Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo P. Pinda (MB), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wakati wa kuhitimisha mkutano wa kumi na tano wa bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania tarehe 28 Juni, 2014.
UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Spika,
1. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema
kwa kutupatia uzima na afya hadi kufikia siku ya leo. Tumekuwepo hapa kwa takriban
miezi miwili ambapo tumeweza kupokea na kujadili Taarifa za Mapitio ya Utekelezaji
wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa mwaka 2014/2015 kwa Wizara
mbalimbali na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015.
2.
Napenda kutumia nafasi hii ya awali kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi
nzuri ya kutukuka ambayo wameifanya kwa nidhamu na ufanisi mkubwa, hususan wakati
wa Mjadala wa Bajeti ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta. Kipekee niwashukuru
Wajumbe wa Kamati ya Bajeti chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mtemi Andrew John
Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi kwa kazi yao nzuri ya kuchambua Bajeti
ya Serikali na Sheria zinazoambatana na masuala ya Bajeti. Changamoto zilikuwa nyingi,
lakini kwa pamoja tumekubaliana na kuafikiana. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kwenda
kushirikiana na Wananchi katika utekelezaji wa Bajeti hii ili kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa
Spika,
3. Katika kipindi hiki tukiwa hapa Bungeni, yapo matukio ya kusikitisha
yaliyotokea ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipoteza Wapendwa wao. Aidha, yapo
matukio ya Kitaifa yaliyosababisha kupoteza maisha ya Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda
kutumia nafasi hii kuwapa pole Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote waliofikwa na
misiba na majanga mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wote waliopotelewa na Ndugu, Jamaa
na Marafiki.
Mheshimiwa Spika, 4. Kipekee niwape pole ndugu, jamaa na
marafiki waliopotelewa na ndugu zao na wote waliopata majeraha wakati kulipotokea
Mlipuko wa Bomu pale Darajani, Zanzibar. Tukio hili la kusikitisha halipendezi kwa
Nchi yetu. Niwaombe Wananchi wote kwa umoja wetu tushirikiane kuwa Walinzi katika
maeneo yetu na kuwezesha kuwatambua mapema wale wote wenye nia mbaya ya kuharibu amani
na utulivu katika Nchi yetu.
b) Shughuli za Bunge
Mheshimiwa
Spika,
5. Katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kufanya
uchaguzi wa Wajumbe wa Wawakilishi kwenye Bodi za Taasisi, Mabaraza na Tume za Bunge.
Napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Terezya Luoga Huvisa, Mbunge
wa Viti Maalum kuwa Mjumbe katika Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere;
Mheshimiwa Goodluck Joseph Ole-Medeye, Mbunge wa Arumeru Magharibi kuwa Mwakilishi
wetu katika Bunge la Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC-PF); Mheshimiwa
Alphaxard Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara kuwa Mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge;
Mheshimiwa Henry Daffa Shekifu, Mbunge wa Lushoto; Mheshimiwa Sylvester Massele, Mbunge
wa Dole; na Mheshimiwa Zainab Rashidi Kawawa, Mbunge wa Viti Maalum wote kuwa Wajumbe
katika Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Beatrice
Matumbo Shelukindo, Mbunge wa Kilindi na Mheshimiwa Dkt. Maua Abeid Daftari, Mbunge
wa Viti Maalum kuwa Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi – Muhimbili;
na mwisho nimpongeze Mheshimiwa Rashid Mfutakamba, Mbunge wa Igalula kuwa Mjumbe wa
Bodi ya Utawala ya Chuo cha Ufundi Arusha. Tunaamini wote waliochaguliwa watatuwakilisha
vyema katika Taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika,
6. Pamoja na kupokea,
kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, jumla ya Maswali 321 ya Msingi na 879 ya
Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali
37 ya Msingi na 30 ya Nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Papo kwa Papo
kwa Waziri Mkuu.
7. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote kwa kuuliza Maswali ambayo yalilenga katika kuwaletea Wananchi maendeleo katika
Majimbo yetu na kwa Taifa letu kwa ujumla. Vilevile, niwapongeza Mawaziri na Naibu
Mawaziri wote ambao wamefanya kazi kubwa ya kuandaa majibu na maelezo ya ziada katika
kila Swali lililoulizwa.
c) Miswada, Maazimio na Kauli za Serikali
Mheshimiwa
Spika,
8. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili
Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali
na kukamilisha hatua zote ni Muswada wa Sheria wa Fedha wa Mwaka 2014 [The Finance
Bill 2014]; na Muswada wa Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2014
[The Appropriation Bill, 2014].
Mheshimiwa Spika,
9. Miswada ifuatayo
imesomwa kwa mara ya kwanza:
i) Muswada wa Sheria wa Kufanya Marekebisho
katika Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa 2014 [The Public
Private Partnership (Amendment) Act, 2014] ulisomwa kwa mara ya kwanza.
ii)
Muswada wa Sheria ya Utawala wa Kodi 2014 (The Tax Administration Act 2014);
iii)
Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali [Miscellaneous (Amendments)
Bill 2014]; na
iv) Muswada wa Sheria Mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
[The Value Added Tax Act, 2014] unaopendekeza kufuta Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani.
d) Maazimio
Mheshimiwa Spika,
10. Vilevile,
katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge pia walikubali Maazimio ya Bunge kama ifutavyo:
i)
Azimio la kuridhia kubadilisha Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwa Taasisi inayojitegemea
kiutendaji [Tengeru Institute of Community Development (Establishment Order, 2013)];
ii)
Azimio la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Fedha na Uwekezaji (SADC Protocal on Finance
and Investment);
iii) Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kuanzisha Umoja wa
Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki [Protocol on the Stablishment of the East African
Community Monetary Union].
Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
11.
Katika Mkutano huu pia Mawaziri waliweza kutoa Kauli za Serikali zifuatazo: i)
Kauli ya Waziri wa Maji Kuhusu Matatizo ya Uzalishaji Maji katika Mtambo wa Maji wa
Ruvu Juu;
ii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Ugonjwa
wa Homa ya Dengue;
iii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Hali
ya Mashine za Mionzi za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).
SERIKALI
ILIVYOJIPANGA KUTEKELEZA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa
Spika,
12. Wakati wa Mjadala wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015;
Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu Sera
na Mikakati iliyopangwa na Serikali ya kuimarisha maandalizi na usimamizi wa utekelezaji
wa Mpango na Bajeti ya Serikali. Tunashukuru kwa michango hiyo mizuri ambayo Serikali
inaahidi kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,
13. Napenda kutumia fursa
hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge wengine kuwapongeza Mheshimiwa Stephen Masato
Wasira (Mb.) - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu; na Mheshimiwa Saada
Mkuya Salum (Mb.) - Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha vizuri Hotuba za Mpango na Bajeti
ya Serikali na pia kutoa maelezo mazuri ya ufafanuzi wakati wa kuhitimisha Hoja hii
tarehe 24 Juni 2014. Vilevile, nawapongeza Mawaziri wa Kisekta na Naibu Mawaziri kwa
kuwasilisha Bajeti za Wizara zao kwa umahiri mkubwa. Pamoja na pongezi hizo, napenda
kutoa msisitizo katika maeneo machache yafuatayo:
a) Kuimarisha utengemavu
wa Viashiria vya Uchumi Jumla
Mheshimiwa Spika,
14. Ukuaji wa uchumi
jumla ulio endelevu unahitaji mazingira ya uchumi jumla yaliyotengamaa na yanayotabirika.
Mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukiongezeka na
kufikia wastani wa Asilimia 7 kwa mwaka licha ya changamoto za upandaji bei za chakula
na mafuta ya petroli katika soko la dunia. Ili kuweza kuendeleza ukuaji huu mzuri
wa uchumi hapana budi kuendelea kutengamaza vigezo muhimu vya uchumi jumla, ikiwa
ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha Ukuaji halisi wa Pato la Taifa na kukua kwa
kiwango cha juu zaidi ya Asilimia 7.0; kudhibiti kasi ya upandaji bei kwa kuhakikisha
kwamba kiwango cha mfumuko wa bei ni chini ya tarakimu moja, ikiwezekana kisichozidi
Asilimia 5; na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi. Kutengamaza
viashiria hivi kutaihakikishia Nchi yetu kuendelea kwa kasi katika kukuza uchumi na
kupunguza umaskini hasa ule wa kipato kwa Wananchi wetu wengi wa Vijijini. Tayari
dalili nzuri zinaanza kujitokeza, kwani kiwango cha Watanzania walio katika umaskini
kimepungua kutoka Asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi Asilimia 28.2 mwaka 2012. Aidha, wastani
wa Pato la Mwananchi kwa mwaka limeongezeka kutoka Shilingi 516,000 mwaka 2007 hadi
Shilingi 1,003,000 mwaka 2012.
b) Kuimarisha utaratibu na usimamizi wa
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
15.
Mwaka 2014/2015, ni wa Nne wa utekelezaji wa Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011/2012 – 2015/2016). Ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango unafikia malengo
yaliyokusudiwa, Serikali imeiagiza Tume ya Mipango kuendelea na utaratibu wa kukagua
na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleo ya kipaumbele na
ile ya kimkakati ili kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora
vilivyokubalika na inalingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali (Value
for money). Vilevile, kuhakikisha kuwa Miradi hiyo inakamilika kwa wakati; na pale
ambapo kuna changamoto za kiutekelezaji kutoa ushauri stahiki Serikalini wa njia za
kufanikisha miradi husika. Kwa upande wa miradi inayotekelezwa katika ngazi za Sekretariati
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu
– TAMISEMI, Serikali itaimarisha mfumo wa ufuatiliaji kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana
katika mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” (Big Results Now – BRN).
Mheshimiwa
Spika,
16. Sambamba na hatua hizo, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu
kuwa, Serikali imeanza kufanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011/2012 – 2015/2016). Lengo la mapitio hayo ni kupima hatua ya utekelezaji
wa mpango na kubaini changamoto pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya Mpango
wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Taarifa ya mapitio ya
Nusu ya Kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 –
2015/2016), itatolewa Desemba 2014. Madhumuni ya Taarifa hii ni kuhakikisha kuwa maeneo
ambayo hayakutekelezwa ipasavyo na maeneo mapya yaliyoibuka (emerging issues) hususan
kuiandaa nchi kwa uchumi wa gesi na umuhimu wa kuimarisha ushindani wa Tanzania katika
uzalishaji na biashara ya Kimataifa.
c) Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji
wa Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
17. Kutokana na michango mizuri
ya mawazo ambayo Serikali imepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa Mjadala
wa Bajeti ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta, Serikali imejipanga vizuri
zaidi kuimarisha ukusanyaji wa Mapato katika Mwaka 2014/2015. Hata hivyo, ni vyema
Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kwenye eneo la mapato yanayokusanywa na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali ya awamu ya nne imefanikiwa kuongeza mapato hayo
kutoka Wastani wa Shilingi Bilioni 117 kwa mwezi Mwaka 2005/2006 hadi Wastani wa Shilingi
Bilioni 800 kwa Mwezi mwaka 2013/2014. Ongezeko hilo ni sawa na Asilimia 351. Lengo
la Serikali ni kuongeza kasi zaidi katika eneo hili hata kuzidi kiwango hiki.
