Tanzania yampongeza Papa Francisko kwa kutetea amani duniani!
Askofu mkuu Francisco Montecillo Padila, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Jumatatu
tarehe 30 Juni 2014 ameadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, kwa
kufanya kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza
Kanisa Katoliki. Sherehe hii imehudhuriwa na Maaskofu Katoliki Tanzania waliokuwa
kwenye mkutano wao mkuu wa mwaka Jijini Dar es Salaam pamoja na viongozi mbali mbali
wa Serikali. Sherehe hizi zimefanyika kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania.
Katika
hotuba yake, Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe amelipongeza
Kanisa la Tanzania kwa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani,
upendo na mshikamano wa kitaifa kwa kukazia kwa namna ya pekee kabisa uhuru wa kuabudu!
Waziri Membe anasema hakuna amani ya kweli bila ya kuwa na uhuru wa kuabudu.
Serikali
ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika
ustawi na maendeleo ya watanzania wote katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.
Kanisa limeendelea pia kuhamasisha umuhimu wa watanzania kusimama kidete kuinda na
kutetea amani, kwa kuvumiliana na kuheshimiana katika tofauti zao, wakitambua kwamba,
wote ni watoto wa Mungu, tofauti zao ni utajiri mkubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya watanzania wote.
Waziri Membe anasema anakumbuka kwa namna ya pekee mahubiri
yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro wakati alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kukazia:
amani, utunzaji wa mazingira sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Anampongeza Baba Mtakatifu kwa kuwahamasisha
wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutumia ushawishi wao katika kujenga na kudumisha misingi
ya amani, upendo na mshikamano wa kimataifa sanjari na kuendeleza majadiliano ili
kweli amani na maridhiano kati ya watu yaweze kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu
ni mtu anayetekeleza kile anachokisema katika uhalisia wa maisha yake kama ilivyojionesha
wakati wa hija yake ya kitume katika Nchi Takatifu. Huko aliweza kukutana, kuzungumza
na kusali na waamini wa dini mbali mbali na hatimaye, hivi karibuni aliweza kuwaalika
Marais wa Israeli na Palestina mjini Vatican kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki
ya kati.