2014-07-04 11:11:34

Uaminifu katika maisha ya ndoa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawaalika wanandoa na familia kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, kwa kujikita kiaminifu katika maisha na utume wa ndoa, kama sehemu ya mchakato wa kutakatifuzana ndani ya familia. Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni kwa wanandoa kutoka Majimbo mbali mbali nchini Kenya waliokuwa wamekusanyika Jimbo kuu la Nairobi kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa familia kitaifa, uliokuwa umeandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Kilele cha maadhimisho haya ilikuwa ni Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Salesianus Mugambi, Mwenyekiti wa Tume ya Ndoa na Familia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, ambaye katika mahubiri yake amewataka wanandoa kuwa kweli ni walimu wa imani, kwa kujenga na kukuza utamaduni wa sala katika familia na maisha ya waamini katika ujumla wao pamoja na kuendelea kulifahamu Kanisa ili kuweza kulitumikia kwa ukarimu zaidi.

Askofu Mugambi amewakumbusha wanandoa kwamba, leo hii ndoa inakabiliana na changamoto mbali mbali, mwaliko kwa wanandoa wenyewe kusimama imara bila kuyumba katika misingi ya imani, maadili na utu wema. Ni wajibu wao kujikita katika maisha ya sala pamoja na kuziombea familia nyingine zinazoogelea katika shida na mahangaiko ya ndani.

Waamini wajitaabishe kulifahamu Kanisa Katoliki kwa njia ya maisha na utume wake; Liturujia na Ibada; Nyaraka na mafundisho mbali mbali yanayotolewa na viongozi wa Kanisa pamoja na ushuhuda wa waamini katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, ili kweli waweze kushiriki katika kuyachachua malimwengu kwa njia ya kweli na shuhuda za Kiinjili. Habari za Kanisa wanazosoma na kuzisikia kwenye vyombo vya habari hazitoshi, kumbe kuna haja ya kujibidisha zaidi ili kulifahamu Kanisa.

Askofu Mugambi anasikitika kusema kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii vimekuwa na mwelekeo hasi kwa vijana wengi, kiasi kwamba, kuna baadhi yao wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha. Vijana wengi wanajikuta hawafahamu kwa undani Mafundisho ya Kanisa na tunu msingi zinazosimamiwa na kufundishwa na Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu na matokeo yake vijana wanajikuta wakimezwa na malimwengu pamoja na mmong'onyoko wa maadili na utu wema.

Askofu Mugambi amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa linaweza kukua na kukomaa kutokana na mchango unaotolewa na waamini walei kwa kulitegemeza Kanisa kwa njia ya mchango lakini zaidi kwa njia ya utakatifu wao wa maisha. Ni wajibu kwa waamini kushirikisha karama na vipaji vyao kwa ajili ya ujenzi na ustawi wa Kanisa mahalia, huku wakimshuhudia Kristo na Kanisa lake katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku!







All the contents on this site are copyrighted ©.