Mheshimiwa
Spika,
18. Pamoja na kuipongeza TRA kwa jitihada hizo, Serikali itafanyia kazi
maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ya kupanua wigo wa vyanzo vya Kodi pamoja
na taarifa zilizopatikana zinazoonyesha kwamba bidhaa nyingi zinapita kwenye bandari
bubu au vituo vya forodha bila kulipakodi stahiki. Hatua za kupunguza misamaha ya
Kodi zitaendelea kuimarishwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuielekeza Mamlaka
ya mapato Tanzania kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuimarisha zaidi miundo ya ukusanyaji
na ulipaji kodi. Ni muhimu, Mamlaka ya Mapato kurahisisha zaidi taratibu za kukusanya
Kodi kwa kuweka na kutangaza kwa uwazi Kodi zinazostahili kulipwa kulingana na aina
ya bidhaa na kuondokana na utaratibu wa kufanya makadirio au kutumia mwanya wa majadiliano
na walipa kodi jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa rushwa na hivyo kuikosesha Serikali
Mapato yake stahiki. Vilevile, naviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoa ushirikiano
wa kutosha katika kudhibiti na kuzuia ukwepaji wa kodi na ushuru katika bandari zetu
na maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa Spika,
19. Ni imani yangu kuwa
tukiweka wazi kodi zinazopaswa kulipwa na tukirahisisha taratibu za kukusanya Mapato
ya Kodi hususan Bandarini na maeneo ya mipakani tutaweza kuweka mazingira mazuri ya
kusaidia kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza urasimu na vishawishi vya kudai
Rushwa. Nashauri, Mamlaka ya Mapato Tanzania ijipange upya vizuri ili kuhakikisha
kwamba jukumu la kukusanya kodi linatekelezwa vizuri na kwa weledi mkubwa. Tukiwa
na uhakika wa makusanyo ya mapato yetu ya ndani, naamini tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa
Spika,
20. Kuhusu mapato yasiyotokana na Kodi hususan Maduhuli, uzoefu wa mwaka
2013/2014 umeonesha kwamba mwenendo wa ukusanyaji wa mapato hayo hauridhishi. Kwa
mfano, kuanzia Mwezi Julai, 2013 hadi Aprili, 2014; Makusanyo yasiyotokana na Kodi
yalifikia Shilingi Bilioni 425.5 ikiwa ni Asilimia 57 ya lengo la kukusanya Shilingi
Bilioni 741.1 kwa mwaka. Aidha, kwa upande wa mapato ya Halmashauri, makusanyo yalifikia
Shilingi Bilioni 252.8, sawa na Asilimia 66 ya makadirio ya mwaka. Mwenendo huo nao
hauridhishi hivyo, ni lazima sasa tujipange upya kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Mheshimiwa Spika,
21. Ili kuimarisha ukusanyaji wa Mapato yatokanayo
na Kodi na yasiyo ya Kodi (Non-Tax Revenue) na ya Halmashauri kuanzia Mwaka ujao wa
Fedha, Wizara zenye jukumu la kukusanya Kodi na Maduhuli pamoja na makusanyo ya Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Idara za Serikali zinazojitegemea kuanzia
sasa zitatakiwa kuandaa Mpango Mkakati na Mpango Kazi (Action Plan) wa mwaka wa kukusanya
Mapato na Maduhuli yao yote na kutoa taarifa bila kukosa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya
Waziri Mkuu kuhusu makusanyo ya kila robo mwaka; ifikapo tarehe 15 ya mwezi unaofuata
kila baada ya robo mwaka ambaye atawasilisha taarifa hiyo ya utekelezaji kwenye Kamati
Ndogo za Baraza la Kazi la Baraza la Mawaziri zinazohusika kwa ajili ya tafakuri na
maelekezo.
Mheshimiwa Spika,
22. Tayari Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu ameagizwa kuandaa utaratibu mzuri wa kupata Taarifa za Makusanyo ya Mapato yatokanayo
na Kodi na Maduhuli kutoka Wizara na Taasisi zote za Serikali zinazojitegemea. Aidha,
naagiza kila Katibu Mkuu wa Wizara, Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji Wakuu
wote wa Taasisi, Wakala za Serikali na Idara za Serikali zinazojitegemea kuhakikisha
zinakusanya Mapato kulingana na Mpango Mkakati wa Mpango Kazi na kuwasilisha Taarifa
hizo kwa wakati.
MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa Spika,
23.
Eneo la misamaha ya Kodi limekuwa likilalamikiwa na Wananchi wengi na Waheshimiwa
Wabunge kwa muda mrefu. Katika eneo hili, ni vyema Wananchi na Waheshimiwa Wabunge
kutambua kuwa kuna misamaha ya Kodi ya aina mbalimbali. Kundi la Kwanza ni misamaha
ya Kodi inayotolewa kwa Washirika wetu wa maendeleo wanaotoa misaada katika miradi
mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi linajumuisha pia misamaha ya bidhaa za Sukari,
Mchele, Mafuta ya Diseli, n.k. Kundi la Pili ni misamaha ya Kodi kwa Asasi zisizo
za Kiserikali na Mashirika ya Dini yanayotoa huduma kwa Wananchi pasipo kutegemea
kupata faida. Kundi la Tatu ni misamaha ya Kodi ambayo hutolewa ikiwa ni Mkataba wa
kuvutia Uwekezaji Nchini. Kwa kawaida Misamaha ya aina hii hutolewa kupitia Kituo
cha Uwekezaji (TIC) ili kuvutia Uwekezaji katika Miradi Mikubwa ambayo tunategemea
kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo yatakuwa makubwa sana ikilinganishwa
na msamaha wa kodi uliotolewa.
Kwa mujibu wa Takwimu za hivi karibuni za Mamlaka
ya Mapato Tanzania za Mwaka 2012/2013 zinaonesha kuwa Misamaha ya Kodi ya bidhaa za
mtaji kwa Wawekezaji waliopewa Hati za Usajili na Cheti cha hadhi ya Uwekezaji mahiri
kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ni Asilimia 19.7 ya Misamaha yote.
24.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa na Kituo cha Uwekezaji TIC mwaka 2012 kwa Makampuni
Makubwa 50 ya Uwekezaji yaliyosajiliwa na TIC, kiasi kilichowekezwa katika kipindi
cha miaka mitano (2005 – 2010), ni Shilingi Trilioni 1.7 ambapo katika uwekezaji huo,
Makampuni hayo yalilipa Kodi Shilingi Trilioni 1.1. Aidha, Makampuni hayo yalitoa
ajira 981,000 za moja kwa moja na 112,070 zisizo za moja kwa moja. Misamaha ya Kodi
iliyotolewa kwa Makampuni hayo ni Asilimia Saba (7) tu ya Kodi yote iliyolipwa na
Makampuni hayo. Misamaha kwa makundi mengine ikiwemo Miradi ya Wahisani mbalimbali
na Asasi zisizo za Serikali (NGOs), n.k ni Asilimia 38.6; na Misamaha kwa Sekta Binafsi
ni Asilimia 23.8 ya Misamaha yote iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mheshimiwa
Spika,
25. Serikali inatambua kuwa bado tuna kazi ya kubwa ya kuhakikisha kwamba
misamaha ya kodi inayotolewa kwa Wawekezaji na Walengwa wengine Nchini inatumika vizuri
katika miradi iliyokusudiwa, na si vinginevyo. Kwa mfano, msamaha wa kodi uliotolewa
kwenye mafuta ya dieseli hatutarajii mafuta hayo yaingie sokoni badala ya kutumika
kwenye mradi wa uwekezaji uliokusudiwa. Hivyo, kutokana na umuhimu wa kuvutia uwekezaji
Nchini, misamaha ya kodi iiliyoidhinishwa na Bunge Kisheria itaendelea kutolewa kwa
Wahusika. Nitoe wito kwa wote watakaopata misamaha hii kuwa waadilifu na kuitumia
kwa malengo yaliyokusudiwa. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote atakayetumia
vibaya misamaha hii. Serikali kwa upande wake itaimarisha zaidi usimamizi wa matumizi
ya misamaha hii na itahakikisha inatumika kwa lengo lililokusudiwa.
KUONDOA
URASIMU KATIKA VITUO VYA FORODHA
Mheshimiwa Spika,
26. Mwezi Februari,
2014 nilipokutana na Wafanyabiashara waliotaka kugoma kutumia Mashine za kisasa za
kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devise-EFD) walinieleza kwamba moja ya eneo linalowasumbua
ni urasimu mkubwa katika maeneo mengi ya Vituo vya Forodha Mipakani na Bandarini hasa
Dar es Salaam. Katika Vituo hivyo vya Forodha walisema zipo Taasisi nyingi za Serikali
zinazofanya ukaguzi wa mizigo inayoingizwa Nchini na ile inayotoka kwenda Nje ya Nchi.
Miongoni mwa Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Idara ya
Uhamiaji; Jeshi la Polisi; Wakala wa Viwango (TBS); Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula
na Dawa (TFDA); Mkemia Mkuu wa Serikali; Tume ya Nguvu za Atomiki; Idara ya Misitu
na Nyuki; Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Mimea na Wadudu (TPRI); Kitengo cha Afya ya
Mimea cha Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; na Kitengo cha Afya ya Mifugo cha
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika,
27. Serikali
iliweka Taasisi nilizozitaja hapa kwa nia njema ya kusimamia vizuri na kudhibiti uingizaji
na utoaji wa mizigo bandarini na bidhaa zinazopitishwa katika mipaka ya Nchi yetu.
Hata hivyo, baadhi ya Watendaji wasio waaminifu wanatumia mwanya huo kuwalazimisha
Wafanyabiashara kutoa fedha zao bila kupata risiti eti kwa ajili ya kusaidia mizigo
kupitishwa kwa urahisi. Aidha, nimeelezwa kuwa baadhi ya Watendaji wanatumia nafasi
zao kuongeza urasimu usio na lazima ili kudai rushwa, jambo ambalo linaongeza gharama
kwa Wafanyabiashara na kuleta athari za kuchelewesha utoaji wa mizigo bandarini na
kuathiri sifa za bandari zetu. Naagiza Wizara husika kufuatilia utendaji kazi wa Vyombo
hivyo kwa karibu na kushughulikia kwa haraka malalamiko mbalimbali na kupata ufumbuzi
wa tatizo la urasimu katika Vituo vya Forodha. Yapo Makampuni ya Mawakala yapatayo
527 yanayofanya kazi za Mawakala wa kutoa bidhaa Bandarini. Tunayo taarifa kuwa, Utitiri
wa Makapuni hayo nao umekuwa chanzo kikubwa cha rushwa na ukwepaji Kodi. Serikali
haikubaliani na aina hii ya Utendaji wa Makampuni hayo. Utendaji huo uachwe sasa.
Navitaka Vyombo husika kufuatilia kwa karibu sana mienendo ya Makampuni yote ya Mawakala
wa kutoa bidhaa Bandarini na kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Spika,
28.
Pamoja na changamoto zilizopo katika bandari zetu, napenda kutumia fursa hii kumpongeza
Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb.) kwa kazi kubwa anayofanya
ya kusimamia kwa karibu uboreshaji wa utendaji katika Mamlaka ya Bandari; hasa kupunguza
muda wa kutoa mizigo bandarini kutokana na kuweka utaratibu wa kufanya kazi kwa saa
24. Ninamtaka aongeze juhudi zaidi ili kuimarisha utendaji kazi katika eneo hili ili
kuongeza sifa kwa Bandari zetu.
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA SASA
(BIG RESULTS NOW-BRN)
Mheshimiwa Spika,
29. Utekelezaji wa mfumo
wa Matokeo Makubwa Sasa umeendelea vizuri, na licha ya matatizo ya upatikanaji wa
fedha matokeo yake yameanza kuonekana kama ilivyoainishwa na Waheshimiwa Mawaziri
wa Sekta husika walipowasilisha Hotuba zao katika Mkutano huu. Uzoefu tulioupata katika
kipindi hiki, ni kwamba upatikanaji wa matokeo makubwa kwa muda mfupi unawezekana,
ilimradi tuwe tumechagua vipaumbele vyetu kwa usahihi, tunafuatilia utekelezaji kwa
karibu, na kutanzua changamoto mara zinapojitokeza. Napenda kutumia fursa hii tena
kuwashukuru Wadau wote wa Maendeleo waliowezesha kupata matokeo haya. Natoa wito kwa
Viongozi na Watendaji katika ngazi zote tuendeleze kasi na umakini wa kufuatilia utekelezaji
wa Miradi ya kipaumbele ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” ili tuweze
kufanikiwa zaidi katika kipindi kijacho.
