Askofu mkuu Giancarlo Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso-Bojano, Italia, anawakumbusha
waamini kwamba, Jimbo lao limesimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto
kwa waamini kujifunza kusema, asante, kwani Ekaristi Takatifu maana yake ni Shukrani
na changamoto ya kusimamia mema na kujenga urafiki, upendo na mshikamano wa kweli
kwa kujitoa kwa ajili ya wengine ndani ya Jamii.
Hii ni changamoto ya kujenga
na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu kwa kuendeleza ari na moyo wa ushirikiano,
wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko anayetarajiwa
kutembelea Jimboni humo, Jumamosi ijayo, tarehe 5 Julai 2014. Kwa namna ya pekee,
waamini wanaalikwa kujiandaa kiroho kwa ajili ya kumpokea Baba Mtakatifu, kwa kuonesha
ukarimu na mshikamano na maskini pamoja na wahamiaji.
Askofu mkuu Bregantini
anawataka kushikamana na kuonjeshana umoja wa kweli, kwani Baba Mtakatifu anapenda
kuwakumbatia wote ili kuwaonjesha huruma na upendo kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Kwa maneno machache, waamini wajiandae kikamilifu kumpokea na kumwonesha moyo wa upendo
na ukarimu Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea Jimboni humo!