Familia zijengewe uwezo kukabiliana na changamoto za maisha!
Vitendo vya jinai na unyanyasaji vinavyofanywa dhidi ya watoto wadogo ni sehemu ya
litania ya mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya watoto kwa sasa na kwa siku za
usoni.
Kuna utalii
wa ngono unaowahusisha watoto wadogo, picha za ngono, mauaji ya watoto wenye ulemavu
wa ngozi, watoto wanaofanyishwa kazi za suluba na kupelekwa mstari wa mbele wakati
wa vita na machafuko ya kisiasa. Haya ni mambo yanayohitaji kujenga utashi wa kisiasa,
ili kuchukua hatua madhubuti kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi, Jamii, Taifa na
Kimataifa, ili kuweza kukabiliana, kuyashughulikia kisheria na hatimaye, kuyang’oa
katika Jamii.
Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na biashara haramu ya binadamu
inayoendelea kushamiri kila kukicha jambo ambalo ni kinyume cha utu na heshima ya
binadamu. Utumwa mamboleo ni biashara ya kitaifa na kimataifa inayowaingizia wahusika
mabillioni ya fedha. Baadhi ya watu wanajikuta wametumbukizwa katika biashara hii
kwa kupewa ahadi za uwongo, kwa kutamani kupata maisha bora zaidi au fursa za ajira,
lakini mwishoni, wanajikuta wakiuzwa kama bidhaa sokoni.
Kuna haja kwa Jumuiya
ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu ili kupata kiini cha matatizo haya ili kuyapatia
ufumbuzi wa kudumu. Watoto wengi wanajikuta wakinyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima
yao kutokana na: umaskini wa hali na kipato wa familia zao; athari za myumbo wa uchumi
kimataifa; kinzani za kisiasa, kikabila na kidini; mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa
kwa watoto kujikuta wanakosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha.
Ni mchango
kutoka kwa Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye
Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva wakati wa mkutano wa Baraza la haki
msingi za binadamu la Umoja wa Mataifa, uliofanyika hivi karibuni mjini Geneva. Anasema,
kwa miaka kadhaa Vatican imeonesha wasi wasi wake kutokana na madhara ya kuvunjika
kwa ndoa na familia nyingi duniani na kwamba, wanaoteseka zaidi ni watoto. Familia
nyingi zinakabiliana na matatizo makubwa kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana
na wajibu wake.
Kutokana na changamoto hizi, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuibua mbinu mkakati na sera makini kwa ajili ya kujenga na kuimarisha misingi bora
ya familia pamoja na kuzijengea familia uwezo wa kiuchumi ili kukabiliana na gharama
ya maisha. Mikakati hii ikitekelezwa kwa umakini mkubwa inaweza kusaidia kupunguza
kwa kiasi kikubwa migogoro ya kifamilia, madhulumu na nyanyaso kwa watoto wadogo na
wanawake.
Ujumbe wa Vatican unaendelea kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa
kuheshimu sheria za kimataifa kuhusu watoto wadogo kupelekwa mstari wa mbele katika
vita na migogoro ya kijamii. Ni jambo lisilokubalika kuona kwamba, watoto wanapelekwa
mstari wa mbele kuwa ni chambo cha mapigano. Inasikitisha kuona kwamba, watoto wanapokonywa
matumaini ya maisha bora kwa sasa na kwa siku za usoni, kwa kulazimishwa kwenda Jeshini,
kutekwa nyara, kujeruhiwa na hatimaye kufa wakiwa vitani!
Imeandaliwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.