Mheshimiwa Spika,
30. Napenda
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha
mchakato wa Ajira za nafasi wazi za Watumishi wa Taasisi ya Kuratibu na Kusimamia
Mfumo wa Tekeleza sasa kwa Matokeo Makubwa kilichopo Ofisi ya Rais, yaani President’s
Delivery Bureu (PDB). Vilevile, Serikali itaimarisha Vitengo na Taasisi zote zinazosimamia
mfumo huu, ikiwa ni pamoja na kukamilisha uundaji wa Vitengo na Kamati za kuratibu
utekelezaji katika Wizara na Taasisi zinazotekeleza Programu ya Uboreshaji wa Mazingira
ya Biashara Nchini. Serikali pia itaandaa na kutangaza matokeo ya utekelezaji wa mfumo
huu katika mwaka wake wa kwanza wa 2013/2014, baada ya kuhakikiwa na jopo huru la
Kimataifa. Hatua hii inalenga kukamilisha mfumo wa uwajibikaji ambao ni chachu muhimu
ya mafanikio ya mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Vilevile, Wizara zingine,
Mikoa na Halmashauri zote zinaendelea kuhimizwa kutumia mfumo huu katika kuchambua,
kupanga, na kutekeleza mipango na miradi yake yote ya maendeleo kwa kuzingatia mfumo
huu wa Matokeo Makubwa Sasa.
KILIMO
Hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
31. Hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha
katika maeneo mengi kufuatia albaki ya mavuno ya msimu uliopita na matarajio ya mavuno
mazuri katika msimu wa kilimo wa 2013/2014 ambayo uvunaji wake umeanza katika baadhi
ya maeneo. Aidha, kufuatia mwenendo mzuri wa hali ya unyeshaji wa mvua katika msimu
wa 2013/2014 katika maeneo mengi ya nchi, kuna matarajio ya uzalishaji mkubwa wa mazao
ya chakula na hivyo upatikanaji mzuri zaidi wa chakula kwa mwaka 2014/2015.
Mheshimiwa
Spika,
32. Hali ya akiba ya chakula katika Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula ni nzuri. Mwanzoni mwa mwaka 2013/2014 Akiba ya Chakula ilikuwa Tani 25,452.6
na baada ya kununua Tani 219,377.3, akiba ilifikia Tani 244,829.9. Hadi kufikia tarehe
4 Juni 2014 Serikali ilitoa Jumla ya Tani 54,845.0 kama chakula cha Msaada na Maafa
ikiwemo njaa, mafuriko na operesheni mbalimbali na kubaki na akiba ya Tani 189,984.9.
Aidha, Serikali ina mpango wa kuuza Tani 75,000 ili kuacha Maghala wazi kwa ajili
ya mazao mapya yatakayonunuliwa katika msimu mpya wa 2014/2015 na hivyo, kuyaacha
Maghala ya Serikali yakiwa na Akiba ya Tani 114,984.9 za Mahindi ifikapo Julai, 2014.
Katika mwaka 2014/2015 Serikali itanunua Tani 160,000 za Nafaka na kuzijumlisha zile
za akiba kutoka msimu wa 2013/2014, hivyo kuwa na hifadhi ya jumla ya Tani 274,984.9
za Nafaka.
Mheshimiwa Spika,
33. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu
na Wananchi kuwa Serikali kwa mara ya kwanza imefikia uamuzi wa kununua Mpunga na
kuhifadhi katika Maghala ya Taifa kama Chakula cha Akiba. Uamuzi huu umefikiwa kwa
kuzingatia kuwa baada ya Serikali kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mchele kutoka
nje ya Nchi kufidia pengo la upungufu wa mchele hapa Nchini, baadhi ya wafanyabiashara
hao waliendelea kuingiza mchele hata baada ya muda wa vibali vyao kuisha hivyo kuwafanya
Wakulima kukosa soko la mpunga baada mavuno kuongezeka. Napenda kulijulisha Bunge
lako Tukufu kuwa katika msimu huu wa mavuno, Serikali imedhamiria kuanza na hifadhi
ya Tani 10,000 za mpunga kwa lengo la kujiridhisha kama hifadhi ya mpunga haitakuwa
na matatizo. Baada ya kujiridhisha, katika misimu inayofuata, Serikali itaongeza kiasi
cha Mpunga utakaohifadhiwa na Serikali kwa nia ya kuziba pengo la upungufu wa mchele
iwapo hali hiyo itatokea badala ya kutegemea Wafanyabiashara tu kuagiza Mchele kutoka
nje ya Nchi.
Nitumie fursa hii kuwahimiza wakulima kuongeza uzalishaji wa
zao hili kwa vile sasa Serikali imeamua kuhifadhi Mpunga kama ilivyo kwa Mahindi na
Mtama. Aidha, niwaahidi Wananchi kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya
kuhifadhi mpunga katika Maghala ya Taifa ili kuwawezesha Wakulima wengi kupata soko
kama ilivyo kwa mazao ya Mahindi na Mtama. Ninaagiza kuanzia sasa Taasisi zote zinazotoa
vibali vya kuingiza sukari, mchele na ngano kutoka nje ya nchi kuhakikisha kuwa Wafanyabiashara
wenye vibali vinatumika tu kwa muda uliopangwa.
Mheshimiwa Spika,
34.
Naagiza pia kwa Wakala wa Hifadhi Taifa ya Chakula kuanza kununua nafaka kwa wakati
ili wakulima waweze kunufaika na bei nzuri zitakazotolewa. Ni matarajio yangu kuwa
Wakala pamoja na kununua nafaka kwa bei ya soko na kupitia vituo vya ununuzi, vikundi
vya wakulima na mawakala, watahakikisha kuwa wakulima hasa wa mahindi wanapata si
chini ya Shilingi 500 kwa kilo ambayo ni bei ya msimu uliopita ili kuwawezesha kurudisha
gharama za uzalishaji. Aidha, nawasihi Wakulima wasikubali kuuza mazao yao chini ya
bei hiyo. Lengo ni kuwawezesha kurejesha gharama za uzalishaji. Bei elekezi kwa nafaka
nyingine pia zitangazwe kwa kuzingatia gharama za uzalishaji mapema kabla ya msimu
wa ununuzi kuanza. Nichukue fursa hii kuwasihi Wananchi hasa katika Kanda zile wanazouza
nafaka iliyo na ubora hafifu hasa uchafu kujirekebisha na kuacha tabia hiyo mara moja,
kwani kwa kufanya hivyo wanavuruga jitihada za Serikali za kusaidia Wakulima Wadogo
kuinua maisha yao.
Mazao ya Asili ya kuingiza Fedha za Kigeni
Mheshimiwa
Spika,
35. Nchi yetu inayo mazao yanayotuingizia fedha za kigeni ikiwa ni
pamoja na Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Tumbaku n.k. Kwa madhumuni ya Hotuba yangu
ya leo nimeona nizungumzie uendelezaji wa mazao ya Korosho na Pamba. Kutokana na bei
ya mazao haya kuendeea kutegemea bei katika Soko la Dunia, Wakulima wetu wameendelea
kupata bei za chini na zisizokuwa na uhakika kila msimu wa mauzo unapowadia. Hivyo,
ni vyema sasa tukazingatia umuhimu wa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa soko la
ndani linakuwa la uhakika kwa mazao haya. Aidha, Serikali imekuwa ikiweka mikakati
ya kusindika mazao ya Pamba na Korosho hapa Nchini kwa lengo la kuyaongezea thamani
na kuongeza Tija katika uzalishaji kwa eneo. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali sasa
imejikita katika utafiti wa mbegu na miche bora pamoja na kufufua viwanda ambavyo
vitatumia malighafi zitokanazo na mazao haya hapa Nchini.
Mapango wa kufufua
Viwanda vya Korosho
Mheshimiwa Spika,
36. Uzalishaji wa korosho
umeendelea kuwa tegemeo kubwa la wakulima wa Mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara na
pia Mkoa wa Pwani. Kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali za kufufua zao hili,
katika msimu wa 2013/2014, uzalishaji wa Korosho umeongezeka hadi kufikia Tani 127,939.4
ikilinganishwa na Tani 121,703.8 kwa msimu wa 2012/2013. Pamoja na ongezeko katika
uzalishaji, mchango wa zao hili kwa Pato la Mkulima na Taifa umekuwa mdogo kutokana
na Taifa kuendelea kuuza korosho ghafi nje ya Nchi kwa zaidi ya Asilimia 90 hivyo,
kuikosesha Nchi mapato na faida nyingine nyingi kwa wakulima. Hali hii imetokana na
Wawekezaji wa Viwanda 12 vya kubangua korosho vilivyojengwa na Serikali miaka ya 1980
na kubinafsishwa mwaka 2004 kushindwa kuvifufua viwanda hivyo kutokana na changamoto
mbalimbali ikiwemo kukosa mitaji na kuendelea kutumia Teknolojia iliyopitwa na wakati.
Mheshimiwa
Spika,
37. Napenda kulijulisha Bunge lako na wananchi kwamba kutokana na changamoto
hizo, mwezi Februari, 2014 niliitisha Kikao kilichohusisha baadhi ya Watendaji Wakuu
wa Serikali, baadhi ya Wamiliki wa Viwanda vya kubangua Korosho na baadhi ya Taasisi
ya Fedha kujadili mikakati ya kufufua viwanda vya kubangua korosho hapa nchini. Hivyo,
Serikali kwa kushirikiana na wadau hao iliamua ifanyike tathmini ya gharama na mikakati
ya kufufua Viwanda vya kubangua korosho hatua kwa hatua na kwa kuanzia Serikali kwa
kushirikiana na Wamiliki itaanza kufufua Viwanda vinne (4) vyenye uwezo wa uzalishaji
(Installed Capacity) wa kati ya Tani 5,000 hadi 10,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa
Spika,
38. Kwa kuanzia Serikali iliamua tathmini ifanyike kwa viwanda vya
Newala-I; Masasi; Lindi Farmers kilichopo Nachingwea; na Kiwanda cha Kampuni ya BUCCO
kilichopo Lindi kwa ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni ya Oltremare ya Italy
ambayo ina uzoefu mkubwa duniani katika utengenezaji wa mashine za usindikaji wa Korosho.
Kampuni hii ndiyo iliyojenga baadhi ya viwanda vya kubangua korosho hapa nchini kikiwepo
Kiwanda cha TANITA. Tathmini hii itaangalia hali ilivyo katika masuala ya kiufundi,
usindikaji na miundombinu; uwezo na madeni ya Kifedha; Masuala ya Kisheria kuhusu
Mikataba mbalimbali iliyowekwa na wawekezaji hawa, Mfumo wa upatikanaji wa malighafi;
na uwezo wa Rasilimali watu wa viwanda hivyo.
Mheshimiwa Spika,
39.
Tathmini ya awali ya gharama za kufufua viwanda hivyo vinne iliyofanywa na Kampuni
ya Oltremare kwa kushirikiana na Kampuni ya Agrofocus ya hapa Tanzania ilibaini kuwa
kuna njia mbili zinazoweza kutumika: Kwanza, iwapo Serikali itaamua kuvifufua Viwanda
vya Newala 1; Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa kila kimoja kubangua Tani 15,000
kwa mwaka, pamoja na cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka; kwa pamoja zitahitajika
jumla ya Paundi 31,280,690. Pili, iwapo Serikali itaamua kuvifufua viwanda vya Newala
1, Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa kila kimoja kubangua Tani 22,000 kwa mwaka,
na Kiwanda cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka, kwa pamoja zitahitajika jumla
ya Paundi 44,185,022. Hata hivyo, kabla ya kuweka mikakati ya kupata fedha hizo, Serikali
imeamua kupeleka kikosi kazi chake kutathmini tena gharama hizo na kuzilinganisha
na hizo za awali kwa nia ya kushirikiana na vyombo vya fedha na Kampuni ya Oltremare
ya Italy kufufua viwanda hivi.
