2014-06-28 08:59:48

Itifaki ya ushirikiano kati ya Serbia na Vatican


Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Ijumaa tarehe 27 Juni 2014 ameongoza ujumbe wa Vatican katika kutia sahihi Itifaki ya makubaliano kati ya Vatican na Serikali ya Serbia kuhusu Serikali kushirikiana na Kanisa katika utoaji wa elimu ya Sekondari. Ujumbe kutoka Serikali ya Serbia uliongozwa na Bwana Veljko Odalovic, Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya nchi za nje.

Itifaki hii inawahamasisha viongozi wa pande hizi mbili kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuendeleza elimu ya sekondari kwa njia ya mawasiliano ya mara kwa mara. Itifaki hii inatambua pia vyeti vinavyotolewa kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za Sekondari zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa nchini Serbia. Itifaki ya Mkataba huu itaanza kutekelezwa baada ya pande zote mbili kuhitimisha masharti, utekelezaji wake na masuala ya fedha. Itifaki inalipatia Kanisa uwezo wa kuanzisha na kuendeleza shule za Sekondari zinazofundisha masomo ya Kanisa na elimu dunia.

Mwishoni, taarifa kutoka Belgrade inasema kwamba, Itifaki hii itaanza kutumika rasmi mara tu baada ya pande hizi mbili kukamilisha masharti yote yaliyotajwa katika itifaki ya ushirikiano kati ya Serikali ya Serbia na Kanisa Katoliki nchini Serbia.







All the contents on this site are copyrighted ©.