2014-07-03 08:52:24

Mageuzi ya kiuchumi yazingatie utu na heshima ya binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha mwaka mmoja tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki amekuwa na mvuto mkubwa kwa watu wengi ndani na nje ya Kanisa. Mchakato wa mageuzi yaliyoelekezwa na Makardinali katika vikao vyao, yanaanza kutoa cheche za matumaini kwa maisha na utume wa Kanisa. RealAudioMP3

Papa Francisko ni kiongozi ambaye anaendelea kulichangamotisha Kanisa kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwatangazia watu Injili ya Furaha na Matumaini, kwa kuguswa na shida na mahangaiko ya watu wanaowazunguka badala ya kujifunga katika ubinafsi na hali ya watu kujitafuta wenyewe. Kanisa lipo kwa ajili ya watu na mafao ya wengi. Linatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kuwahudumia watu, kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima yabinadamu pamoja na kutafuta mafao ya wengi, haki na amani.

Hivi ndivyo Kardinali Vincent Gerard Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anavyomwelezea Baba Mtakatifu Francisko katika makala iliyochapishwa hivi karibuni kwenye Jarida la uchumi lijulikanalo kama “Huffington Post” linalochapishwa nchini Uingereza. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, kama ilivyo pia hata katika masuala ya uchumi na maendeleo ya watu.

Sera makini za uchumi hazina budi kujikita katika kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; uchumi unaoendekeza matabaka na kinzani, unaweza kusababisha majanga katika maisha ya watu. Inasikitisha kuona kwamba, leo hii sera zinazotawala katika masuala ya uchumi na maendeleo ya watu ni “mwenye nguvu mpishe” na wale “akina yakhe pakavu tia mchuzi” wanaendelea kuambulia patupu! Athari za myumbo wa uchumi kimataifa umesababisha watu wengi kukosa fursa za ajira na hatimaye kuanza kukata tamaa ya maisha bora!

Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho na mtindo wake wa maisha anapinga sera na mikakati ya kiuchumi ambayo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu na kumgeuza binadamu kuwa kama “soli ya kiatu”. Kumbe, hapa Baba Mtakatifu anakazia mshikamano wa upendo na udugu kati ya watu, ili kushirikishana rasilimali na utajiri wa dunia, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Lengo ni kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mateso ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Jukwaa la uchumi Kimataifa, lililofanyika huko Davos, Januari mwaka huu, aliwasihi wajumbe kutoa kipaumbele cha pekee kwa mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu na kwamba, kazi ni kielelezo cha utimilifu wa maisha ya binadamu. Bila kazi mwanadamu anajiona mtupu, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake mbele ya Familia na Jamii inayomzunguka. Viongozi wa taasisi na makampuni mbali mbali watambue kwamba, wanayo dhamana kubwa mbele ya jamii inayowazunguka, kumbe wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi nateknolojia kuna uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula, lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, bado kuna watu wanateseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo. Chakula kipo, kinatumika na kutupwa jalalani, hali inayoonesha ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya wengine. Kuna watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, kinzani, migogoro na maafa asilia, lakini wanakumbana na kifo hata kabla ya kufika kwenye “Nchi ya ahadi”, iliyojaa maziwa na asali. Kwa wale wanaofanikiwa kufika salama salimini, wanabaguliwa na kutengwa.

Kardinali Vincent Gerard Nichols anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kukazia pia kanuni maadili katika masuala ya uchumi na maendeleo na biashara; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu na heshima ya binadamu; mafao y awengi. Haya ni mambo yanayopaswa pia kuzingatiwa katika masuala ya uchumi na maendeleo. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa mabadiliko ya kina, ingawa ni safari ndefu hadi kupata mafanikio yanayokusudiwa.

Ni matumaini ya Kardinali Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales kwamba, changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, zitawasaidia watu wengi zaidi kufanya tafakari ya kina itakayosaidia kuleta mabadiliko yanayozingatia utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya binadamu. Haya yote yanawezekana, ikiwa kama watu watasikiliza kwa makini na hatimaye, kuzifanyia kazi changamoto hizi.

Taarifa hii imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.