Serikali na Kanisa vishirikiane kwa ajili ya mafao ya wengi!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 30 Juni 2014 amekutana na kuzungumza na
Mfalme Felipe VI na Malkia Letizia wa Hispania mjini Vatican, baadaye wamekutana na
kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana
na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican.
Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na wageni
wake, Mfalme Felipe VI amesema hii ni safari yao ya kwanza nje ya Hispania kama mwendelezo
wa safari kama hii iliyofanywa na Mfalme Juan Carlos I na Malkia Sofia kunako tarehe
28 Aprili 2014, kama sehemu ya mchakato unaopania kuimarisha ushirikiano kati ya Vatican
na Hispania.
Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu na mgeni wake wamegusia
mambo mbali mbali, lakini zaidi umuhimu wa majadiliano na ushirikiano kati ya Kanisa
na Serikali, kwa ajili ya mafao ya wananchi wote wa Hispania. Wamegusia pia matatizo
yanayoendelea kujitokeza katika ngazi ya kikanda na kimataifa hasa katika maeneo ambayo
mtutu wa bunduki unaendelea kutawala!