2014-06-27 16:34:06

Mtetezi wangu yu hai!


Mahubiri ya Mhashamu Askofu Gervas Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo la Mpanda katika Parokia ya Mtakatifu Gaudence, Makoka siku ya alhamisi 26 Juni 2014 wakati wa ibada ya Misa Takatifu ya kumwombea na kumuaga Marehemu Sr Crescentia Kapuli wa Shirika la Watawa wa Bikira Maria Malkia wa Afrika, Jimbo Katoliki Mbeya aliyeuwawa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi siku ya Jumatatu tarehe 23 Juni 2014 katika eneo la Riverside Jijini Dar Es Salaam.

Ndugu zangu waamini na wageni wetu wote,
Tumsifu Yesu Kristo! ......................................... Milele Amina.

Ndugu wapendwa, ni vigumu kidogo kutoa mahubiri siku kama ya leo, na hasa ukizingatia tukio lenyewe linaleta kigugumizi kidogo kutoa mahubiri. Lakini basi tunapohubiri hatuubiri yale tunayopenda, yale ambayo tunatamani sisi, tunahubiri yale ambayo Roho wa Mungu anatusukuma tuseme. Basi ninawaalikeni tutafakari machache.

Ndugu wapendwa, kifo cha Sista Crescentia Kapuli kimewastua wengi na wa mbali na wa karibu wanashindwa kuamini kama ndivyo hivyo kilivyokuwa na kama sababu ndizo hizo na wengine hawaamini kama ni kweli amefariki. Lakini ni kweli amefariki na leo hapa palikokuwa nyumbani kwake kwake anaagwa.

Sista Kapuli anakwenda kupumzishwa/kulazwa/kuzikwa, na anatuachia maswali mengi. Pengine maswali hayo hatuwezi kupata majibu yake sasa katika wakati kama huu angekuwa anaweza kusema tungemuuliza maswali, tungemuuliza Sista Kapuli! Ilikuwaje, bila shaka tungemuuliza na ninaamini asingekuwa najibu refu, asingekuwa na jibu refu na ndilo jibu analotupa sasa.

Anasema kama Ayubu, “Laiti maneno yangu yangeandikwa” akimaanisha yangebaki watu wasome, wajifunze. Laiti maneno yangu yangeandikwa. Ayubu ni kati ya watu wa nyakati hizo za zamani alipita majaribu makubwa ikiwemo kupoteza mali zake na kupata mateso makubwa ya kimwili, ya kiroho, ya kijamii na hata ya kiakili.

Na katika mazingira yake wengi waliamini amelaaniwa na Mungu na wakamshawishi amuache Mungu. Lakini yeye akasema “laiti maneno yangu yangendikwa”, yangeandikwa ili yadumu, lakini basi hayajaandikwa, lakini anasema “najua wazi mkombozi wangu anaishi”. Na huyu mkombozi wangu mwishowe atanipa haki yangu hapa duniani. (Ayubu 19:25).

Nafikiri Sista Kapuli angewaza kusema hivyo hivyo: “najua wazi mkombozi wangu anaishi, mwili wangu umeharibiwa, uwezo wangu wa kuishi umeondolewa, lakini pamoja na kuharibiwa mwili wangu huu, najua mkombozi wangu anaishi, atanipa haki yangu hapa hapa duniani. Tutasema “atasemaje hivyo”? ni kweli bado tunaye na bado atalazwa katika maeneo yetu/ ardhi yetu, kaburi lake litakuwepo nasi siku zote. Kwa hiyo ana haki ya kusema atanipa haki yangu hapa hapa duniani.
Yeye pekee angeweza kusema ukali wa maumivu aliyopata, mateso aliyopata na angeweza kutuambia na nani aliyefanya vile, lakini amebadilisha mwelekeo wake, hamtazami aliyetenda hicho, hamtazami aliyemtenda hayo, anamtazama mkombozi wake; “Najua mkombozi wangu yu hai, atanipa haki yangu. Kwa nini hamtazami aliyetenda hivyo? Kwa sababu anajua kuishi kwake na kufa kwake ilikuwa kwa ajili ya Mungu, sio kwa ajili yake yeye mwenyewe.

