2014-06-30 09:18:09

Shuhudieni imani katika matendo!


Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican anawataka waamini kuonesha ujasiri na ari kwa kumshuhudia Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Anawashukuru waamini ambao daima wamekuwa mstari wa mbele katika kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao. RealAudioMP3

Askofu mkuu Mamberti ameyasema haya hivi karibuni katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya wanachama wa Chama cha Watakatifu Petro na Paulo pamoja na kupokea ahadi kwa wanachama wapya waliojiunga na Chama hiki, kwa kuwataka kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma.

Askofu mkuu Mamberti anawataka wanachama kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na kwa njia hii watakuwa na ujasiri wa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kumshuhudia kati ya watu. Hapa mambo mawili yanakwenda sambamba, yaani imani na uaminifu kwa Mungu kama msingi wa huduma makini inayotolewa na wanachama hawa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kujenga na kuimarisha Kanisa la Kristo.

Askofu mkuu Mamberti anawaalika wanachama hao kuwashirikisha hata vijana katika mchakato wa huduma kwa maskini, ili kuendeleza utume huu hata kwa siku za usoni, kwani ni huduma inayojielekeza zaidi katika maisha ya kiroho na kitamaduni. Watambue kwamba, Baba Mtakatifu anathamini sana mchango na huduma wanayoitoa kwa niaba ya Kanisa, katika unyoofu, ukarimu na sadaka ya mambo mengi katika maisha.

Askofu mkuu Mamberti anawashukuru wanachama hawa kwa mapokezi mazuri wanayoyafanya kwa waamini na mahujaji wanaomiminika kila siku kusali na kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; kwa kusimamia na kuratibu ibada zinazoadhimishwa ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro bila kusahau huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu wote ni ushuhuda wa huduma ya mapendo kwa Kristo na Kanisa lake.

Askofu mkuu Mamberti anawataka wanachama hao kuendeleza moyo wa upendo na ukarimu kwa watu wanaokutana nao katika huduma, ili waweze kubaki na picha yenye kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Hii ni huduma inayowataka kuonesha ukarimu wa pekee, uvumilivu na heshima kwa watu, weledi, lakini zaidi, ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika matendo.

Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, baadhi ya wanachama wamepewa tuzo ya heshima kutokana na kujipambanua zaidi katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.