Aidha, Kampuni ya Oltremare ya Italy imekubali
kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utawala na uendeshaji wa viwanda hivyo pindi vitakapofufuliwa;
na kuisaidia Tanzania kupata Soko la Korosho zitakazobanguliwa. Naamini kabisa ufufuaji
wa viwanda hivi utasaidia kuboresha teknolojia, kuongeza ufanisi, ajira na mapato
ya Serikali na bei ya korosho ghafi kwa mkulima badala ya kutegemea bei ya Soko la
Dunia pekee.
Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
40. Zao
la Pamba lina mchango mkubwa katika kukuza Uchumi wa Nchi yetu na kuondoa umaskini
kwa zaidi ya Wakulima 400,000 na wategemezi wao katika Mikoa takriban 15 hapa Nchini.
Hata hivyo, bado Kilimo chake kinakabiliwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto
hizo ni pamoja na tija ndogo, matumizi kidogo ya teknolojia za kisasa na zana duni.
Aidha, kuna huduma duni za ugani na utafiti, kukosa mitaji na soko la uhakika; migogoro
baina ya wakulima na wafanyabiashara, na Uhaba wa Viwanda vya kuongezea Pamba thamani.
Mheshimiwa
Spika,
41. Katika msimu wa 2011/2012 Serikali kwa kushirikiana na Shirika la
Gatsby Charitable Foundation ya Uingereza chini ya Ufadhili wa Lord David Sainsbury
ilianza majaribio ya Mfumo wa Kilimo cha Pamba cha Mkataba kupitia Program ya Kuendeleza
zao la Pamba katika Mkoa wa Mara na Wilaya za Bariadi na Kibondo kwa madhumuni ya
kutafuta ufumbuzi wa changamoto nilizoeleza punde. Matokeo ya majaribio yalionesha
kuwa, uzalishaji uliongezeka kutoka Kilo 398 kwa ekari hadi Kilo 558 kwa ekari; na
ubora wa pamba uliongezeka hadi kufikia Asilimia 78 kutoka Asilimia 48 za awali.
Mheshimiwa Spika,
42. Baada ya Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kuanza mikakati ya kusimamia kilimo cha Mkataba cha pamba, takwimu za mwezi Mei, 2014
zinaonesha kuwa Wilaya Saba (7) katika Kanda ya Magharibi zilishiriki katika Kilimo
cha Mkataba. Aidha, takriban wakulima 90,000 wamenufaika na mikopo ya Pembejeo ya
Kilimo cha Mkataba msimu huu kupitia Wachambuzi takriban 15, ikilinganishwa na wakulima
30,000 katika msimu uliopita. Vilevile, takwimu hizo zinaonyesha wakulima 140,000
ndani ya kilimo cha mkataba wamelima zaidi ya ekari 400,000; na kwamba katika msimu
huu kati ya Makampuni 42 ya pamba, Makampuni 26, yameshiriki kwenye kilimo cha mkataba
ikilinganishwa na Makampuni 12 yaliyoshiriki msimu uliopita. Kwa ujumla wakulima wengi
wameelezea kunufaika kutokana na Kilimo cha Pamba cha Mkataba hasa kutokana na kuongezeka
kwa kipato.
Mheshimiwa Spika,
43. Pamoja na mafanikio hayo,
yaliyojitokeza changamoto kadhaa ikiwepo ya baadhi ya Wakulima kuuza na Makampuni
kununua pamba nje ya mkataba jambo lililokwamisha Mfumo wa kurudisha mikopo ya pembejeo
katika maeneo yaliyolimwa kwa mfumo wa Kilimo cha Mkataba. Hivyo, Mheshimiwa Rais
alitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha
Mkataba kwenye zao la pamba katika maeneo yote yanayolimwa pamba. Lengo ni kushirikisha
Wadau wengine, kuainisha na kupata ufumbuzi wa kasoro zilizojitokeza katika misimu
iliyopita; kupanga mikakati ya utekelezaji; kuweka utaratibu mzuri wa kulinda uwekezaji
wa wachambuaji na pia kulinda haki za wakulima kwa kuzingatia mikataba inayowekwa
kati ya wakulima na wachambuaji.
Nitumie fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa
na Wilaya kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais kwa Viongozi kusimamia kikamilifu kazi
hiyo ili Wakulima wanufaike na Mfumo huu wa Kilimo cha Mkataba. Njia nyepesi ya kutoa
elimu juu ya Kilimo cha Mkataba ni kutumia Mashamba Darasa na Mashamba ya Mfano. Nawaagiza
Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri wasimamie vema na kwa
karibu utaratibu huu.
Mheshimiwa Spika,
44. Kutokana na tatizo
lililojitokeza la baadhi ya wakulima wa pamba kuuziwa Tani 1,088 za mbegu ya pamba
kipara ambayo haikuota kutoka Kampuni ya Quton, kwa niaba ya Serikali napenda kuwapa
pole Wakulima hao. Kama Serikali ilivyoahidi hapo awali, tumesitisha malipo ya Shilingi
Bilioni 1.7 za ruzuku kwa Kampuni ya Quton. Aidha, Serikali inaitaka Kampuni ya Quton
kutorudia makosa haya katika siku zijazo. Maafisa Ugani wasimamie kwa karibu upandaji
wa mbegu hizi wakati wa msimu kwa kutoa elimu stahiki.
Mheshimiwa Spika,
45. Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili la mbegu hafifu, Serikali
kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaendelea
na juhudi za kukaribisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbegu bora kipara
kutoka ndani na nje ya Nchi ili kuweka mazingira ya ushindani ambao utaleta ubora
zaidi. Aidha, Taasisi zinazohudumia zao la pamba ziangalie kama kuna uwezekano wa
kupata mbegu za pamba hata kutoka nje ya Nchi kwa kuzingatia masuala ya ubora na unafuu
wa bei. Nichukue fursa hii kuwakumbusha Bodi ya Pamba na wagani wa zao la pamba kuhakikisha
kuwa ubora wa mbegu (germination percentage) unafanyiwa tathmini kabla mbegu hazijagawiwa
kwa wakulima. Aidha, Wakulima waelimishwe manufaa ya kutumia Mbegu Kipara kwamba wakati
wa kuziandaa zinawekewa viuatilifu ambavyo vinaua vimelea na wadudu ambao wanatokana
na mavuno ya msimu uliopita, hivyo kupunguza uwezekano wa pamba inayotokana na mbegu
hizi kupata magonjwa na wadudu mapema ikilinganishwa na mbegu za manyoya.
46.
Mbegu Kipara zinaweza pia kutumika na mashine za kupandia (planter) hivyo kuwezesha
mimea ya pamba kuota katika mstari na kwa nafasi stahili na kumwezesha mkulima kupata
mimea mingi kwa ekari (plant population) kama inavyoshauriwa kitaalamu miche 22,222,
hivyo kuongeza tija kwa ekari tofauti na mbegu za manyoya. Naamini kupitia ushirika
na Kilimo cha Mkataba Wakulima wataweza kuungana kupata planter ili kupunguza sulubu
ya jembe la mkono wakati wa kupanda. Ninaiagiza Bodi ya Pamba iendelee kusimamia zoezi
la wakulima waliochaguliwa kuzalisha mbegu bora kwa Kampuni ya Quton ili kuwezesha
ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora kwa Wakulima.
Mheshimiwa Spika,
47. Pamoja na changamoto zinazoikumba tasnia ya pamba na hasa Kilimo cha mkataba
cha pamba, nichukue fursa hii kuwasihi wakulima wa pamba ambao hawajajiunga na mfumo
huu kufanya hivyo kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwa wale waliojiunga tayari.
Napenda kuwakumbusha Wagani wa Pamba kusimamia ipasavyo suala la usafi wa pamba inayouzwa
na wakulima ili wakulima wapate bei nzuri. Aidha, kutokana na kilimo cha mkataba katika
zao la tumbaku na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani kwa zao la korosho kuwanufaisha
sana wakulima wa mazao hayo, niwatake viongozi wote wanaohusika na uimarishaji wa
zao la pamba kuimarisha kilimo cha pamba na suala la kilimo cha pamba cha mkataba
ili kuweka utaratibu utakaomfanya mkulima kuuza pamba kwa yule aliyemwezesha kupata
pembejeo na kwa kutumia mfumo wa Ushirika.
Mheshimiwa Spika,
48.
Kupitia Mkutano Mkuu wa Wadau wa Sekta ya Pamba wa tarehe 4 Julai 2013 Jijini Mwanza,
wajumbe waliiomba Serikali kusimamia uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya
zao la pamba na utengenezaji wa bidhaa za pamba hapa Nchini. Nakubaliana na azimio
hilo kwa sababu hatuwezi kama nilivyoeleza kwa zao la Korosho, kuendelea kusafirisha
sehemu kubwa ya pamba inayozalishwa hapa nchini kama malighafi kwa vile hakutainufaisha
nchi na hata wakulima. Hivyo, narudia tena wito wangu kuitaka Wizara ya Viwanda, Biashara
na Masoko kuhimiza uwekezaji katika viwanda vingi vya kusindika na kutengeneza bidhaa
za pamba hapa Nchini badala ya kuuza pamba ghafi. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu
na Wananchi kuwa, katika kujiandaa na Raslimali Watu kwa ajili ya Viwanda vya Nguo
hapa Nchini, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kimewezeshwa kuanzisha Kozi za Shahada mbili
za Uhandisi wa Viwanda vya Nguo na Ubunifu, na Vyuo vya VETA vinatoa mafunzo hayo
kwa Kada za Chini.
Mheshimiwa Spika, 49. Kwa kuwa msimu wa ununuzi
wa Pamba mwaka 2014/2015 umeshazinduliwa tangu tarehe 18 Juni, 2014, ninawasihi Wakuu
wa Mikoa yote inayolima pamba kusimamia kwa karibu mambo yafuatavyo:
Kwanza:
Kuhakikisha kuwa bei ya chini ya kununua Pamba inakuwa Shilingi 750 kwa kilo;
Pili:
Kuhakikisha kuwa maeneo yote ambayo Bodi ya Pamba itathibitisha kwamba hakuna mnunuzi
aliyetoa huduma au mkopo kwa Mkulima, yawe huru kwa mnunuzi yeyote kupewa Leseni ya
kununua Pamba ili kuwapa fursa Wakulima ambao hawapo katika mfumo wa kilimo cha mkataba
kuuza bila matatizo.
50. Ni matumaini yangu kwamba, hatua hizi zitasaidia
kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa zao la Pamba.
UMUHIMU WA VIWANDA NA KULINDA
VIWANDA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
51. Maendelea ya Nchi yoyote ile yanategemea
sana ujenzi wa viwanda. Kwa maana hiyo, suala la ujenzi wa viwanda haliepukiki kutokana
na sababu kwamba, Viwanda husaidia kuongeza thamani mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi
na mazao ghafi yanayozalishwa katika Sekta zingine. Aidha, Viwanda huongeza muda wa
bidhaa hizo wa kutumika kabla ya kuharibika. Vilevile, mazao yaliyoongezwa thamani
humpatia mkulima bei nzuri na kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao. Uwepo
wa viwanda pia unatusaidia kupata fedha za kigeni, kutoa ajira na hivyo kupunguza
tatizo la ajira kwa watu wetu hasa Vijana. Kwa maana hiyo kuna haja ya kuwepo Sera
na Sheria mahsusi zitakazohimiza na kuchagiza uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na
pia kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Mheshimiwa Spika,
52. Kwa kutambua
umuhimu wa viwanda Nchini, ndio maana Serikali imeanzisha Mpango wa uanzishaji wa
Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje Export Processing Zones - (EPZ) na Maeneo
Maalum ya Kiuchumi Special Economic Zones - (SEZ) kama mkakati mahususi wa kuvutia
Wawekezaji. Katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 jumla ya miradi ya viwanda ipatayo
52 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 474.37 ilisajiliwa na Mamlaka ya EPZ
ambapo ajira 12,347 za moja kwa moja zinatarajiwa kupatikana. Aidha, katika kipindi
cha Januari hadi Mei 2014, pekee jumla ya miradi 21 yenye thamani ya Dola la Kimarekani
Milioni 121.4 inayotarajia kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 4,814 imesajiliwa.
