Majadiliano ya kidini yasaidie kupambana na umaskini na ukosefu wa haki msingi!
Ukweli, upendo na huruma ni tunu msingi katika maisha ya waamini wa dini mbali mbali
duniani, mambo yanayoweza kumsaidia mwamini kuwa kweli ni chombo cha amani, haki na
upatanisho.
Ni changamoto iliyotolewa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais
wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini alipokutana na kuzungumza na wawakilishi
wa dini ya Kihindu, waliokuwa wanaongozwa na Morari Bapu, moja ya wahubiri wakuu wa
dini hii, walipomtembelea mjini Vatican.
Waamini wa dini hii wako mjini Roma
kushiriki katika warsha inayoongozwa na kauli mbiu “mchakato wa upatikanaji wa amani
duniani kwa njia ya mafundisho ya Yesu pamoja na kuangalia mwelekeo chanya kutoka
katika Kanisa Katoliki. Warsha hii imeandaliwa na Mfuko wa Lord Dolar Popat kutoka
London, Uingereza.
Akichangia katika warsha hii, Kardinali Tauran amekazia
umuhimu wa kudumisha tasaufi ya maisha ya kiroho, kwa kuheshimiana; kwa kulinda na
kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa
kidugu. Hapa kuna haja kwa waamini wa dini mbali mbali kujenga madaraja kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Majadiliano
ya kidini ni nyenzo msingi katika kudumisha umoja, mshikamano na udugu kati ya watu.
Kardinali
Tauran anahitimisha kwa kusema kwamba, dini mbali mbali duniani zinaweza kuchangia
katika kutafuta na kusimamia mafao ya wengi, kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa
Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani ya kweli. Hapa kuna haja ya kudumisha
utamaduni wa watu kukutana ili kudumisha mshikamano, ili kwa pamoja, waweze kusimama
kidete kupambana kufa na kupona na ukosefu wa haki msingi, umaskini na magonjwa.