2014-07-03 10:27:13

Jengeni amani!


Kardinali Jean Louis Touran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliaano ya kidini, Jumatano jioni, tarehe 2 Julai 2014 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Watakatifu Mitume mjini Roma, katika mkesha wa kuombea amani na upatanisho nchini Syria na Iraq.

Kardinali Tauran katika mahubiri yake anasema kwamba, falsafa ya mtutu wa bunduki imekuwa mbadala wa majadiliano yanayolenga kutafuta haki na amani ya kweli miongoni mwa wananchi ambao kwa sasa wamekumbwa na vita huko Syria na Iraq. Kanisa litaendelea kusimamia, kutafuta na kuombea amani, kwani huu ni utume ambao Kanisa limekabidhiwa na Kristo Mfufuka na hivyo ni dhamana inayowajibisha.

Kardinali Tauran anasema amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo amemkabidhi mwanadamu kuiendeleza, lakini kwa bahati mbaya, amani inakumbana daima na kinzani kwani haya ni matokeo ya dhambi ya asili. Vita na vitendo vya kigaidi ni kati ya mambo ambayo kwa sasa yanatishia maisha na usalama wa mwanadamu. Vita inapaliliwa kwa njia ya woga usiokuwa na mashiko, hali ya kudhaniana vibaya, chuki, wivu na uchu wa mali na madaraka.

Kardinali Tauran anabainisha kwamba, amani, haki, ukweli na uhuru kamili ni mambo yanayochangamana na daima yanakwenda pamoja. Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya amani kwa kusimama kidete kulinda na kuheshimu utu wa binadamu; kuendeleza haki, kukubali na kuthamini tofauti zinazojitokeza kama utajiri na wala si kikwazo cha umoja na mshikamano kati ya watu; wanatakiwa kushirikiana na wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Kardinali Tauran anasema kwamba, tunu hizi msingi zinapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kwani hii ni dhamana endelevu inayoweza kusaidia kushinda vita, kinzani, tofauti msingi, ukosefu wa usawa kijamii na kiuchumi. Waamini wanapata nguvu hii inayobubujika kutoka katika neema ya Ubatizo na Kipaimara.

Hivyo ni wajibu na dhamana yao kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo vya amani kwa kuwathamini na kuwatakia wengine mema; kuwa na kiasi, tayari kusamehe, kujipatanisha na kusahau, daima wakionesha ile hamu ya kutaka kujenga umoja, kupatanisha na kuomba msamaha. Mafao ya wengi yapewe kipaumbele cha kwanza kuliko kutanguliza ubinafsi kwa kuonesha upendo na mshikamano na maskini pamoja na kutetea uhai ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.