Katika miradi hiyo, ipo Miradi inayosajiliwa kwa utaratibu wa kushirikisha Sekta ya
Umma na Binafsi (Private Public Partnership-PPP). Ujenzi wa miradi hiyo iko katika
hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika,
53. Ni kweli
kwamba, Serikali imeweka juhudi kubwa katika ujenzi wa Viwanda katika sehemu mbalimbali
Nchini na pia kupanua wigo wa bidhaa zinazozalishwa. Kwa mfano, hivi sasa kuna Viwanda
vya Chuma takriban 17 vinavyojumuisha Viwanda vya mabati, misumari, nyaya za uzio,
nyaya za umeme, bidhaa za chuma, ikiwemo nondo na mabomba ya chuma kwa ajili ya matumizi
mbalimbali. Lakini pia tunavyo Viwanda vya kuzalisha Saruji vipatavyo vitano (5) vya
Dar es Salaam, (TPCC), Tanga (TCC), Mbeya (MCC), Pwani (Rhino Cement Mkuranga), na
Lindi (Lee Building Material ya Kilwa Masoko). Vilevile, Viwanda Vipya vya Saruji
vinajengwa Arusha, Dar-es-Salaam (3), Tanga (2), Lindi, Pwani na Mtwara. Upanuzi huu
wa Viwanda vya Saruji vitaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi Wazalishaji Wakuu
Barani Afrika na hivyo kujitosheleza Kitaifa na kuuza nje.
54. Tunavyo pia
Viwanda vikubwa vya Kusindika Ngozi Saba (7) katika Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam,
Kilimanjaro (2), Morogoro, Pwani na Shinyanga. Tunavyo Viwanda vya Nguo Tisa (9) katika
Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam (4), Mara, Morogoro, Mwanza na Tanga na tunavyo pia
Viwanda vya Sukari katika Mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Morogoro ambavyo vyote kwa
ujumla wao vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa
Spika,
55. Pamoja na jitihada kubwa iliyowekezwa katika ujenzi wa Viwanda
hivyo Nchini, tunayo Changamoto kubwa ya namna ya kuvilinda Viwanda hivi dhidi ya
ushindani usio halali (Unfair Competition) ili viweze kukua na kuimarika kiushindani,
Kikanda na Kimataifa. Mathalani, zipo bidhaa au vifaa vinavyoingizwa Nchini na kuuzwa
kwa bei ya chini ikilinganishwa na bei ya bidhaa aina hiyo hiyo zinazozalishwa Nchini.
Bidhaa hizo huuzwa kwa bei ya chini kutokana na wazalishaji wa Nchi zinakotoka bidhaa
husika kupewa ruzuku au bidhaa hizo zinakuwa na ubora duni usiokidhi Viwango vya Ubora
au kutozwa ushuru mdogo au kupewa msamaha wa ushuru. Hali hii husababisha ushindani
usio wa haki katika Soko la Ndani na ni changamoto kubwa kwa Taifa letu na Afrika
Mashariki kwa ujumla. Naomba uniruhusu nitoe mifano michache ambayo itatuwezesha kuona
ni namna gani tunaweza kukabili changamoto hii kwa lengo la kulinda Viwanda vyetu
Nchini.
Mheshimiwa Spika,
56. Nikianza na Saruji. Kama nilivyosema
tunavyo Viwanda vitano vya Saruji vyenye uwezo wa kuzalisha Saruji hadi Tani Milioni
3.8 kwa mwaka. Mahitaji ya Saruji kwa sasa ni Tani Milioni 3.9 kwa mwaka na zipo juhudi
za kuongeza uzalishaji kupitia uwekezaji katika miradi tisa (9) mipya ya ujenzi wa
Viwanda vya Saruji ambavyo kwa ujumla wake inatarajiwa vitazalisha Tani Milioni 8.3
kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika,
57. Pamoja na uzalishaji huo mkubwa, changamoto
kubwa ni namna ya kuhimili gharama kubwa za uzalishaji wa Saruji ikiwemo umeme, gharama
za usafirishaji, na ushindani mkubwa dhidi ya saruji kutoka nje ya nchi ambayo ina
ruzuku, hivyo kuvuruga soko la ndani kwa Viwanda vya Saruji. Aidha, ziko taarifa za
ukwepaji kodi na udanganyifu ambao umeendelea kuwa tatizo kubwa sana katika Sekta
ya Saruji. Kwa kutambua changamoto hiyo, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubaliana
kuweka Ushuru wa Forodha wa Asilimia 55 mwaka 2005 na kuushusha kufikia Asilimia 35
mwaka 2010. Matarajio yalikuwa ni kuvilinda Viwanda hivi ili vijijenge kwa miaka mitano
na baada ya hapo kuendelea kuvilinda kwa kuviweka chini ya kundi la bidhaa nyeti,
yaani kuwa na wigo wa pamoja wa Ushuru wa Forodha wa zaidi ya Asilimia 25.
Mheshimiwa
Spika,
58. Hali iliyojitokeza katika Viwanda vya Saruji haitofautiani sana
na Viwanda vya Chuma ambavyo navyo vina changamoto kubwa hasa katika uzalishaji na
ubora wa bidhaa za chuma. Mathalan, ziko taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba karibu
Viwanda vyote vya Nondo Nchini vinazalisha chini ya viwango, jambo ambalo halikubaliki
kabisa. Nilibahatika kufanya Ziara Mkoa wa Mwanza ambapo nilikuta katika Mradi mmoja
wa ujenzi wa Tanki la Maji – Mkandarasi alikuwa ananunua Nondo kutoka Uganda kwa madai
kuwa Nondo zilizokuwa zinazalishwa na Viwanda vyetu kwa maelezo yake zilikuwa chini
ya viwango. Kiwango stahiki kinapaswa kuwa BS 406, BS 500, n.k. lakini Viwanda vyetu
vinazalisha chini ya kiwango hicho, yaani BS 400. Ni wakati muafaka sasa Viwanda vyote
kuzingatia viwango vya Kimataifa ili kuepusha majanga yanayotokana na udhaifu huo
na pia kuwezesha Nondo hizo kutumiwa na wahitaji wote wa hapa ndani na nje ya Nchi.
Ninahimiza Shirika la Viwango Nchini liendelee kusimamia ubora wa bidhaa za Nondo
kwa maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
59. Kwa sasa kuna
Viwanda vya Nondo takriban 15 ambavyo vina uwezo wa kuzalisha Nondo Tani 420,000 kwa
mwaka. Mahitaji ya Nondo ni Tani 200,000 kwa mwaka, ikiwa ni ziada ya Asilimia 40
zaidi ya mahitaji. Aidha, Viwanda hivi vya Nondo peke yake vinatoa ajira ya moja kwa
moja ya watu 4,000 na wengine takriban 40,000 ambao siyo wa moja kwa moja.
60.
Lakini pia tuna Viwanda vikubwa vya Chuma viwili (2) vyenye uwezo wa kuzalisha Mabati
Tani 150,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ni Tani 100,000 kwa mwaka ikiwa ni ziada ya
Tani 50,000, sawa na Asilimia 50 ya mahitaji. Viwanda hivi navyo vimezalisha ajira
ya takriban Watu 16,000.
Mheshimiwa Spika,
61. Mifano hiyo miwili
ya Uzalishaji wa Nondo na Mabati inadhihirisha kwamba tatizo la uzalishaji kukidhi
mahitaji halipo, bali tatizo ni uagizaji wa Nondo zinazoingizwa Nchini kwa kulipiwa
Ushuru mdogo, naambiwa wa Asilimia 10 tu kama Kodi kwa visingizio mbalimbali na hivyo
kutoa ushindani usio halali kwa Nondo zinazozalishwa Nchini. Aidha, mabati yanayoingizwa
Nchini yamewekwa katika orodha ya “Deemed Capital Goods” ambayo haiwabani watekelezaji
wa Miradi mbalimbali nchini kutumia mabati yanayotengenezwa na Viwanda vya Ndani.
Mheshimiwa Spika,
62. Tunavyo Viwanda vya kusindika Ngozi takriban
tisa (9). Viwanda hivi vina uwezo wa kusindika vipande vya Ngozi Milioni 13.2 kwa
mwaka katika hatua ya mwanzo yaani (Wet Blue). Kati ya hivyo vipande vya ngozi za
ng’ombe ni milioni 2.5 na vya mbuzi na kondoo ni Milioni 10.7. Aidha, usindikaji wa
ngozi ghafi umefikia Vipande 945,596 vya Ng’ombe na Vipande 2,713,636 vya Mbuzi na
Kondoo kwa mwaka 2013. Kama ilivyo kwa Viwanda vya Chuma na Saruji, changamoto kubwa
ya usindikaji wa ngozi ni pamoja na ushindani usio wa haki unaosababishwa na uingizaji
wa viatu vya plastiki na mitumba ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa viatu
vya Ngozi na bidhaa nyingine za Ngozi Nchini.
Mheshimiwa Spika,
63.
Vilevile, tunalo tatizo kubwa katika Viwanda vya uzalishaji wa Sukari Nchini. Tunavyo
Viwanda takriban Vinne vya Sukari. Uwezo wa uzalishaji Sukari Nchini ni Tani 300,000
kwa mwaka. Mahitaji ya Sukari ni Tani 590,000 kwa mwaka (Tani 420,000 ni Sukari ya
Matumizi ya Kawaida na Tani 170,000 Sukari ya Matumizi ya Viwandani). Kwa maana hiyo,
kuna upungufu wa Tani 290,000 sawa na Asilimia 49. Kati ya hizo Tani 170,000 (29%)
ya Sukari ya matumizi ya Viwandani na Tani 120,0000 (20%) Sukari ya Matumizi ya Kawaida.
Kutokana na upungufu huo, Serikali iliweka utaratibu wa kuagiza na kusambaza Sukari
kutoka Nje ya Nchi ili kufidia pengo hilo kwa kuruhusu Waagizaji kulipa Ushuru wa
Asilimia 25 na pia Ushuru wa Forodha Asilimia 10 kwa Viwanda vinavyotumia Sukari kwa
ajili ya matumizi ya Viwandani. Vipo pia vibali vya bila ushuru kabisa vinavyotolewa
wakati wa upungufu wa sukari.
Mheshimiwa Spika,
64. Utaratibu huu
pamoja na kusimamiwa na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), umesababisha malalamiko mengi
kuwa hatua hizi za kushusha Viwango vya Ushuru wa Forodha zimesababisha waingizaji
Sukari kukwepa kabisa Kodi, ikiwemo Ushuru wa Forodha na VAT. Aidha, zipo hisia kuwa
sukari hiyo ambayo ni nyingi zaidi ya kiasi kilichoruhusiwa kuingizwa Nchini inatokana
na Wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kutumia kinyume cha Sheria vibali vya Mamlaka
ya Mapato Tanzania vinavyowaruhusu kupitishia Nchini Sukari inayosafirishwa kwenda
nje ya Nchi (Transit Sugar) kwa kuibakiza bidhaa hiyo hapa Nchini na sukari ya viwandani
kuuzwa kama sukari ya mezani.
Mheshimiwa Spika,
65. Sukari hii
inayoingizwa nchini huathiri uzalishaji na mtiririko wa usambazaji sukari ya ndani
hivyo kutishia ukuaji wa viwanda vya ndani vya Sukari na uzalishaji wa sukari kwa
ujumla. Vilevile, itakumbukwa kuwa Serikali kwa nia njema, tulianzisha utaratibu wa
“Outgrowers” ili Wakulima wanaoishi kandokando ya Viwanda vya Sukari kulima Miwa na
kuuzia wenye Viwanda kule Kilombero, Mtibwa na Kagera ili kuboresha maisha yao kiuchumi.
