2014-07-03 09:02:02

Changamkieni teknolojia ya habari katika Uinjilishaji!


Askofu Bernadin Mfumbusa, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawahimiza wanahabari wakatoliki kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia katika sekta ya habari ili kuwatangazia watu Injili ya Furaha kwa uhakika Zaidi.

Askofu Mfumbusa ameyasema hayo, Jumatatu tarehe 30 Juni 2014 wakati alipokuwa anafungua warsha ya siku tatu ya mawasiliano kwa wajumbe kutoka katika Nchi za Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, kwenye Kitivo cha Mawasiliano ya Jamii, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania, SAUT, huko Msimbazi, Jijini Dar es Salaam.

Askofu Mfumbusa amewataka wanahabari Wakatoliki kwenda na wakati kwa kuchangamkia matumizi ya njia za mawasiliano ya kisasa, ili kuchangia kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Kanisa kwa miaka mingi Barani Afrika limekuwa nyuma katika matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii.

Umefika wakati kwa wanahabari wa Kikatoliki kutumia mitandao ya kijamii ili kuweza kupanua wigo wa mawasiliano na watu mbali mbali duniani. Askofu Mfumbusa anasema, leo hii kuna simu za kiganjani zipatazo billioni 5. 9 zinazotumika kila siku kukicha, njia hizi pia zinaweza kutumiwa na Kanisa Barani Afrika ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Kuna watu wengi Barani Afrika wanaoendelea kutumia mitandao ya kijamii, mapinduzi makubwa yanayojionesha Barani Afrika.

Warsha hii iliwahusu zaidi waandishi wa habari wanaotekeleza dhamana yao kwenye mitandao na imeandaliwa na Idara ya Mawasiliano ya Jamii, AMECEA na inawashirikisha wajumbe kutoka Sudan ya Kusini, Malawi, Zambia, Kenya, Uganda na Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.