Patriaki Bartolomeo wa kwanza, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro
na Paulo, Mitume iliyoadhimishwa Jumapili tarehe 29 Juni 2014, amemwandikia ujumbe
wa matashi mema, Baba Mtakatifu Francisko akimwomba kutunza na kuhifadhi katika mioyo
yao, matukio makuu yaliyowakutanisha hivi karibuni huko Yerusalemu na Roma, kiasi
kwamba, wameimarisha urafiki na udugu pamoja na kuendeleza utashi wa kuwa na umoja
kamili kadiri ya mapenzi ya Yesu Kristo mwenyewe.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza
anakumbuka hija ya kitume iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu,
kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Patriaki Anathegoras na Paulo
VI walipokutana na kusali pamoja, huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya
kiekumene. Anamshukuru kwa kuonesha ujasiri wa kuitisha mkutano kwa ajili ya kuombea
amani huko Mashariki ya Kati. Hili ni tukio ambalo liliwakutanisha Marais kutoka Israeli
na Palestina, kiasi cha kuwaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi!
Patriaki
Bartolomeo wa kwanza anamwombea Baba Mtakatifu, afya ya roho na mwili, ili aweze kuendelea
kutekeleza dhamana na utume wake kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake,
akiwaonjesha watu karama na upendo wake kwa Mungu na jirani!