Hivyo, kutokana na hali ilivyo kwa sasa, Wakulima hawa wakiwemo Wakulima wa Kilombero
wameshindwa kulipwa kwa wakati baada ya kuuza Miwa yao Kiwandani kwa vile Wazalishaji
wamekuwa wakiuza Sukari chini ya Wastani wa mauzo ya kawaida.
Mheshimiwa Spika,
66.
Nimeamua kuongea haya yote kuhusu hali halisi ya Viwanda vyetu na bidhaa zinazozalishwa
humu Nchini ili kuona umuhimu wa kujenga Viwanda na changamoto tulizonazo katika kulinda
Viwanda vyetu vya ndani kwa kutumia mifano ya bidhaa za Chuma ikiwemo Mabati, Nondo,
Saruji na Sukari. Yapo mambo mengi ambayo yanajitokeza katika kila moja. Lakini jambo
la msingi ni namna ya kuangalia kama tunapokuwa na mahitaji yanayozidi uwezo wa uzalishaji
Viwandani tuchukue hatua gani. Ni lazima kama Nchi pamoja na upungufu wa bidhaa uliopo,
sasa tuamue kulinda Viwanda vyetu vya ndani dhidi ya Ushindani usio halali kwa nguvu
zetu zote. Lazima sasa tukae tuone namna ya kudhibiti uingizaji wa bidhaa ambazo zinakwamisha
maendeleo ya Viwanda vyetu. Aidha, tuangalie njia bora ya kupunguza gharama za uzalishaji,
ikiwemo bei kubwa za umeme. Matarajio ni kwamba, baada ya kupatikana kwa Gesi tunaamini
gharama za Umeme zitapungua na kupunguza gharama za uzalishaji Viwandani.
Mheshimiwa
Spika,
67. Tumeona changamoto zinazokabili bidhaa za Mabati, Nondo, Sukari,
Ngozi na Saruji kama mfano. Ninaagiza Taasisi zetu zikiwemo Wizara ya Fedha, Wizara
ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Viwanda na
Biashara, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bodi ya Sukari, Jeshi la Polisi na Uhamiaji
kukaa kwa pamoja kuangalia njia bora ya kudhibiti uingizaji kiholela wa bidhaa zinazokwamisha
maendeleo ya Viwanda vyetu. Kwa maana hiyo ni vizuri sasa kuchukua hatua stahiki kulinda
Viwanda vyetu kuhimiza mambo muhimu yafuatayo:
i) Wizara ya Viwanda na
Biashara ni lazima sasa kuhakikisha kwamba Viwanda vyetu vinazalisha bidhaa zenye
ubora kwa Viwango vya Kimataifa. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lisaidie, lakini
lazima ubora uwe unalingana na Viwango vya Kimataifa;
ii) Wizara ya Fedha
ihakikishe kuwa bidhaa zilizomo katika kundi la bidhaa nyeti katika Afrika Mashariki
haziondolewi katika kundi hilo katika kipindi kirefu kijacho hadi hapo suala la Ruzuku
likipatiwa ufumbuzi wenye manufaa kwa Nchi changa katika Shirika la Biashara Duniani
(WTO);
iii) Wizara ya Fedha iangalie uwezekano wa watumiaji wa Industrial
Sugar wanalipia Ushuru kamili na kisha baadaye wapewe Duty Drawback baada ya kuthibitishwa
kuwa Sukari husika kweli ilitumika katika uzalishaji. Wizara ya Fedha pia iweke utaratibu
ulio bora wa uagizaji wa Sukari kufidia upungufu huu kutumia Bulk Importation, na
kisha kusambazwa kwa usimamizi madhubuti na kwa bei maalum, n.k.;
iv) Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Bodi ya Sukari wakae na kutathmini mahitaji halisi
ya Sukari, ikilinganishwa na uwezo wa Viwanda vya Sukari vilivyopo Nchini, pamoja
na kukamilisha taratibu za kisheria na kimfumo za uagizaji wa Sukari kuziba upungufu
pale inapobidi. Aidha, ni muhimu kuhimiza upanuzi katika uzalishaji wa Sukari kwa
kuhamasisha Uwekezaji mpya katika Sekta hii;
v) Utaratibu wa kuagiza
bidhaa zitakazoingizwa Nchini kuziba pengo lililopo lazima uangaliwe upya ili uagizaji
huo usiathiri Viwanda vya ndani;
vi) Tathmini ya upungufu wa bidhaa unaojitokeza
uangaliwe kwa umakini na kupanga njia bora ya kufidia upungufu huo, ikiwa ni pamoja
na kuweka utaratibu wa vibali vya kuruhusu kuingiza bidhaa Nchini. Vibali vihusishe
muda ule wenye upungufu pekee. Aidha, utaratibu wa sasa wa kutumia Wafanyabiashara
kuleta bidhaa kwa lengo la kufidia upungufu wa bidhaa husika uangaliwe upya ili kuepuka
uingizaji bidhaa kwa wingi kuliko upungufu ambako kunasababisha kudumaza Viwanda vya
ndani; na
vii) Bei za bidhaa zizingatie maeneo yanayozunguka eneo la Uzalishaji.
Kwa mfano, haitarajiwi bei ya Sukari kilo moja inayozalishwa na Kiwanda cha Sukari
cha Kagera iwe kubwa sawa na Sukari hiyo ya Kagera inavyouzwa Mtwara au Ruvuma.
Mheshimiwa
Spika,
68. Ipo mifano kwa baadhi ya Nchi Duniani ikiwemo India ambazo zimejaribu
kuweka Nembo inayoonesha kwamba bidhaa hizi zinazalishwa Nchini na bei yake ni kiasi
fulani. Lengo likiwa ni kuhakikisha kulinda watumiaji wa bidhaa hizo na kulinda pia
Viwanda. Majirani zetu Kenya wameanza kuchukua hatua katika Bajeti ya 2014 kulinda
Viwanda vyao. Kwa mfano, Serikali ya Kenya imeongeza Ushuru wa bidhaa za Chuma kutoka
Asilimia 0-10 na kufikia Asilimia 25 na kuahidi kuweka mezani Muswada mpya wa Sheria
ya Ushuru wa Forodha ili kulinda Viwanda vyake. Nasi tukidhamiria hata kama hatukufanikiwa
kwa kiasi kikubwa mwaka huu, tunaweza kufikia lengo hilo kwa mwaka ujao wa Bajeti.
Nina hakika Tukidhamiria tutaweza kufika!
UTOAJI WA ELIMU KWA WANAFUNZI
WENYE MAHITAJI MAALUMU NCHINI
Mheshimiwa Spika,
69. Sera ya Elimu na
Mafunzo ya mwaka 1995 inasisitiza kuhusu haki ya kila raia wa Tanzania kupata Elimu
wakiwemo watu Wenye Mahitaji Maalumu; Sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 1996 inayozungumzia
umuhimu wa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule kwenda na kupata elimu bora; na
Sera ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu ya 2004 – inasisitiza umuhimu wa Elimu ya watoto
wenye Ulemavu kutolewa katika mazingira Jumuishi na rafiki. Katika kutekeleza Sera
hizo, Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu bora kwa watoto wote wenye umri wa
kwenda shule, wakiwemo wenye Mahitaji Maalumu.
Mheshimiwa Spika,
70.
Kwa sasa zipo Shule za Msingi 22 ambazo ni maalum kwa ajili ya Wanafunzi wenye Mahitaji
Maalum na Shule za Msingi 354 zenye Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi hao. Jumla
ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum katika Shule za Msingi na Vitengo hivyo ni 11,689.
Aidha, ipo Shule moja ya Sekondari ambayo ni maalum kwa Wanafunzi wa Sekondari wenye
Mahitaji Maalum pamoja na Shule za Sekondari 61 ambazo zina Vitengo Maalum kwa ajili
ya Wanafunzi wa aina hiyo. Kwa sasa, wapo Wanafunzi 1,406 wenye Mahitaji Maalum waliopo
katika Shule za Sekondari Nchini.
Mheshimiwa Spika,
71. Tarehe 3
Mei 2014 nilifungua maonesho ya Elimu yaliyokuwa yameandaliwa na Wadau mbalimbali
wa Elimu kwenye Uwanja wa Jamhuri hapa Dodoma. Nilipata fursa ya kutembelea mabanda
mbalimbali yaliyokuwa yakionesha shughuli mbalimbali za elimu. Moja ya Banda nililotembelea
ni lile lililokuwa likionesha hatua mbalimbali za utoaji wa elimu maalum. Katika Banda
hilo nilielezwa njia zinazotumiwa kuwafundisha Wanafunzi wenye Mahitaji maalum hususan
Wasioona na nilioneshwa vifaa vinavyotumika na kuelezwa changamoto zilizopo.
Mheshimiwa
Spika,
72. Tarehe 4 Juni 2014 nilitembelea na kukagua Shule ya Msingi Bwigiri
– Wasioona, Wilayani Chamwino. Katika ziara hiyo nilikagua maktaba, chumba cha kompyuta,
chumba cha kutayarishia mitihani na vyoo. Niliongea pia na Wanafunzi waliokuwa wamebaki
hapo shuleni baada ya wanafunzi walio wengi kuwepo kwenye likizo. Shule hiyo ni miongoni
kwa Shule 120 za Msingi zilizoko kwenye Wilaya ya Chamwino ikiwa na jumla ya Watumishi
39 kati yao 25 wakiwa ni Walimu. Shule ina Wanafunzi 87, kati yao 61 ni Wasioona na
26 Wanaona. Jambo lililonifurahisha katika Shule hiyo ni kuwa Wanafunzi wanaohitimu
Darasa la Saba wamekuwa wakifaulu wote (Asilimia 100) kwa muda wa miaka 13 mfululizo.
Wanafunzi hao wanaofaulu wamekuwa wakijiunga na Shule Maalum za Sekondari kama vile
Shule ya Sekondari Diocese of Central Tanganyika (DCT) Mvumi n.k.
Mheshimiwa
Spika,
73. Tarehe 7 Juni 2014 nilitembelea pia Shule ya Sekondari ya Mvumi
DCT ambako baadhi ya Wanafunzi Wasioona wanasoma. Nilikutana na Walimu pamoja na Wanafunzi
wa Kidato cha Pili na Nne ambao walikuwa wanajiandaa na mitihani ya Kitaifa ya mwaka
2014. Nilifurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Serikali, Kanisa la Anglikana Nchini
na Walimu wa Shule hiyo kwa kuwawezesha Wanafunzi Wasiiona kupata haki yao ya elimu.
74. Ziara zangu hizo zilinithibitishia kuwa Walimu Nchini wakiwemo Walimu
wa Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum wanafanya kazi kubwa na ya Kizalendo ambayo inahitaji
kuungwa mkono wakati wote. Nawapongeza Walimu wote Nchini kwa kazi yao muhimu ya kutoa
elimu kwa Taifa letu. Nitumie fursa hii ya kipekee kabisa kuwapongeza Walimu na Wanafunzi
wote wa Shule ya Msingi Bwigiri – Wasioona kwa kuwezesha mafanikio makubwa na ya kuigwa
yaliyopatikana Shuleni hapo. Aidha, nawapongeza Wasimamizi wa Elimu wa Mkoa wa Dodoma,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa usimamizi
wao mzuri uliowezesha ufaulu na mafanikio hayo kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
75.
