Wanawake simameni imara kupambana na nyanyaso za kijinsia!
Wachunguzi wa masuala ya nyanyaso dhidi ya wanawake katika maeneo ambamo mtutu wa
bunduki unaoekana kutawala zaidi wanabainisha kwamba, dini kwao ni sawa na upanga
wenye makali kuwili, katika baadhi ya maeneo ambamo dini inachukuliwa kama sehemu
ya siasa, viongozi wa kidini na taasisi zao hawakuwa na mchango madhubuti katika kuwasaidia
wanawake waliokumbwa na nyanyaso pamoja na dhuluma wakati wa vita na machafuko ya
kijamii.
Lakini utafiti
unaonesha kwamba, pale ambapo dini zimekuwa mstari wa mbele kuwasaidia waamini wao
katika mahangaiko wakati wa vita na machafuko ya kidini, zimekuwa msaada mkubwa katika
kuimarisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa wanawake, kiasi kwamba, wameendelea
kuwa kweli ni mashahidi wa imani tendaji. Kwa njia ya imani, wanawake hawa wameweza
kujikita katika mchakato wa kuponya madonda ya nyanyaso na dhuluma yaliyokuwa yamejificha
katika maisha yao!
Haya yamebainishwa hivi karibuni katika semina iliyoandaliwa
na Baraza la Makanisa Ulimwenguni na kuratibiwa na Dr. Fulata Lusungu Moyo. Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa katika maamuzi yake, linaendelea kuwahamasisha wanawake
kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki na amani katika
maeneo ambamo vita na machafuko ya kijamii yameshamiri kwa muda mrefu. Kwa njia hii
wanaweza kusaidia ujenzi wa haki jamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia. Katika vita
na machafuko ya kijamii, wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi.
Majukwaa
ya kijamii na vyama vya kiraia ni fursa nzuri kwa wanawake kuweza kujipanga vyema
kukabiliana na mustkabali wa maisha yao kwa pamoja, kwani umoja ni nguvu na utengano
ni udhaifu. Mafanikio haya yamejionesha kwa namna ya pekee kwa vyama vya wanawake
Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita. Mahali ambapo wanawake
wanashirikishwa kikamilifu katika kupanga na kuamua hatima ya maisha ya kijamii, wamekuwa
mstari wa mbele katika kupigania na kutetea haki msingi za wanawake katika Jamii.
Ni wanawake wanaotaka kuona kwamba, jamii inajengeka katika misingi ya usawa,
haki na kuheshimiana, ndiyo maana kuna umuhimu pia wa kujenga na kudumisha majukwaa
ya majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa wanawake, ili kwa pamoja licha
ya tofauti zao za kiimani, waweze kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima
ya wanawake wote, tayari kujifunga kibwebwe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu
wao.
Uponyaji wa madonda ya nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa wanawake katika
maeneo ya vita na machafuko ya kijamii ni mchakato unaojikita katika hija ya maisha
ya mtu binafsi kiroho pamoja na kushirikishana na wengine katika vyama na majukwaa
ya kijamii.