2014-07-02 10:00:14

Matumizi ya silaha ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu!


Mkutano wa tatu kimataifa uliokuwa unafanya tathmini ya mkataba wa kimataifa uliokuwa unapiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini uliokuwa unafanyika mjini Maputo, Msumbiji kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 27 Juni, 2014 umemalizika.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parorin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Mwenyekiti wa mkutano huo anasema kwamba, matumizi ya silaha ni kielelezo cha kushindwa kwa wote! Baba Mtakatifu ameonesha mshikamano wake wa dhati na nchi zilizoridhia mkataba huu, Mashirika ya Kimataifa, vyama vya kiraia na waathirika wa mabomu ya kutegwa ardhini kwani hawa ni wale ambao wanabeba mwilini mwao alama za silaha zilizotumika dhidi ya ubinadamu na kielelezo cha kushindwa kwa wote!

Baba Mtakatifu anasema, mkutano huu ulikuwa ni fursa kwa nchi zilizoridhia mkataba huu kuwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi, kwa kuwa na mikakati na maamuzi yatakatosaidia kuleta mabadiliko katika maisha ya watu wengi katika zile nchi ambazo mabomu ya kutegwa ardhini bado ni tishio, ni chanzo cha ukosefu wa usalama pamoja na kuenea kwa umaskini. Ardhi ambayo ingetumika kwa ajili ya uzalishaji bado ni chanzo kikuu cha hatari katika maisha, kiasi cha kuwanyima watu ile furaha ya kuishi na kujiendeleza.

Watu wanatafuta amani dhidi ya woga na wasi wasi na kwamba, mabomu ya kutegwa ardhini ni mwendelezo wa vita na wasi wasi hata baada ya amani na utulivu kupatikana, zote hizi ni dalili za kushindwa kwa mwanadamu kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya amani na matokeo yake, hofu inatanda kwa waathirika na watengenezaji wa mabomu haya.

Baba Mtakatifu anasema, amani ni furaha na matumaini yanayomwilishwa kila siku ya maisha, ili kujenga udugu na majitoleo kati ya watu wanaoshirikishana na kushirikiana katika kupinga chuki na hali ya kudhaniana vibaya. Waathirika wa mabomu ya kutegwa ardhini ni kielelezo tosha kabisa cha kushindwa kwa binadamu kulinda na kutetea misingi ya amani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kutafuta, kujenga na kudumisha amani, lakini zaidi kwa kuwalinda wanyonge ndani ya Jamii. Utu na heshima ya binadamu ni urithi wa wote, licha ya tofauti msingi zinazoweza kuonekana.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, utajiri wa kweli haufumbatwi kwa kulimbikiza mali, fedha wala silaha! Furaha ya kweli inabubujika kutoka katika upendo, ushirikiano na ukarimu kutoka moyoni. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuondokana na falsafa ya utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha na badala yake kutumia rasilimali hii kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na utunzaji bora wa mazingira, ili kujenga Jamii inayojipambanua kwa udugu na mshikamano licha ya tofauti msingi zilizopo, lakini zote hizi ni sehemu ya utajiri wa binadamu!

Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe kuendeleza na kuutunza mkataba huu kwa kuendelea kuwa waaminifu, ili kuhakikisha kwamba, hakuna tena mtu anayefariki dunia wala kuwa na wasi wasi kutokana na uwepo wa mabomu ya kutegwa ardhini. Mkataba huu uwe ni kielelezo na mfano wa mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa katika kudhibiti silaha na silaha za kinyukilia ambazo bado kimsingi ni tishio kubwa la maisha na usalama wa binadamu. Jumuiya ya Kimataifa iwekeze zaidi katika kulinda na kudumisha amani, usalama na utulivu.

Kwa kutekeleza mikataba ya kimataifa, Jamii inaweza kuondokana na wasi wasi wa chuki na uhasama na badala yake wananchi wajielekeze zaidi katika kudumisha misingi ya upatanisho, matumaini na mapendo, kwa ajili ya mafao ya wengi na ushirikiano wa kimataifa sanjari na kuibua sera na mikakati inayolinda utu na heshima ya binadamu, kwa ajili ya huduma kwa mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Mwenyekiti wa mkutano wa tatu uliokuwa unatathmini mkataba wa kupiga rufuku: utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini kwa kumpongea Mwenyekiti na wananchi wa Msumbiji katika ujumla wao! Mkutano huu umehudhuriwa na wajumbe 800 kutoka katika nchi 161 zilizoridhia mkataba huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.