Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Baraza la Makardinali, Jumatano wameendelea na
kikao chao kadiri ya ratiba kwa kuangalia shughuli na utendaji wa mji wa Vatican kama
taarifa ilivyowasilishwa na Bertello na kuhusu Sekretarieti ya Vatican kama ilivyowasilishwa
na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baraza la Makardinali limepembua
tena hali na mwenendo wa Benki ya Vatican kwa kuwashirikisha Makardinali wanaosimamia
Benki hii ambao kwa sasa wako mjini Roma.
Akizungumzia kuhusu habari zinazoendelea
kusikika kwenye vyombo vya habari kuhusu Benki ya Vatican, IOR, Padre Federico Lombardi,
Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Benki ya Vatican iko katika kipindi cha
mpito na mageuzi yanayofanyika kwa hali ya utulivu. Mchango unaotolewa na Bwana Ernst
Von Freyberg ni muhimu na umepokelewa kwa mikono miwili. Bado kutakuwa na maelezo
zaidi baada ya kukamilika kwa Baraza la Kipapa la Uchumi, linalotarajia kufanya mkutano
wake, Jumamosi ijayo, baada ya mkutano huo, maendeleo zaidi yataweza kuwekwa hadharani.
Baraza
la Kipapa la Uchumi utawasilisha bajeti ya Vatican kwa mwaka 2013 - 2014. Juma lijalo,
kutakuwepo na mkutano mkubwa wa waandishi wa habari ili kuelezea kwa kina na mapana
yale yatakayojiri katika mkutano wa Baraza la Makardinali unaoendelea kwa sasa mjini
Vatican.