2014-07-01 09:43:15

Waonesheni walimwengu kwamba ninyi ni moto wa kuotea mbali!


Baba Mtakatifu Francisko, amewaandikia ujumbe wa matashi mema vijana kutoka Uholanzi waliokuwa wanashereheke Siku ya Vijana Kitaifa nchini humo, iliyofanyika mwishoni mwa Juma katika Abbasia ya Marienkroon, huko Niewkuijk, Den Bosch. Anawataka vijana kuonja ile furaha ya kweli na yenye mashiko inayotolewa na Yesu mwenyewe katika muhtasari wa mafundisho yake ya Heri za Mlimani.

Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu wa uholanzi kwa kuadhimisha Siku hii ambayo kimsingi inawasaidia vijana kuonja kweli za Kiinjili zinazotangazwa na Mama Kanisa. Maadhimisho haya kitaifa yameongozwa na kauli mbiu "Mkutano wa upya, usafi na kina", muhtasari wa Heri za Mlimani zinazopatikana katika Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo: 5: 3- 12.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani kwa kipindi cha miaka mitatu, wanaendelea kutafakari kuhusu Heri za Mlimani na kwamba, kilele cha tafakari hii kitafanyika Jimbo kuu la Cracovia, Poland kunako mwaka 2016. Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, Heri za Mlimani ni mafundisho ya kina ambamo vijana wanaweza kupata dira na mwelekeo wa maisha yao na kama sehemu ya mchakato wa kuendea furaha ya kweli kinyume na masikitiko na majonzi "yanayopigiwa debe" na walimwengu.

Kwa wale wanaotambulishwa kuwa ni Wenyeheri, kwa macho ya kidunia ni watu ambao wamepoteza dira, kwani dunia inawashabikia watu waliobahatika kupata mafanikio katika maisha hata kwa kupindisha ukweli; ni watu wenye fedha na mali, kiasi cha kuabudiwa; hawa ni wale wenye nguvu wanaopigiwa magoti kila siku, kiasi hata cha kuwanyanyasa jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Heri za Mlimani ni dira na mwelekeo wa kutaka kukumbatia Injili ya Uhai na furaha ya kweli katika maisha na kwamba, huu ni mwaliko wa kumwilisha Heri za Mlimani katika uhalisia wa maisha, ili kukutana na Yesu aliyekumbatia umaskini, akaonesha usafi wa moyo na huruma kama hija inayoelekea kwenye furaha ya kweli.

Hapa vijana wanahamasishwa kuanza mchakato wa kujifunza kuwa kweli ni wafuasi wa Yesu, kwa kumwilisha ujumbe huu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwaonesha walimwengu kwamba, wao kweli ni moto wa kuotea mbali; vijana wenye uwezo wa kupambana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkuu. Ujana pasi na imani, urithi wa kutunza, bila kusimamia ukweli, hakuna maisha, bali ni majanga tupu







All the contents on this site are copyrighted ©.