Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, Tanzania, hivi karibuni ameitaka
Familia ya Mungu nchini Tanzania kujivunia kifo cha Sr. Maria Crescentia Kapuli wa
Shirika la Bikira Maria Malkia wa Afrika, Jimbo Katoliki Mbeya na wala kisiwakatishe
tamaa katika kutekeleza utume wao miongoni mwa Watanzania kwani mauaji haya ya kikatili
ni kati ya changamoto ambazo wanapaswa kuzikabili kwa imani na matumaini pasi na kukata
tamaa! Amewataka waamini na watanzania kwa ujumla kujenga na kudumisha moyo kusamehe
na kuwaombea wauaji ili watubu na kumrudia Mungu.
Aidha Sr.Maria Bilgita Mbanga
ambaye ni Makamu Mama mkubwa kutoka Parokia ya makoka na mwalimu wa shule ya mwenyeheri
Anwarite ambaye alikuwa na marehemu Sista Cresensia aliyekuwa Mama mkubwa wake hadi
mauti yanamkuta ameelezea tukio hilo la kusikitisha.
Akizungumza katika ibada
ya misa takatifu ya mazishi katika kanisa la nyumba ya masista Hasamba, Askofu Nyaisonga
aliyeongoza misa akiwa na Mhashamu Askofu Evaristus Marcus Chengula (IMC) amesema
mateso aliyoyatapa sr.Maria Crescentia yanaashiria alama ya kushinda mauti.
Askofu
Nyaisonga ambaye muda wote wa mahubiri yake alionekana kujizuia kulia huku macho yake
yakionekana kulengwa na machozi ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kutenda haki
katika suala hilo huku akiwasihi wauaji kumrudia Mungu na kutubu ili wawe raia wema.
"Masista tukio hili lisiwarudishe nyuma bali liwatie nguvu na kuwa chachu ya utume
wenu, muwe kama askari vitani anapopigwa mmoja wengine mnasonga mbele, Sr. Crescentia
alifanyakazi katika mazingira yenye changamoto kubwa na alilijuwa hilo, amekufa na
Yesu,"alisema.
Alisema waamini wanapaswa kuwasamehe waliotenda uhalifu huo
na kuwataka waendelee kuwaombea ili waweze kumrudia Mungu na kuishi kwa amani na kutafuta
riziki kwa njia za halali.
Makamu mama mkubwa Sr. Maria Bridgita licha ya kutoa
ushuhuda wake katika shamba la Mungu la masista akizungumza na Mwandishi wa habari
hizi anasimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa
"Baada ya kusindikizana hadi
Benki ya CRDB pale Mlimani City tulikuta wateja wachache Sr. alihudumiwa na baadaye
alinipa ishara niende kumsaidia nikafanya hivyo tukahifadhi fedha katika mabegi yetu
mawili na nyingine katika bahasha na akampigia simu mkandarasi ambaye aliwasiliana
naye tangu tukiwa shuleni kuwa tutamlipia pale pale Benki,"alisema Sr.Bridgita.
Aliongeza,"Tuliona
yule Mkandarasi anachelewa kuja Sr.Crescentia akasema twende tukafanye kazi nyingine
alafu tukifika shuleni tutampigia aje, lakini tulipokuwa tunatoka karibu na mlango
tukakutana naye Mkandarasi tukarudi naye katika chumba maalum tukamkabidhi fedha zake
zilizokuwa katika begi langu tukamsainisha tukaaagana naye."
"Tukapanda gari
letu kuelekea River Side, Ubungo, Jijini Dar es Salaam ambako tulichukuwa gunia tano
za maharage wakati tukiwa katika mafungo Jimboni Mbeya tulimpigia simu mwenye duka
hilo apeleke maharage shuleni, baada ya kufika na kuegesha gari pembeni niliteremka
na kwenda kulipa Sr. Crescentia na Dreva walibakia ndani ya gari kunisubiri".
"Sikuchelewa
sana baada ya kulipa fedha yule mwenye duka alisema ameleta mchele mzuri akanipa kilo
mbili za zawadi nikarudi katika gari nikiwa nataka kumuonesha sista mchele ghafla
nilisikia mlio kama wa bomu ukitokea upande wangu nikadhani Dereva amegongesha gari
nikawa namlaumu naye Dereva alijibu hajagongesha."
