Askofu mkuu Franco Coppolla aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko
kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, hivi karibuni
aliwasili nchini humo na kupokelewa na viongozi wa Kanisa Afrika ya Kati.
Baadaye, Askofu
mkuu alipeleka nakala za hati zake za utambulisho kwa Waziri wa Mawasiliano na Upatanisho
wa Kitaifa toka Jamhuri ya Afrika ya Kati Bwana Antoinette Montaigne anayekumbuka
kwamba, tarehe 29 Juni 2013 alishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa
na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati
alipokuwa anatoa Palio Takatifu kwa Maaskofu wakuu, mmoja wapo akiwa ni Askofu mkuu
wa Jimbo kuu la Bangui.
Baadaye Askofu mkuu Coppola aliwasilisha pia hati zake
za utambulisho kwa Rais Catherine Samba-Panza, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya
Kati aliyekuwa ameambatana na viongozi wakuu waandamizi nchini humo.
Rais
Samba-Panza amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kujali mateso na mahangaiko ya
wananchi wa Afrika ya Kati, ambao wamepitia kipindi kigumu cha vita ya wenyewe kwa
wenyewe pamoja na misigano ya kijamii iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali
zao. Anashukuru pia mchango mkubwa uliofanywa na Kanisa Katoliki katika kuwahudumia
wananchi waliokuwa wamepoteza matumaini kutokana na vita.
Kwa upande wake,
Askofu mkuu Franco Coppola anasema, Kanisa Katoliki, litaendelea kushikamana kwa dhati
na wananchi wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kujenga na kudumisha misingi ya
haki, amani na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya mafao ya wengi.
Askofu
mkuu Coppola, aliwasilisha nakala za hati zake za utambulisho kutoka kwa Kardinali
Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga, Rais
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.