2014-07-04 15:28:32

Yaliyojiri kwenye mkutano wa Baraza la Makardinali


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Baraza la Makardinali, Ijumaa jioni tarehe 4 Julai 2014 wamehitimisha mkutano wao wa tano na kalenda inaonesha kwamba, watakutana tena tarehe 15-17 Septemba 2014 na baadaye tarehe 9 hadi 11 Februari 2015. Mambo yaliyojiri katika mkutano huu ni pamoja na: Utawala wa Mji wa Vatican, Sekretarieti ya Vatican, Benki ya Vatican pamoja na Mabaraza kadhaa ya Kipapa.

Kwa namna ya pekee wamejadili kuhusu mchango wa waamini na familia katika maisha na utume wa Kanisa mjini Vatican. Haya ni mambo ambayo yatapembuliwa kwa kina na mapana na hatimaye, kufanyiwa kazi ili kupata mwelekeo mpya wa Sekretarieti ya Vatican kadiri ya ushauri uliotolewa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi.

Haya yameelezwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Ijumaa tarehe 4 Julai 2014. Amesema, wajumbe wa Baraza la Makardinali wamechambua na kubadilishana mawazo kuhhusu Balozi za Vatican na dhamana yake katika nchi husikapamoja na kanuni za kuwachagua Maaskofu wapya.

Mkutano huu umekuwa unafanyika kwa kuongozwa na kanuni kuu tatu: uhuru, ukweli na urafiki na wengine wametafsiri kuwa ni “free, frank and friendly” yaani (3F). Hapa Makardinali walikuwa na uhuru wa kuelezea kwa kina na mapana, kwa kuzingatia ukweli na moyo wa urafiki na upendo. Baba Mtakatifu mwenyewe ameshiriki kama wajumbe wengine kwa kuchangia mawazo na mang’amuzi yake.

Hadi sasa hakuna rasimu ambayo inaweza kufanyiwa kazi, lakini kila Kardinali amepewa kitengo cha kushughulikia ili kuwashirikisha wajumbe wengine.








All the contents on this site are copyrighted ©.