2014-06-29 14:34:03

Mnaitwa kumfuasa Kristo Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko katika sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, Jumapili tarehe 29 Juni 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu ishirini na saba, kati yao sita kutoka Barani Afrika na Maaskofu wakuu watatu hawakuweza kuhudhuria Ibada hii, kwa hiyo, Pallio zao watapewa na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ametambua uwepo wa ujumbe wa kiekumene kutoka kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika Ibada hii ulioongozwa na Askofu mkuu Ioannis kama sehemu ya mchakato wa kuendelea kuimarisha hija ya kidugu kati ya Wakristo ili hatimaye, kuweza kufikia lengo la umoja kamili, hamu ya Makanisa haya mawili.

Baba anasema, Mtakatifu Petro alipoanza utume wake kwenye Kanisa la mwanzo mjini Yerusalemu kulikuwa na wasi wasi na woga kutokana na madhulumu ya Mfalme Erode dhidi ya Kanisa. Aliwafurahisha wananchi kwa mauaji ya Mtume Yakobo na baadaye alimtupa gerezani Mtakatifu Petro, lakini akaokolewa na mkono wa Malaika, matendo makuu ya Mungu na kwamba, Mungu anaweza kuwaokoa waja wake kutoka katika woga na wasi wasi na kila aina ya minyororo, ili kuwaweka kweli huru, hiki ndicho kiini cha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo anasema Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawauliza Maaskofu wenzake, Je, wanaogopa nini katika maisha na shughuli zao za kichungaji? Ni wapi wanapokimbilia ili kupata faraja na usalama wa maisha yao? Je, wanapata hifadhi kwa wakuu wa dunia na watu wenye mamlaka? Je, wanamezwa na kiburi pamoja na mafanikio wanayopata, kiasi cha kuwafanya kujisikia kuwa huru zaidi? Baba Mtakatifu anawauliza Maaskofu, Je, ni wapi wanapokita usalama wao?

Ushuhuda wa Mtakatifu Petro unawakumbusha kwamba, imani kwa Mwenyezi Mungu ndilo kimbilio lao la kweli, kwani ana nguvu ya kuwaondolea woga na kuwaweka huru kweli kutoka katika utumwa na vishawishi vya dunia hii. Maaskofu wakuu na wale waliovikwa Pallio Takatifu wanahamasishwa kufuata mfano bora wa maisha kutoka kwa Mtakatifu Petro sanjari na kuhakiki imani yao kwa Mwenyezi Mungu.

Mtakatifu Petro baada ya kuulizwa mara tatu na Yesu, ikiwa kama kweli alikuwa anampenda, anaambiwa kuchunga na kulisha Kondoo wa Yesu. Hapa Mtakatifu Petro aliweza kuungama hadharani upendo wake kwa Kristo mara tatu na hivyo kurekebisha kile kitendo cha Mtakatifu Petro kumkana Yesu mara tatu wakati alipokuwa anasulubiwa. Tukio hili liliacha madonda makubwa katika moyo wa Mtakatifu Petro, wakati huu, Petro anatambua mapungufu yake ya kibinadamu na kujiachilia ili kuongozwa na huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani na hapa woga, wasi wasi na ukosefu wa usalama vinatoweka mara moja.

Mtakatifu Petro anang'amua kwamba uaminifu wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko mapungufu yake ya kibinadamu yaliyompelekea hata akamkana Yesu mara tatu. Uaminifu wa Mungu unafukuzia mbali wasi wasi na uwezo wa mwanadamu kufikiri. Hata leo hii, Yesu anaendelea kuwauliza wafuasi wake, Je, mnanipenda? Lengo ni kung'amua wasi wasi na magumu ya maisha wanayokabiliana nayo kila siku, ili kuweza kujiachilia mikononi mwa Mungu anayefahamu yote na kujiaminisha kwake Yeye ambaye ni mwaminifu daima na kamwe hawezi kuwaacha kamwe!

Baba Mtakatifu anasema, uaminifu wa Mungu unawaimarisha Wachungaji kinyume kabisa cha uwezo, imani na huduma kwa Mungu na jirani katika upendo. Upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu unamtosha Mtakatifu Petro na wala hana sababu ya kuwa na wivu usiokuwa na mashiko, bali kupiga moyo konde na kumfuasa Kristo kwa ari na ujasiri mkuu zaidi. Mang'amuzi haya ya Mtakatifu Petro ni muhimu sana hata kwa Maaskofu wakuu leo hii!

Yesu leo hii anaendelea kuwaita wote kumfuasa, hakuna sababu ya kupoteza muda kwa udadisi usiokuwa na mashiko, au kwa kushikamana na mambo mpito na badala yake kujikita katika mambo msingi na kumfuasa Yesu, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika maisha na utume wao. Wanaitwa kumfuasa Yesu kwa njia ya kuhubiri, kushuhudia kwa maisha ya neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na Daraja Takatifu, kumnadi Yesu katika vipaumbele, uhalisia na majadiliano ya maisha.

Wanaitwa kumfuasa Yesu katika mchakato wa utangazaji wa Injili ya Furaha hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kwamba, asiwepo hata mtu mmoja anayekosa Neno la uzima linalomkomba mwanadamu kutoka katika woga kwa kumkirimia uaminifu kwa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.