Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya ambaye pia ni mwakilishi
wa Vatican kwenye Makao makuu ya Shirika la mazingira na makazi ya watu la Umoja wa
Mataifa, hivi karibuni ameshiriki katika mkutano wa mazingira uliokuwa unafanyika
Jijini Nairobi, Kenya kwa kukemea ulaji wa kupindukia na kwamba, umefika wakati kwa
watu kubadili tabia hii. Vatican itaendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa
katika kulinda na kutunza mazingira.
Ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku
za usoni unategemea kwa kiasi kikubwa, jinsi ambavyo mwanadamu anavyojitahidi kulinda
na kutunza mazingira, kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa kwani mazingira ni zawadi
ya kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitunza na kuiendeleza. Mwanadamu
katika historia yake amekuwa ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira, changamoto
kwa sasa kuonesha unyenyekevu, kiasi na kuanza kujikita katika kulinda na kutunza
mazingira.
Askofu mkuu Balvo amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu wa mazingira
ambao kwa mara ya kwanza katika historia umefanyika Jijini Nairobi kwa ngazi ya kimataifa,
ili kutafuta njia, mbinu na mikakati ya kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira,
kwani mazingira ni kazi ya uumbaji inayowawajibisha binadamu. Amempongeza pia Marehemu
Professa Wangari Maathai, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utunzaji bora wa
mazingira nchini Kenya, changamoto ya kuendeleza kazi ya uumbaji.
Vatican inafuatilia
kwa umakini mkubwa mikakati na malengo yaliyoainishwa na Shirika la Mazingira la Umoja
wa Mataifa kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuratibu ulaji wa kupindukia, ili kuwa
na ustawi na maendeleo kwa siku za usoni, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ikumbukwe kwamba, rasilimali ya dunia
ni kwa ajili ya mafao ya wote. Lakini, uzoefu unaonesha kwamba, kuna baadhi ya watu
wenye uchu wa mali na fedha wanaoendelea kuharibu mazingira kwa ajili ya mafao yao
binafsi. Jamii inapaswa kujirekebisha kwa kuzingatia msingi na kanuni maadili katika
masuala ya fedha na uchumi.
Maendeleo endelevu ya mwanadamu hayana budi anasema
Askofu mkuu Balvo kujikita katika mwelekeo wa kijamii na maisha ya kiroho, kwa wote
bila upendeleo, ili kuchangia mustakabali wa mafao na maendeleo ya wengi!