Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya hivi karibuni limekutana na kuzungumza na Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya kuhusu hali tete inayoendelea kujitokeza nchini humo na hasa misigano
ya kisiasa inayohatarisha usalama, umoja na mshikamano wa kitaifa. Maaskofu wanatawaka
wanasiasa nchini Kenya kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa na kuanza kushughulikia
masuala msingi kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wa Kenya.
Maaskofu
wanaitaka Serikali kuharakisha mageuzi katika vikosi vya ulinzi na usalama, kubainisha
sera na mikakati ya kukuza na kuendeleza uchumi pamoja upatikanaji wa fursa za ajira
kwa vijana, kwani vijana wengi kwa sasa wanatumiwa na wanasiasa kwa ajili ya mafao
yao binafsi pamoja na kupambana na umaskini.
Rais Uhuru Kenyatta kwa upande
wake anasema, yuko tayari kukutana na kuzungumza na Wananchi wa Kenya kadiri ya sheria
na katiba ya nchi. Serikali ya Kenya inaendelea kuongeza rasilimali watu na fedha
ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Utawala wa sheria utaendelea
kuimarishwa nchini Kenya na watambue kwamba, sheria ni msumeno.
Kardinali John
Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anawataka waamini na watu wote wenye
mapenzi mema nchini Kenya kuungana pamoja kusali ili kuombea amani, usalama na ustawi
wa wananchi wote wa Kenya.