Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican, Jumapili tarehe 29 Juni 2014, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza
mawazo yake huko Iraq ambako habari za kusikitisha na kutia uchungu na simanzi zinaendelea
kusikika kila kukicha!
Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuungana na Maaskofu
mahalia kuwataka viongozi wa Serikali kuanzisha mchakato wa majadiliano, ili umoja
na mshikamano wa kitaifa uweze kutawala na hatimaye, kushinda kishawishi cha kutaka
kujitumbukiza katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Baba Mtakatifu Francisko
anasema kwamba, yuko karibu na familia zote zinazoteseka nchini Iraq, lakini kwa namna
ya pekee kabisa yuko karibu na Familia za Kikristo ambazo zinalazimika kuyahama makazi
yao kutokana na hatari inayowazunguka. Vita inazaa vita nyingine, majadiliano ni njia
pekee ya ujenzi wa misingi ya amani.
Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasalimia
ndugu, jamaa, marafiki na waamini waliohudhuria kwenye Ibada ya Misa Takatifu ili
kuwasindikiza Maaskofu wakuu 27 waliovishwa Pallio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican. Anawapongeza wasanii waliopamba mji wa Roma kwa maua kama sehemu
ya maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, wasimamizi wa Roma.
Anawashukuru
waamini wote wanaoshiriki kwa ukarimu kuchangia Mfuko wa Ukarimu wa Papa kwa ajili
ya kuwasaidia watu wanaokumbwa na majanga mbali mbali katika maisha. Anawatakia kheri
na baraka wanaojibidisha kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kituo cha michezo katika
Nchi Takatifu.