"Ghafla walitokea watu watatu
na kutuamrisha tusipige kelele na ndipo nilipoingiwa hofu bila kujitambua niliangukia
katika mlango wa pili na kujikuta nipo nje ya gari nikijizoa zoa huku mkoba wangu
ukiokotwa na mmoja wa wale majambazi nami nikajikuta nimeshikwa na vijana katika duka"
Niliwauliza
Sista yupo wapi waliniambia nitulie baadaye wakaja akina mama fulani wakilia na kunitia
moyo na nikauliza kimetokea nini na sista yupo wapi wakaniambia amelala amepoteza
fahamu lakini baada ya kuwasumbua sana wale vijana wakaniachilia nikaenda lilipo gari
nikakuta kundi la watu wamemzingira sista yupo chini amefunikiwa na kitenge huku damu
zikitiririka, ilinichanganya zaidi kwani mimi nilijuwa tulikimbia wote mda ule".
Alisema
baada ya hapo aliambiwa apige simu kwa wenzake alishindwa ambapo akina mama walimsaidia
kuwajulisha kilichotokea na watu wengine waliwapigia Mapadre na baadaye walifika na
kunichukuwa huku gari lingine likimbeba sista na wakati nikihojiwa ndipo nilijuwa
sista amefariki baada ya Polisi kuulizwa akajibu sista mwenzake marehemu tunaye hapa."
Hiyo ndiyo hali halisi ya tukio lilivyotokea na kuchukuwa maisha ya Sista Crescentia,
alimaliza kusimulia Sr.Bilgita huku akitokwa na machozi.
Wakizungumza baada
ya mazishi baadhi ya waumini wameleezea kifo hicho cha kikatili,kustaajabisha na kuitaka
serikali kuchukuwa mkondo wake ili iwe fundisho kwa watu wengine akama ambavyo wazazi
kutoka parokia ya Mbalizi na Sr.Anjelina walivyosema kuwa wameshtushwa na mauaji ya
kikatili na kinyama aliyofanyiwa Sr.Crescentia mithili ya watu waliokuwa wakilipiza
kisasi.
"Labda walikuwa wanamjuwa ndiyo maana wamemuadhibu kiasi hicho lakini
kwa nini?, Haingii akilini hata kidogo, maana hata wangempiga kofi tu,"walisema.
Baadhi
ya waamini kutoka kanisa kuu la Kiaskofu Parokia ya Mbeya mjini Cotrida Enjewele,
Maria Simfukwe, Iporito Mwihava pamoja na Veronica Mwakifuna hawakubaki nyuma kuelezea
hisia zao kuhusiana na kifo cha Sista huyo kwa kusema wamebakia njia panda, wamepigwa
butwaa na mauaji hayo.
Sisi watanzania wapenda amani na waamini wote wa imani
tofauti ambao tunaamini Mwenyezi Mungu yupo, tunadiriki kusema wote waliotenda ama
kuhusika katika tukio hilo la kuzima mwanga wa mshumaa wa Sr.Crescentia hapa duniani
Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kutubu na kumwongokea, lakini pia haki itendeke!
Ninachopenda
kusema mauaji ya aina hii hayawezi kuvumilika hata kidogo,sisi watanzania,wapenda
amani tunatarajia Jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola vitachukuwa hatua madhubuti
kuhakikisha watu hao wanapatikana na kufikishwa katika mkono wa sheria.
Sote
tunaamini na tunatarajia kusikia kuwa kutokana na umakini na umahiri mkubwa wa maofisa
wetu wa vyombo vya dola wahusika watakamatwa, ili mchezo kama huu usije kurudia tena
kwa kuwakatili roho watu wa mungu na raia wengine wema.
Nilipoamini kuwa Jeshi
la Polisi na vyombo vingine vya dola vikiamua kweli kufanyakazi na vinafanikiwa ni
pale alipouawa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Liberatus Barow na hata
mfano mdogo alipouawa Askari Polisi wa kituo kidogo cha Mkwajuni,wilayani Chunya kwani
wahusika na mtandao mzima walikamatwa vivyo hivyo tunavyoamini kwa tukio hili la Mtumishi
wa mungu.
Ni rai yangu katika tukio hili Polisi mtende haki katika kuwatafuta
na kuwakamata wahusika wa mauaji badala ya kuwakamata vibaka na kuwabambikia kesi
kama wanavyoita vijana wa mitaani 'mkawapa kichwa' ili kufunga jarada la upelelezi
na hatimaye kutangaza watuhumiwa wamekamatwa.
Mwenyezi Mungu anapenda kuona
haki inatendeka licha ya sisi wanadamu tuliopewa dhamana kukengeuka na hata kufikia
hatua vijana wa mitaani wakisema haki mbinguni sheria duniani, kwani laana na adhabu
tunazionja humu humu duniani za kutotenda haki ila ni siri iliyo katika nafsi na familia
zetu.
Wapo baadhi ya askari waliowahi kudhulumu haki za raia wema kwa kuwapatia
kesi na matokeo yake maisha yao yamekuwa na laana hivyo tunasihi wahusika wakamatwe
na sheria iweze kuchukuwa nafasi yake.