2014-06-29 08:29:31

Fanyeni maamuzi magumu!


Katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, Jumamosi, tarehe 28 Juni 2014, Baba Mtakatifu Francisko jioni, alikutana na kuzungumza na waseminari ambao wako katika hija ya maisha ya Kipadre, wanataka kujisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mungu Injili ya Furaha. Haya ni mapokeo yaliyoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI wakati wa uongozi wake na yanaendelezwa kwa ari na kasi mpya kwa sasa na Papa Francisko!

Ujumbe wa Majandokasisi kutoka Roma uliongozwa na Kardinali Agostino Vallini, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma, ambao ulikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Pango la Bikira Maria wa Lourdes, kwenye Bustani za Vatican, ikumbukwe kwamba, kwa sasa hapa Roma, jua linawaka bila utani!

Baba Mtakatifu akizungumza na Majandokasisi hawa aliwakumbusha hija ya maisha ya kiroho iliyotekelezwa na Bikira Maria hata akadiriki kusimama chini ya Msalaba, huyu ndiye Mama anayewasindikiza hata wao katika safari ya maisha ya wito wao wa Kikasisi. Anawataka Waseminari hawa kujenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria ili kwa njia ya shule ya Bikira Maria waweze kumjifunza, kumfahamu na kumpenda Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kielelezo na ushuhuda wa maisha yao.

Mkristo asiyekuwa na Ibada kwa Bikira Maria ni mpweke na yatima! Mkristo anamhitaji Bikira Maria na Mama Kanisa, ili kupima kiwango cha maisha na wito wa Mkristo. Wakristo wachunguze mahusiano yao na Bikira Maria pamoja na Kanisa. Majandokasisi wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu ana mpango maalum wa maisha kwa kila mmoja wao, jambo la msingi ni kutafuta ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anataka kumtumia kwa ajili ya kazi zake, changamoto ya kuwa na mipango thabiti ya maisha na wala si kufanya mambo kwa pupa!

Maamuzi watakayofanya yawe ni maamuzi ya kudumu na wala si mambo ya mpito! Wakiamua kuwa Mapadre au Watawa wawe kweli ni Mapadre na Watawa wema na watakatifu, watu wanaotambua kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani. Ikiwa kama kijana anataka kufunga ndoa, basi atambue kwamba, huu ni upendo wa kudumu kwani kile alichounganisha Mungu, mwanadamu hana uwezo wa kukifungua! Hapa hakuna upendo wa mpito! Kuna haja ya kufanya mamuzi magumu katika maisha wala hakuna cha "maji kwa glasi".

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni amekiri kwamba, Yeye hajui kuimba, hivyo amewaomba Majandokasisi na wote waliokuwepo pale, kuimba kwa pamoja wimbo wa "Salve Regina". Salam Malkia. Baada ya kusali na kuimba, Baba Mtakatifu aliwapatia baraka zake za kitume, Majandokasisi, wakarudi huku nyoyo zao zimesheheni furaha kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.









All the contents on this site are copyrighted ©.