Uchaguzi Serikali za mitaa Tanzania ni kitendawili!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yanaendelea japo kwa kiasi kikubwa
hatma yake inategemea kukamilika kwa mchakato wa Katiba mpya. Ametoa kauli hiyo
Jumatatu, Juni 30, 2014 wakati akizungumza na Mameya wa Majiji, Manispaa na Wenyeviti
wa Halmashauri za Miji na Wilaya Tanzania katika kikao cha siku moja kilichofanyika
kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga.
Waziri Mkuu yuko Tanga kwa ajili
ya sherehe za Serikali za Mitaa ambayo kilele chake kitafanyika kesho Julai mosi kwenye
uwanja wa Tangamano jijini hapa. Ameamua kukutana na viongozi hao ikiwa ni utekelezaji
wa ahadi ya kukutana nao aliyoitoa Mei 14, 2014 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa ALAT.
"Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bado ni kitendawili kwa sababu kwa kiasi kikubwa inategemea
sana kukamilika kwa Mchakato wa Bunge la Katiba," alisema na kuongeza: "Kama Wizara
tunaendelea na maandalizi tukiamini uchaguzi upo, kama hiyo fursa isipotokea bado
tutakuwa tumekamilisha maandalizi kwa upande wetu.Tunaendelea kuandaa kanuni kwa kushirikisha
wadau wote," alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la
ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali. Kuhusu mapato, Waziri
Mkuu alisema katika mwaka wa fedha wa unaoisha sasa, hali ya ukusanyaji mapato haikuwa
nzuri. Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu alisema amewaandikia barua Wakuu wa Mikoa
akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya makusanyo
ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.
"Katika taarifa hizi itabidi
kila Halmashauri ieleze ilipanga kukusanya kiasi gani, je imefikia lengo na kama sivyo
ni kwa nini. Nia yetu ni kutrack down makusanyo na kuona yamekwama wapi na yamekwamishwa
na nini," alisema. Kuhusu udhibiti wa matumizi, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti
hao kuendelea kuwabana wahusika ili kudhibiti matumizi yasiyofaa. "Lazima muendelee
kuwabana na kuwasimamia wakurugenzi na wataalaam wa kwenye Halmashauri zenu. Fanyeni
kazi kwa ufanisi, msiwachekee wale wanaoharibu," aliongeza.
"Ili muweze kuwabana
vizuri, ni lazima mdai kupatiwa taarifa za fedha kutoka kwa Mkaguzi wa Ndani (Internal
Auditor)... kuna baadhi ya watendaji wanadai kuwa hizi taarifa ni siri wakati siyo
siri," alisema. Aliwaeleza washiriki wa kikao hicho kwamba taarifa hizo ni muhimu
kwao kuzipata na zitawasaidia kuonyesha mapungufu yoyote kama yapo. Aliwataka kila
mmoja wao kwa nafasi zao za Meya na Mwenyekiti wahakikishe wanalenga kupandisha pato
la wananchi wanaowaongoza.