Mh. Padre John Bonaventure Kwofie ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Sekondi-Takoradi,
Ghana
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre John Bonaventure Kwofie wa Shirika
la Roho Mtakatifu kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sekondi-Takoradi, nchini Ghana.
Askofu mteule amewahi kuwa Padre mkuu wa Kanda, Shirika la Wamissionari wa Roho Mtakatifu
Afrika Magharibi. Alizaliwa tarehe 26 Aprili 1958 huko Powa, Jimbo Katoliki la Sekondi-Takoradi,
Ghana.
Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, akapadrishwa kunako tarehe
23 Julai 1988, huko Kumasi, Ghana. Katika maisha na utume wake kama Padre, alipangiwa
shughuli mbali mbali za kichungaji nchini Gambia na kati ya mwaka 1991 akapelekwa
mjini Roma kwa ajili ya masomo ya juu katika Sayansi ya Maandiko Mtakatifu, maarufu
kama Biblicum na huko akajipatia shahada ya uzamili.
Amewahi pia kuwa ni Makamu
mkuu wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika kwa vipindi viwili;
Padre mkuu wa Kanda ya Shirika, Afrika Magharibi, Mratibu wa Wakuu wa Mashirika ya
Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika, utume alioufanya kazi ya mwaka 2003 hadi mwaka
2005.
Kati ya Mwaka 2004 hadi mwaka 2012 alikuwa ni mshauri wa kwanza wa mkuu
wa Shirika la Roho Mtakatifu ulimwenguni. Jimbo la Sekondi-Takoradi lilianzishwa kunako
mwaka 1969 na liko chini ya Jimbo kuu la cape Coast, Ghana.