Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa nchini Tanzania, hivi karibuni yaliadhimisha Kongamano
la Nne la Utoto Mtakatifu, lililofanyika Jimboni Tunduru Masasi. Tukio hili liliwakusanya
watoto wa Utoto Mtakatifu, walezi pamoja na Maaskofu kutoka Majimbo mbali mbali nchini
Tanzania.
Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania aliwataka watoto kusali
na kuendelea kuwa ni mabalozi na wajenzi wa misingi ya haki na amani. Sala za watoto
wadogo zinasikilizwa sana na Mwenyezi Mungu, kumbe ni wajibu wao kusali ili Mwenyezi
Mungu aweze kuwajalia walimwengu haki na amani, kwani kwa sasa watu wengi wanalilia
na kutamani amani ya kweli, ingawa pia kuna watu wanaoichezea amani kwa kuendekeza
mambo yasiyokuwa na mashiko wa tija kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wengi.
Askofu
mkuu Damian Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, aliwataka watoto wa Utoto Mtakatifu kuhakikisha
kwamba, wanatumia vyema akili, ujuzi na maarifa yao kuhusu Mungu kwa ajili ya maisha
yao kwa sasa na ustawi wa Kanisa na Tanzania kwa siku za usoni. Watoto wanawajibika
kutumia vyema muda na fursa zao mbali mbali kwa ajili ya maendeleo yao binafsi, Kanisa
na Jamii inayowazunguka na wala si vinginevyo.
Ni matumaini ya washiriki wa
kongamano hili kwamba, baada ya maadhimisho haya, Jamii itakuwa na mtazamo na mang’amuzi
bora zaidi katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watoto. Watoto ni matumaini ya
Kanisa na taifa kwa leo na kesho, hivyo wanapaswa kuheshimiwa, kulindwa, kuthaminia
na kupewa mahitaji yao msingi yanayojikita katika: elimu bora, afya, chakula, malazi,
mavazi na malezi makini. Watoto ni matumaini na jeuri ya Kanisa, ndiyo maana Kanisa
linaendelea kuwekeza kwa dhati kabisa katika maisha na utume wa watoto ili nao waweze
pia kuwa ni wadau wa Uinjilishaji miongoni mwa watoto wenzao.
Kwa upande wake,
Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda anasema, Kanisa litaendelea kusimama
kidete kulinda na kutetea ukweli, utu wema na maadili ndani ya Jamii. Askofu Nkwande
ameyasema hayo wakati alipokuwa anazungumza na walezi wa Mashirika ya Kimissionari
ya Kipapa nchini Tanzania. Anasema, Kanisa litaendelea kukazia umuhimu wa Jamii kudumisha
misingi ya maadili na utu wema; litakemea mmong’onyoko wa maadili kwa macho makavu
kabisa bila kusita wala kuogopa, kwa mambo yale yanayokwenda kinyume cha mpango wa
Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Askofu Nkwande anasema, Kanisa litaendelea
kupinga ndoa za watu wa jinsia moja, kwani mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha utu
na heshima ya binadamu; unakwenda kinyume na mila na tamaduni za Kiafrika na kwamba,
ni kinyume kabisa cha mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Kanisa Katoliki litaendelea kuwahimiza
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai
dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini au
Eutanasia. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu
na mwanadamu amekabidhiwa kulinda, kuitunza na kuiendeleza.
Kanisa linawahimiza
wazazi na walezi kutekeleza dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto
kadiri ya mafundisho ya Kanisa, mila na desturi njema za Kiafrika. Wazazi wawajibike
barabara katika malezi ya watoto wao na kamwe wasiachie mitandao ya kijamii kuwa ni
walezi mbadala baada ya wazazi kushindwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu.
Askofu
msaidizi Titus Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alipokuwa anatoa nasaha kwa wazazi
na walezi wa Utoto Mtakatifu kama sehemu ya maandalizi ya Kongamano la Utoto Mtakatifu
lililofanyika Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi alisema kwamba, hatima ya Kanisa na
taifa iko mikononi mwa familia zenyewe. Hii inategemea jinsi familia zinavyojihusisha
kwa malezi na makuzi ya watoto wao; kwa kuwajengea watoto hawa msingi wa tunu bora
za maisha na uchaji wa Mungu, wakitambua kwamba, wanapanda mbegu ya maisha ya kimissionari
kwa watoto hawa kwa siku za usoni.
Watoto waliofundwa na kufundika, ni msingi
bora wa Jamii inayowajibika na kusimamia mafao ya wengi. Watoto wapewe malezi bora,
waheshimiwe na kuthaminiwa na kamwe, wasidhulumiwe wala kunyanyaswa na watu waliokengeuka
na kupotoka kimaadili. Wazazi wawaonjeshe watoto wao fadhila ya imani, matumaini na
mapendo; watoto wao ni mwelekeo chanya wa maisha na kamwe wasiwe ni watu waliokata
tamaa kwani matokeo yake ni kutumiwa na baadhi ya watu katika jamii kusababisha kinzani
na uvunjifu wa amani, kama inavyojitokeza sehemu mbali mbali za dunia.
Naye
Padre Timoth Maganga, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa Jimbo kuu
la Dar es Salaam, anawataka wazazi kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao imani
na kweli za Kiinjili kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki. Licha ya kuhakikisha
kwamba, watoto wanapata elimu bora, afya njema, malazi na makazi bora, wawajengee
pia msingi bora wa maisha ya kiroho kwa kuwashirikisha fadhila ya imani, matumaini
na mapendo, ili kweli mwisho wa siku, watoto hawa waweze kuwa ni Wachamungu na raia
wema; watu wanaotegemewa na Jamii.
Wazazi waoneshe mifano bora kwa njia ya
ushuhuda wa imani katika matendo. Wajitahidi kupandikiza mbegu ya miito mbali mbali
katika maisha ya watoto wao. Watoto wanaoonesha nia ya kuwa Mapadre na Watawa wasaidiwe
na wazazi pamoja na walezi wao kutambua sauti ya Mungu katika maisha ya watoto hawa
kwa siku za usoni. Wazazi wajitahidi kukaa na kuishi na watoto wao, ili watoto hawa
mwisho wa siku waweze kupata ukomavu wenye uwiano bora katika maisha yao. Watoto wapate
malezi bora kutoka kwa Baba na Mama; Walimu na kutoka katika Kanisa kwa ujumla.
Kongamano
la Kitaifa la Utoto Mtakatifu hufanyika kila baada ya miaka miwili. Kwa mara ya kwanza
Kongamano hili lilifanyika Jimboni Iringa, likafuatia Jimbo Katoliki la Zanzibar na
Mwaka 2011 Jimbo Katoliki Ifakara likawa Mwenyeji wake.
Imehaririwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.