha faraja na matumaini
thabiti!
Naye Askofu mkuu Giancarlo Bregantini kwa niaba ya waamini wake, amemshukuru
Baba Mtakatifu Francisko kwa kuangalia unyenyekevu wa wananchi wa Molise na kuamua
kuwatembelea. Amemshukuru kwa ushuhuda wa mapendo anaoendelea kuwaonjesha Watu wa
Mungu; Utamaduni wa mshikamano ili kukabiliana na changamoto za maisha, kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii pamoja
na kuishi katika uhuru wa wana wa Mungu kwa kuiga mfano wa Bikira Maria.
Ni
changamoto hii inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kuwaonesha upendo na ukarimu wageni na
wahamiaji, kwa kujikita katika ukweli na haki. Anawashukuru waamini na watu wote wenye
mapenzi mema waliojisadaka kwa ajili ya kufanikisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu
Francisko Mkoani Molise, Kusini mwa Italia.