Kanisa litaendelea kuwasaidia maskini na wagonjwa!
Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni kati ya magonjwa yanayoendelea kuhatarisha maisha ya watu
wengi duniani, lakini zaidi wale wanaoishi katika Nchi zinazoendelea duniani. Kunako
mwaka 1993 Shirika la Afya Duniani lilitangaza mikakati ya kupambana na ugonjwa huu
na kuna mafanikio ambayo yameanza kuonekana.
Kati ya mwaka 1995 hadi mwaka
2012, maisha ya watu millioni 22 yaliokolewa na wagonjwa millioni 56 walipata tiba.
Haya ni mafanikio makubwa, lakini bado kuna changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuhakikisha kwamba, inatokomeza ugonjwa wa Kifua kikuu duniani kwa kutumia dawa makini
dhidi ya ugonjwa huu pamoja na magonjwa yanayohusishwa na Ukimwi.
Hayo
yamesemwa na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wahudumu wa
Sekta ya afya wakati alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu
mikakati ya kutokomeza ugonjwa wa Kifua kikuu katika nchi zile ambazo zina idadi ndogo
ya wagonjwa wa kifua kikuu Barani Ulaya. Mkutano huu umefunguliwa mjini Roma, tarehe
4 Julai na unatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 5 Julai 2014. Mkutano huu umeandaliwa
na Shirika la Afya Duniani kwa kushirikiana na Chama cha Magonjwa ya mfumo wa hewa
Barani Ulaya.
Takwimu zinaonesha kwamba, kunako mwaka 2012 kulikuwa na wagonjwa
wa Kifua kikuu millioni 8.6, kati yao, wagonjwa millioni 1.3 walifariki dunia. Wengi
wao ni watu maskini, wanawake, watoto, wahamiaji, wafungwa watu wasiokuwa na makazi
pamoja na wagonjwa wa Ukimwi. Nchi maskini duniani kama vile Afrika na Ulaya ya Mashariki
pengine hazifanikiwa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Mwaka 2015, kumbe kuna haja kwa
Jumuiya ya Kimataifa kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa huu hata baada ya Mwaka
2015.
Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua kikuu yawahusishe wadau mbali mbali,
ili kuunda kikosi kazi makini kitakachotekeleza mikakati hii kwa ari na kasi kubwa
zaidi pamoja na kuyashirikisha Mashirika ya Kidini kwani haya mara nyingi yanafanya
kazi katika maeneo ya vijijini na miongoni mwa watu maskini. Kanisa kwa upande wake,
litaendelea kuonesha mshikamano na maskini pamoja na wagonjwa kama sehemu ya utekelezaji
wa utume wake wa Kinabii na kwamba, hii ni haki jamii. Jamii inayojali haina budu
kujenga mahusiano bora na wagonjwa kwa kuwaonjesha huruma kama sehemu ya ubinadamu.
Askofu
mkuu Zygmunt Zimowski anawashukuru wadau mbali mbali kwa kushirikisha: ujuzi, maarifa,
weledi, muda na rasilimali fedha na watu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaosumbuliwa
na Kifua kikuu sehemu mbali mbali duniani. Bado kuna haja ya kuendeleza mshikamano
na huruma kwa wagonjwa wa Kifua kikuu, ili kuendeleza utu na heshima ya binadamu!