2014-06-27 07:40:58

Onesheni huruma na mapendo kwa wagonjwa!


Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, amri kuu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. RealAudioMP3

Naam, “Upendo mkuu” ndiyo kauli mbiu itakayoongoza Onesho la Sanda Takatifu, Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia. Onesho hili litafanyika kuanzia tarehe 19 Aprili na tarehe 24 Juni 2015, siku ambazo waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kupata nafasi ya kusimama kidogo na kufanya tafakari ya kina kuhusu Sanda Takatifu.

Sanda hii inayomwonesha mtu aliyeteseka; akapigwa mijeledi na kuvishwa taji la miba. Ni mtu aliyefariki dunia, lakini baada ya siku tatu, akafufuka kutoka katika wafu. Upendo ndiyo changamoto endelevu inayotolewa na Krisdto pamoja na Kanisa lake kwa watu wa nyakati zote. Kila mtu anaalikwa kujisadaka kwa ajili ya jirani zake. Hivi ndivyo anavyosema Askofu mkuu Cesare Nosiglia, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Torino.

Changamoto ya mtu kujisadaka kwa ajili ya wengine ni endelevu na inamgusa kila mtu kadiri y anafasi na dhamana yake ndani ya Kanisa na Jamii inayomzunguka. Watu wanaweza kujisadaka kwa kutoa muda wao kwa ajili ya matendo ya huruma kwa Mungu na jirani: kwa kuwatembelea na kuwahudumia wagonjwa na wazee wasiojiweza. Sanda Takatifu iwakumbushe waamini na watu wenye mapenzi mema taabu na mateso ya wagonjwa wanaokufa hospotalini kwa kukosa huduma makini, woga na upweke.

Waamini waguswe na mateso ya wagonjwa, ili waweze kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Sanda Takatifu iwachangamotishe watu kutoa huduma makini kwa wale wanaowahudumia: kiroho na kimwili; waoneshe moyo na mshikamano wa udugu na upendo, kwa kutembea katika shida na mahangaiko ya wagonjwa hawa. Sanda Takatifu inagusa undani wa maisha ya mtu, ambaye baada ya kuiona kamwe hawezi kubaki kama alivyokuwa bila ya kuguswa na mahangaiko ya watu.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia anasema kwamba, Sanda Takatifu ya Torino ina uhusiano mkubwa na mateso na kifo cha Yesu, mwaliko wa kuthamini na kuenzi maisha ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu wasikubali kukumbatia utamaduni wa kifo, bali wasimame kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Watu waguswe na mateso ya wagonjwa wanaoishi kwa matumaini; watu ambao daima wanakiona kifo usoni pao!

Pengine wagonjwa kama hawa si watu wa kulalama; ni watu ambao wamepokea na kuukubali mpango wa Mungu katika maisha yao! Waamini wanapotembelea Wodi za wagonjwa mahututi, waguswe ili kuwaonjesha upendo, kama walivyofanya watakatifu kama Mama Theresa wa Calcutta, Mtakatifu Vincent wa Paulo na watu wengine wengi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi; wale wanaosimama usiku na mchana wakisikiliza kilio cha damu kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; watu ambao wanataka kuenzi Injili ya Uhai. Sanda Takatifu ichochee moyo wa toba na wongofu wa ndani; moyo wa huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.