2014-06-28 08:24:31

Kuna vizingiti, lakini msikate tamaa!


Baraza la Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, limehitimisha mkutano wake wa 47 uliokuwa unafanyika mjini Roma kwa kuwataka wajumbe kusonga mbele katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao, licha ya vikwazo na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo kwenye Makanisa ya Mashariki.

Wajumbe wamepata kusikiliza ushuhuda uliotolewa na viongozi wa Kanisa kutoka Romania, kwa kuangalia masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, mambo ambayo ni sehemu ya maisha ya kawaida huko Romania. Wamepembua kuhusu athari za myumbo wa uchumi kimataifa na matumaini ya wananchi wa Romania kwa sasa na kwa siku za usoni baada ya kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti kunako mwaka 1989.

Wajumbe wamesikiliza ushuhuda unaotolewa na Wakristo wa Makanisa ya Mashariki kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kuendeleza majadiliano ya Kiekumene pamoja na kushirikishana utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa kwenye Liturujia mbali mbali za Makanisa ya Mashariki.

Sakramenti ya Ndoa; mahusiano kati ya Bwana na Bibi; kanuni msingi na maadili za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu ni kati ya mada zilizopatiwa umuhimu wa pekee, kwa kuzingatia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wajumbe wameangalia kuibuka na kukua kwa vijana wa kizazi kipya, watoto wanaoishi katika ulimwengu wa digitali unaoendelea kuwazingua vijana kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Hapa kuna umuhimu kwa wadau mbali mbali kuwasaidia vijana katika malezi na majiundo yao kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema. Vijana wafundwe kuwa na matumizi bora na sahihi ya mitandao ya kijamii wanapokuwa shuleni au majumbani mwao!

Tatizo la wakimbizi na wahamiaji kutoka katika Makanisa ya Mashariki na umuhimu wa kupata huduma za maisha ya kiroho ni mambo ambayo pia yamejadiliwa kwa kina na mapana na kwamba, waamini wanapaswa kushirikishana utajiri unaofumbatwa katika maisha, liturujia na Mapokeo ya Kibizantini. Waamini wawe ni mashahidi wanaozingatia misingi ya demokrasia ya kweli kwa kuondokana na rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma. Kanisa lioneshe ushuhuda huu si tu kwa kunyooshea watu kidole, bali kwa njia ya ushuhuda makini na wenye mashiko.

Wakati wa madhulumu, wakristo walishikamana, wakaonesha ujasiri na msimamo wao katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini bado wanaendelea kuchangamotishwa kuonesha ushuhuda wa maendeleo ya maisha yao ya kiroho kwa kushikamana na wakristo kutoka kwenye Makanisa ya Mashariki.

Imekwishagota miaka 25 tangu Serikali ya Ukraini, ilipotoa uhuru wa kidini, hali nchini humo bado ni tete na kwamba, usalama wa maisha ya watu uko hatarini. Lakini wananchi wa Ukraini wanakumbushwa kwamba, ulinzi na usalama uko mikononi mwao, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwapatia msaada wa kudumisha mambo msingi ambayo tayari wanataka kuyafanyia kazi kwa ajili ya kudumisha umoja wa kitaifa, amani na utulivu.

Kanisa kwa upande wake, linapaswa kuendelea kuimarisha mikakati ya shughuli za kichungaji Parokiani, kwa njia ya Liturujia, huduma za kiroho kwa waamini pamoja na kubainisha mikakati ya maendeleo kwa mtu mzima: kiroho na kimwili. Wahamasishe miito mitakatifu ili kuwa na viongozi wa Kanisa watakaoweza kuganga na kuponya madonda ya chuki na utengano uliojionesha nchini Ukraini.

Wakristo wa Makanisa ya Mashariki wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kutoka kimasomaso kutangaza Injili ya Furaha, licha ya vikwazo na changamoto zilizoko mbele yao: kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimaadili. Viongozi wa Makanisa haya wanawashukuru waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya waamini huko Mashariki ya Kati kwa kuchangia kwa hali na mali. Mchango huu ni kielelezo cha mshikamano wa upendo miongoni mwa Wakristo.

Wajumbe wanawahamasisha Wakristo kutoka Mashariki ya Kati kuendelea kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pasi na kukata tamaa kwani kuna cheche za matumaini ya amani ya kudumu, baada ya Papa Francisko kukutana na kusali na wakuu wa nchi kutoka Palestina na Israeli.







All the contents on this site are copyrighted ©.