Pamoja na pongezi hizo, Ziara zangu hizo ziliniwezesha kufahamu changamoto wanazokabiliana
nazo Wanafunzi Wasioona wakiwa shuleni. Ni kweli changamoto ni nyingi, lakini kubwa
nililoliona na ambalo limewagusa Wanafunzi hao pekee ni lile la Wanafunzi Wasioona
kutofundishwa somo la Hisabati katika ngazi ya Sekondari na hivyo, kutofanya mtihani
wa somo hilo wa kumaliza Kidato cha Nne na kusababisha kushushwa madaraja yao ya ufaulu
sawa na Wanafunzi wa kawaida katika Shule zingine Nchini wasiofaulu somo hilo. Lakini
Shule hizi zinakosa vitendea kazi muhimu kama vile Braille Printer, Embossing Photocopy
Machine, Kompyuta, n.k.
Mheshimiwa Spika,
76. Ninafahamu kuwa changamoto
nyingine si za Wanafunzi wasioona tu bali zinawahusu pia Wanafunzi wenye Mahitaji
Maalum pamoja na Walimu wao kwa ujumla. Napenda kutoa wito kwa Watendaji wanaohusika
na elimu maalum Nchini kushughulikia changamoto zonazowakabili Walimu na Wanafunzi
wenye Mahitaji Maalum pamoja na Majengo ya Shule zao. Ni imani yangu kuwa kila mmoja
anayehusika atachukua hatua mapema ili kuwawezesha Wanafunzi Wasioona na wote Wenye
Mahitaji Maalum kupata elimu stahiki katika mazingira stahiki.
AFYA
Uwiano
wa Idadi ya Watu wa Vijijini na Mijini wanaohudumiwa na Daktari
Mheshimiwa
Spika,
77. Idadi ya Watanzania inakadiriwa kuwa Milioni 48.2 kati yao wanaoishi
Vijijini ni Milioni 36.6 na wanaoishi Mijini ni Milioni 11.6. Watanzania hao wanahudumiwa
na Madaktari ni 2,311 waliopo Nchini kwa sasa. Madaktari wanaoishi maeneo ya Vijijini
ni 523 na wanaoishi maeneo ya Mijini ni 1,788. Mgawanyo huu wa Madaktari unafanya
kuwa Daktari mmoja kitaifa anahudumia Wastani wa Watanzania 19,982. Kwa upande wa
Vijijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi 66,211 wanaoishi Vijijini na kwa maeneo
ya Mijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi 6,460. Hali hii inaonesha kuwa Daktari
mmoja anayehudumia maeneo ya Vijijini anahudumia zaidi ya mara kumi ya idadi ya watu
wanaohudumiwa na Daktari anayefanya kazi Mjini.
78. Kiwango hiki cha Daktari
mmoja kwa Watanzania 19,982 ni kikubwa sana ikilinganishwa na wastani wa kawaida wa
Daktari mmoja kwa Watu 10,000. Kinahitaji kupunguzwa kwa kuongeza idadi ya Madaktari
Nchini. Serikali itaendelea kugharamia elimu ya Madaktari Nchini na kuwawezesha kuwa
na mazingira bora ya kazi kwa kuzingatia hali ya uchumi wa Nchi. Nia ni kuongeza idadi
ya Madaktari wa ngazi na vitengo mbalimbali vya Afya na kuwasambaza Nchini hususan
maeneo ya Vijijini ili Daktari mmoja ahudumie Watanzania wachache zaidi. Saratani
ya Shingo ya Kizazi
Mheshimiwa Spika,
79. Serikali imeanzisha mpango
wa kitaifa wa kukinga na kuzuia saratani ya shingo ya kizazi. Aidha, Serikali itaendelea
kutoa elimu kuhusu kujikinga na saratani ya awali, kupanua vituo vya kupima dalili
za awali za saratani na kupatiwa tiba ya ugandishaji baridi kwenye Mikoa mitatu iliyobakia
ya Mtwara, Rukwa na Simiyu. Huduma ya rufaa itaboreshwa kwa wagonjwa wanaofikiriwa
kuwa na saratani kwa ajili ya tiba katika Taasisi ya Saratani ya Dar-es-Salaam. Aidha,
chanjo ya kuwakinga Wasichana wenye umri wa miaka 9-13 dhidi ya saratani imeanza kutolewa
katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kujifunza mfumo wa kutumia Shule kwa ajili ya kutoa
chanjo hii nchi nzima.
HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
80. Kwa ujumla hali ya usalama katika Mipaka yote ya Nchi yetu inaendelea kuwa
shwari licha ya kuwepo changamoto kadhaa. Mathalani katika Mpaka wa Kaskazini ambapo
Tanzania inapakana na Kenya na Uganda kumekuwepo na changamoto ya Wahamiaji haramu
hususan katika Wilaya za Misenyi na Karagwe na changamoto ya uharibifu wa alama za
Mipaka. Aidha, katika Mpaka wa Kusini pamekuwepo na changamoto ya utata wa Mpaka kati
ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa na changamoto ya ujenzi holela unaofanywa
na Wananchi waishio Mpakani eneo la Tunduma.
Mheshimiwa Spika,
81.
Serikali kupitia Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti hali hiyo ikiwa ni
pamoja na kufanya mazungumzo ya pamoja baina ya Wataalamu wetu na Wataalamu wa Nchi
hizo jirani kwa mfano:
i) Tarehe 05 hadi 12 Octoba, 2013 Mjini Arusha vilifanyika
Vikao vya pamoja kukagua, na kuhakiki Mpaka kati ya Tanzania na Kenya;
ii)
Mwezi Februari 2014 Jijini Dar es Salaam kilifanyika kikao cha kuboresha Mipaka ya
Tanzania, Burundi, Zambia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika ziwa Tanganyika;
iii)
Mwezi Mei, 2014 kilifanyika Kikao cha TUME ya Uimarishaji na Uhakiki wa Mpaka baina
ya Tanzania na Burundi Mjini Ngara.
Mheshimiwa Spika,
82. Pamoja
na kwamba kwa ujumla hali ya usalama wa Mipaka yetu ni shwari, bado Nchi yetu kama
sehemu ya Afrika Mashariki inakabiliwa na tishio la mashambulizi ya Kigaidi ambalo
linawakumba Majirani zetu. Serikali kupitia Jeshi la Wananchi Tanzania inaendelea
kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Nchi jirani, Nchi Marafiki pamoja
na Jumuia ya Kimataifa ili kukabili tishio hilo. Nitoe wito tena kwa Wananchi wetu
kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Vyombo vya Usalama katika kuhakikisha Nchi yetu inakuwa
salama wakati wote.
AJALI ZA BARABARANI
Mheshimiwa Spika,
83.
Suala la ajali za barabarani bado ni changamoto kubwa hapa Nchini likichangia vifo
na majeruhi wengi na uharibifu wa mali. Pamoja na hatua mbalimbali za kisheria, bado
kumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha Januari
2011 hadi Mei 2014, jumla ya Ajali 78,654 ambazo zilisababisha Vifo 13,375 na Majeruhi
67,936 zilitokea. Hii ni idadi kubwa ya ajali, vifo na majeruhi.
Mheshimiwa
Spika,
84. Ziko sababu mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa ajali za barabarani
zikiwemo makosa ya kibinadamu (Uzembe wa Madereva, Ulevi, Mwendokasi na Uegeshaji
mbaya wa magari barabarani n.k.) ambayo kwa ujumla yanachangia Asilimia 77 ya ajali
zote zinazotokea, ubovu wa vyombo vya moto unaochangia Asilimia 16, na mazingira ya
barabara yaani ubovu wa miundombinu na hali ya hewa vinavyochangia Asilimia 7.
Mheshimiwa
Spika,
85. Katika kukabiliana na ajali za barabarani, Serikali kupitia Vyombo
mbalimbali imechukua hatua za kuimarisha mafunzo kwa Madereva kwa kutunga Kanuni zinazowalazimisha
kusoma masomo ya umahiri wa kuendesha magari ya abiria na magari makubwa ya mizigo
(HDV); kudhibiti mwendokasi na kuanzisha Mfumo wa kufuatilia mwendo wa Mabasi na Malori
utakaodhibiti makosa mbalimbali ya usalama barabarani. Hatua nyingine ni kuanzisha
mfumo wa uwekaji nukta (Point system) katika Leseni za Madereva ili kuwaondoa barabarani
madereva wanaokithiri kwa makosa, kupima kiasi cha ulevi kwa Madereva; na kupanua
wigo wa elimu ya usalama barabarani kwa njia ya televisheni, redio, simu na magazeti.
Kwa upande wa Usimamizi wa Sheria zilizopo, hatua stahiki zinachukuliwa kwa kuongeza
usimamizi na mafunzo kwa watendaji wote wanaosimamia Sheria ili kuwaongezea ufanisi
na kudhibiti nidhamu yao. Watendaji wanaokiuka maadili ya kazi wanachukuliwa hatua
za kinidhamu.
Mheshimiwa Spika,
86. Kwa upande wa ubovu wa vyombo
vya moto, Serikali inaandaa Kanuni za Ukaguzi wa Lazima. Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT) kimekamilisha ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa magari ikiwa ni pamoja
na mitambo ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Ninatoa wito pia kwa Sekta Binafsi
kujitokeza kuwekeza katika eneo hili ili mitambo hii iwepo ya kutosha. Aidha ni muhimu
sasa kuanzisha Gereji maalum kwa ajili ya matengenezo yatakayokuwa yanapimwa kwa mfumo
huu. Sambamba na hatua hizo, Jeshi la Polisi pia linaandaa Kanuni zitakazowalazimu
Madereva kubandika mkanda ang’avu kuzunguka magari makubwa ya mizigo na mabasi ili
kusaidia kuongeza muonekano wa magari hayo wakati wa giza.
Mheshimiwa Spika,
87. Pamoja na jitihada hizo za Serikali za kuandaa Kanuni mbalimbali, Sheria mpya
ya Usalama Barabarani inaweka muundo bora wa usimamizi wa shughuli za Usalama barabarani
kwa kuweka hitaji la kuundwa kwa Taasisi Kiongozi ya Usalama Barabarani (Road Safety
Lead Agency). Sheria hiyo itaanisha majukumu ya Taasisi Wadau wa Usalama Barabarani
na kuratibu utekelezwaji wa majukumu ya Taasisi hizo. Uwepo wa Chombo hiki utaongeza
uwajibikaji wa kila Taasisi katika eneo lake tofauti na sasa ambapo suala la usalama
barabarani linachukuliwa kama jukumu la Polisi pekee. Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Taasisi na Wadau mbalimbali wanafanya mapitio ya rasimu ya Muswada huu ambao mara
utakapokamilika utawasilishwa Bungeni.
MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI NA VIKONGWE
Mheshimiwa
Spika,
88. Nchi yetu bado inaendelea kukumbwa na tatizo la Mauaji ya Watu
wenye Ulemevu wa Ngozi na Vikongwe kwa imani za ushirikina. Katika kipindi cha mwaka
2012 hadi 2014, takwimu zinaonesha kwamba jumla ya Watu 3 wenye Ulemavu wa Ngozi waliuawa
katika Mikoa ya Arusha, Tabora na Simiyu na wengine 2 walijeruhiwa katika Mkoa wa
Rukwa. Kufuatia matukio hayo, watuhumiwa 8 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa
mauaji na wengine 4 wanashtakiwa kwa kujeruhi. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya
Vikongwe 1,393 waliuawa kikatili katika Mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu, Mwanza,
Tabora, Singida, Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa.
Mheshimiwa Spika,
89. Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili, Serikali inachukua hatua ya kuzihusisha
Kamati za Ulinzi na Usalama za ngazi mbalimbali kuanzia Vitongoji na Mitaa katika
mapambano dhidi ya mauaji ya Vikongwe kwa kufanya Mauaji ya Watu wenye Ulemavu na
Vikongwe kuwa Agenda ya kudumu katika Mikutano yao. Aidha, tutaendelea kutoa elimu
kwa Wananchi kupitia Vyombo vya Habari, Viongozi wa Dini na Watu mashuhuri katika
maeneo husika ya kuepukana na imani potofu za ushirikina. Jeshi la Polisi linaendesha
Program mbalimbali kuelimisha Jamii kukabiliana na uhalifu kufanya ufuatiliaji wa
matukio ya mauaji ya Vikongwe ikiwa ni pamoja na kuweka mkakati wa kuharakisha upelelezi
wa kesi za matukio ya Mauaji.
