Papa kutembelea Jimbo la Molise, tarehe 5 Julai 2014
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 5 Julai 2014 anatarajiwa kutembelea Jimbo
Katoliki la Molise, lililoko Kusini mwa Italia. Hii itakuwa ni mara yake ya tano kutembelea
Majimbo Katoliki nchini Italia. Atakapowasili Jimboni humo atazungumza na wafanyakazi
kutoka katika Mkoa wa Molise, baadaye saa 4:30 asubuhi ataadhimisha Ibada ya Misa
Takatifu na baadaye atakwenda kwenye Kanisa kuu ili kusalimiana na wawakilishi wa
wagonjwa kutoka Molise.
Kama kawaida, Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana
na maskini wanaohudumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Campobasso na baadaye
atakutana na vijana wa kizazi kipya kutoka Abruzzo na Molise. Baba Mtakatifu, baadaye
ataelekea mjini Isernia anakotarajiwa kukutana na kuzungumza na wafungwa wanaotumikia
adhabu zao mbali mbali gerezani humo. Akiwa mjini humo atakutana na kusalimiana na
wagonjwa. Jioni, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na wananchi wa Isernia na hapa
atatangaza Mwaka wa Jubilee ya Celestini.
Baada ya shughuli zote hizi, Baba
Mtakatifu anatarajiwa kurejea tena Vatican kuendelea na kipindi chake cha mapumziko
na kazi! Kama kawa, Idhaa ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega kukuza yale
yanayojiri katika matukio kama haya!