MAUAJI YA WANAWAKE MKOANI MARA
Mheshimiwa
Spika,
90. Pamoja na Mauaji ya Vikongwe na Watu wenye Ulemavu wa Ngozi katika
Mkoa wa Mara kumetokea mauaji ya kinyama ya Wanawake kutokana na sababu za kishirikina
katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014 hususan katika Wilaya za Butiama na Musoma.
Waathirika wa matukio haya walikuwa wakiuawa kwa kunyongwa kwa kutumia khanga nyakati
za mchana wakiwa katika shughuli zao na hivyo kusababisha hofu kubwa katika Jamii.
Jumla ya matukio tisa (9) ya kuuawa Wanawake yaliripotiwa katika Kata nne za Mugango,
Etaro, Nyegina na Nyakatende.
Mheshimiwa Spika,
91. Kufuatia matukio
hayo Serikali kupitia Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Mkoa imechukua hatua za haraka na jumla ya watuhumiwa 15 wamekamatwa na kufikishwa
Mahakamani kwa kesi za mauaji. Aidha, Kikosi Kazi cha Makosa dhidi ya Binadamu na
vitendea kazi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kikiongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai Tanzania Kamishna ISAYA MNGULU walifika Mkoani Mara kwa ajili ya
ufuatilia wa karibu wa kitaalamu wa matukio haya. Timu hiyo wenye Wataalam mahiri
katika eneo la Upelelezi wanaendelea kufuatilia matukio haya sambamba na kutoa elimu
juu ya Ulinzi Shirikishi wa namna ya kukabiliana na matukio kama haya,ikiwa ni pamoja
na kutoa elimu zaidi kuhusu uhalifu huu na kufanaya Operesheni ijulikanayo kama “Zuia
Mauaji ya akina Mama Wilaya ya Butiama.”
Mheshimiwa Spika,
92.
Kutokana na juhudi hizo, hali ya Usalama katika maeneo hayo imeimarika na matukio
hayo hayajajitokeza tena. Napenda kutoa wito kwa Wananchi wote kutambua kuwa jukumu
la ulinzi ni la kila Mwananchi, hivyo hatuna budi kuwafichua wale wote wanaofanya
uhalifu katika Jamii. Lengo ni kuwalinda Wananchi na kuhakikisha kuwa maeneo tunayoishi
yanakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha ili Wananchi waendelee na shughuli zao za
uzalishaji badala ya kuhofia maisha yao.
MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI
WA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
93. Kama wote tunavyofahamu, Bunge Maalum
la Katiba liliaanza majukumu yake mapema mwezi Februari 2014 ambapo katika kipindi
hicho Wajumbe walikamilisha kuandika na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la Katiba,
kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Bunge Maalum, Wajumbe kujadili Sura ya Kwanza na ya
Sita ya Rasimu ya Katiba hiyo na Kamati za Bunge Maalum kuwasilisha maoni yao Bungeni.
Hata hivyo, na kwa masikitiko makubwa wakati tukiwa katika hatua za uwasilishaji,
baadhi ya Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba na Wananchi (UKAWA) waliamua kutoka nje
ya Bunge kwa sababu ambazo wanazijua wao.
Mheshimiwa Spika,
94.
Wote tunafahamu kuwa, Bunge Maalum la Katiba lina Wajumbe wa aina tatu wakiwemo Waheshimiwa
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza
la Wawakilishi na Wajumbe 201 wanaotoka katika Makundi mbalimbali. Kwa kuwa Waheshimiwa
Wabunge wote wa Bunge hili ni sehemu ya Wajumbe wa Bunge Maalum, naomba nitumie fursa
hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa ujumbe mfupi kwa Wajumbe wa Bunge Maalum ambao
naamini utaweza kuwafikia popote walipo.
Mheshimiwa Spika,
95. Kifungu
cha 26 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinatoa masharti na mamlaka ya Bunge
Maalum kutunga Kanuni kwa ajili ya kuendesha shughuli za Bunge Maalum. Ni kwa kupitia
mamlaka kama ilivyofafanuliwa katika Kifungu hiki, Wabunge wa Bunge Maalum waliweza
kutunga Kanuni za Bunge Maalum kwa maridhiano kwa muda wa takriban mwezi mmoja. Vilevile,
ni kupitia Kanuni hizo, Viongozi wa Bunge Maalum waliweza kuchaguliwa na kufanya Bunge
hilo kuwa Chombo Maalum chenye Uongozi na kuwa na Mamlaka yake ya Kisheria.
Mheshimiwa
Spika,
96. Kanuni ya 46 ya Bunge Maalum la Katiba inaeleza mambo yasiyoruhusiwa
kwenye Bunge Maalum yakiwemo kutumia lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au inayodhalilisha
watu wengine. Aidha, Kanuni hii ya 46 inatoa utaratibu mzima wa jinsi ya kushughulikia
masuala haya ndani ya Bunge Maalum. Kanuni ya 16 (3) inatoa nafasi kwa Mjumbe au Wajumbe
wa Bunge hilo ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mwenyekiti uliotolewa, kuwa atakuwa
na haki ya kuwasilisha kwa maandishi malalamiko yake kwa Katibu ndani ya siku moja
kuanzia tarehe ya uamuzi.
97. Kwa muendelezo huo huo, Kanuni ya 59 (1) (d)
inaelekeza kuwa, moja ya majukumu ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum ni kuchunguza
kuhusu masuala yote ya haki, kinga na madaraka ya Bunge Maalum yatakayopelekwa kwenye
Kamati hiyo na Katibu kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa
kwenye Bunge Maalum. Kutokana na utaratibu huo wa Kikanuni kama ilivyoainishwa katika
Kanuni hizo za Bunge Maalum, ninapenda kutumia fursa hii kuwashauri “Wana UKAWA” ambao
wengi wao wamo ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wenzangu
wote wa Bunge Maalum ambao wamo ndani na nje ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa ujumla wetu kutumia mifumo iliyowekwa na Bunge Maalum kupeleka malalamiko
yote katika Kamati ya Kanuni ya Bunge Maalum ili yapatiwe ufumbuzi ndani ya Bunge
Maalum na siyo nje ya Bunge. Hilo ndilo jambo la busara!!
Mheshimiwa Spika,
98.
Mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya, ambao kimsingi ni wa Kisheria umeanza siku nyingi
na kwa hatua mbalimbali shirikishi kwa makundi ya watu na Vyombo mbalimbali, kupokezana
majukumu kwa lengo la kufanikisha azma ya kupata Katiba Mpya. Ninapenda kuwakumbusha
Wajumbe wenzangu wa Bunge Maalum la Katiba popote walipo ndani na nje ya Bunge hili
kuwa, kuwepo kwetu katika Bunge Maalum la Katiba ni jambo la Kisheria na si jambo
la kawaida wala la hiari. Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, sote kwa ujumla wetu
tuna wajibu wa kukamilisha sehemu yetu kama Wajumbe wa Bunge Maalum kwenye mchakato
mzima wa kuandaa Katiba Mpya.
Mheshimiwa Spika,
99. Vilevile, napenda
kukumbusha kuwa Bunge Maalum la Katiba si hatua ya mwisho ya mchakato huu. Baada ya
Bunge Maalum la Katiba kumaliza wajibu wake, Rasimu itakayokuwa imependekezwa na Bunge
Maalum itatakiwa kuwasilishwa kwa Wananchi wote wa Tanzania waisome, waielewe na kisha
waweze kuipigia kura ya maoni kuikubali au kuikataa kwa mujibu wa Sheria iliyopo ya
Kura ya Maoni mwaka 2013. Hivyo, ni vyema tukaelewa vizuri suala hili na kwamba, bado
kuna Wananchi wenzetu wengi kwa idadi ambao nao wanasubiri haki yao ya Kisheria katika
kukamilisha mchakato huu kabla ya kupata Katiba Mpya. Hivyo tusiwanyime haki hiyo!
100.
Ninapenda kuwashauri Wajumbe wenzangu ambao wameamua kususia Vikao vya Bunge Maalum
la Katiba kutafakari uamuzi na matendo yao kwa kutambua masharti ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na wajibu wao kwa Wananchi. Sisi wote
tuliopo hapa tuna wajibu huo wa kukamilisha kazi hii muhimu tuliyopewa kisheria ya
kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata Katiba Mpya.
101. Hivyo, natoa wito
kwa Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba ambao wamesusia Vikao vya Bunge Maalum
la Katiba, warejee kwenye Bunge hilo ili tuweze kuendelea na Mjadala wa Rasimu ya
Katiba huku tukitumia utaratibu mzuri wa maridhiano uliowekwa Kikanuni kutatua tofauti
zilizopo.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
102. Changamoto kubwa
iliyoko mbele yetu baada ya kuwepo hapa Bungeni kwa takriban miezi miwili ni kusimamia
utekelezaji wa Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha. Sisi kama Wabunge tuondoke hapa
kwa lengo moja la kushirikiana na Wananchi kusukuma maendeleo na Bajeti tuliyoipitisha
ikiwa ndiyo kichocheo kikuu. Twendeni tukasisitize umuhimu wa kuishi kwa amani, upendo
na mshikamano. Tukiwasimamia vizuri na kuwaongoza Wananchi katika matumizi ya rasilimali
hata kama ni kidogo kiasi gani, Nchi yetu itasonga mbele kimaendeleo na maisha bora
kwa Wananchi wetu yatapatikana.
SHUKRANI
Mheshimiwa Spika,
103.
Baada ya kusema hayo, napenda hasa nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha
Mkutano huu. Nikushukuru kwa namna ya pekee wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika na Naibu
Spika kwa kutuongoza vizuri kulingana na Kanuni za Bunge. Aidha, nimshukuru Mwenyekiti,
Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala kwa kuongoza vizuri baadhi ya Vikao
vya Bunge wakati wa Mkutano huu. Ninawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango
yenu ya dhati na yenye Mantiki kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu. Niwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Watumishi na Wataalam wote wa Serikali waliosaidia kujibu
Maswali na hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge zilizojitokeza hapa wakati wa Mkutano
huu. Vilevile, nawashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kuwapatia Wananchi habari
kuhusu Majadiliano yaliyokuwa yanaendelea hapa Bungeni. Wote kwa ujumla wenu nawashukuru
sana.
Mheshimiwa Spika,
104. Kipekee napenda kuwashukuru Madereva
wote ambao wamekuwa makini katika kazi ya kuwaendesha Viongozi wote, wakiwemo Waheshimiwa
Wabunge na Wataalam kutoka shemu mbalimbali Nchini na kuwawezesha kufika hapa Dodoma
kuhudhuria Mkutano huu wa Kumi na Tano. Vilevile, nawashukuru Wananchi wa Mkoa wa
Dodoma, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt. Rehema Nchimbi kwa ukarimu wao
kwa muda wote tuliokaa hapa Dodoma. Nivishukuru pia Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo
vimehakikisha muda wote tumekaa kwa Amani na Utulivu mkubwa. Mwisho namshukuru Katibu
wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah na Watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa huduma nzuri
zilizowezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano huu bila matatizo.
Mheshimiwa
Spika,
105. Nitumie fursa hii kuwaombea safari njema mnaporudi katika maeneo
yenu ya kazi. Lakini pia niwaombee kheri na Baraka tele Waislamu wote ambao wameanza
na wanaendelea na Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kila atakayeamua kufanya Ibada
hiyo aifanye kikamilifu na kama Kitabu cha Quran Tukufu kinavyoelekeza.
Mheshimiwa
Spika,
106. Baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu
sasa liahirishwe hadi tarehe 04 Novemba, 2014 siku ya Jumanne, Saa 3:00 Asubuhi litakapokutana
katika Mkutano wa 16 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.