Mtume Paulo amewaambia Warumi, “ iwapo twaishi au tunakufa ni kwa ajili ya Mungu”. Kwa hiyo analielekeza tumaini lake kwa mkombozi wake, “mkombozi wangu yu hai, na atanipa haki yangu na mwisho nitamwona Mungu” Haya yatakuwa ni maneno yake Sista Crescentia alipofariki hayatuondolei msiba, hayatuondolei uchungu tulio nao, lakini ni maneno yake ya kutupa sisi faraja, ya kutujenga kiimani.
Ningekuwa najua walihusika kwa namna moja au nyingine kwa kifo cha Sista wako hapa, ningekuwa najua aliyekula njama hiyo au aliyemsaliti sista kwa namna mojawapo basi ningewauliza, unapata faida gani kutoa uhai wa mwanadamu mwenzako ili hali na wewe siku moja utakufa? Unapata fahari gani? Yawezekana amesukumwa na tamaa fedha, yawezekana, kwamba, walifikiri sista ana fedha, au yawezekana kuna mtu aliwatuma kwamba atawapa fedha, yawezekana, lakini fedha hizo zina raha gani, fedha hizo za damu, fedha hizo zina raha gani, utapata faida gani?

Wanaweza kusema maisha ni magumu lakini ugumu wa maisha unaondolewa kwa kumwaga damu?, ugumu wa maisha unaisha kwa kuua? Unapomuua mwanadamu mwenzako ni sawa na unajiua mwenyewe. Hivi hivi wahenga walisema “auae kwa upanga atakufa kwa upanga”. Maandiko yanasema “tamaa ikikua inazaa dhambi na dhambi ikikua inazaa mauti”.

Uuaji huu una faida gani kwa anayetenda. Hata hapa hatuwezi kupata jibu kwa sababu hawawezi kuwa na ujasiri wa kutujibu au pengine hawako hapa au pengine hawajui kiswahili, inawezekana. Hakuna faida kuua ili kupata unafuu. Hakuna faida wala hakuna raha kupata mali kwa kuangamiza. Na wala kupata mali kwa kuangamiza hakuondoi ugumu wa maisha. Sana sana tunajenga uasi na mwisho wa dhambi ni mauti vile vile.

Tukumbuke, tukumbuke tunaokuwa na maelekeo ya kudhulumu uhai kwa sababu hizi za kimaisha. Tukumbuke, tukumbuke kila anayeishi na anayekufa ni wake Mungu. Sisi sote ni wake Mungu tuwe tunaishi au tumekufa. Tukumbuke kila wakati kwamba, Maandiko yanatumbia “sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu”.

Nafikiri pengine mtu ambaye amepungukiwa kabisa akili hawezi kuelewa kwamba yeye ni kiumbe. Tukumbuke kwamba, sisi sote ni viumbe wa Mungu, pamoja na tabia zetu mbaya, pamoja na mipango yetu mibaya, sisi sote ni viumbe wa Mungu. Na mtume Paulo alipowaambia Warumi (14:10), anatuambia na sisi: “sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu ya Mungu”. Ndiyo maana Sista anasema “mtetezi wangu yu hai, atanipa haki yangu”.

Mtume Paulo anasema “kila mtu atatoa habari zake mwenyewe mbele yake”. Sasa ni ipi ingekuwa mbegu safi?, ni mbegu ya wokovu, ni mbegu inayoita kwenye toba, ni mbegu inayoalika kwenye toba, inayoalika mageuzi. Kwamba, kwa kutenda hivi, matokeo yake ni haya, mabaya hivi, yanayowafanya watu kwa maisha yote wanasononeka, wanatokwa na machozi, kwa sababu tu ya mkono wangu, yanayowafanya watu wanaacha shughuli zote nyingine na kubaki wanahangaika kwa sababu tu ya mkono wangu, kwa sababu tu ya mipango yetu, kwa sababu tu ya kutamani hizo fedha, na hivyo tumefanya kitendo ambacho kimeondoa uhai wa mwanadamu mwenzetu, na yeye alinyonya kama sisi na anaishi kama sisi, ni kitu kibaya, ni mwaliko wa toba na wongofu na wa mageuzi. Ni mwaliko unaoita mabadiliko.

Si tukio la pekee hili katika nchi yetu. Yanatokea matukio kama haya. Lakini hatuwezi kuacha kutoa mwaliko huo, ndiyo jibu pekee, kwamba, kwa kuuana hatuwezi kuondoa ugumu tunaouona maishani petu, kwa kuuana hatuwezi kupata utajiri na ustawi tunaoutamani, kwa kuuana hatuwezi kutuliza hasira yetu au chuki yetu tuliyo nayo. Tutaendelea kusema hivyo na hatuna njia nyingine. Ni hili hasa linaloweza kutuhakikishia amani na utulivu tunaoutamani.
Niliwahi kusali na wafungwa mahali fulani. Waliniambia: “Baba tunaomba utupelekee salamu kwa watanzania, uwambie kwamba, tumekosa. Pili tunaahidi kutokurudia na tatu watupe nafasi tena tushuhudie kwamba, sisi pia tunaweza kuwa watu wema”. Na mmoja akaniambia: “tena nikitoka nitakuwa mhubiri kuliko hata ninyi”.

Alikuwa anaongea maneno yanayomtoka moyoni, lakini bado unasema, lakini mbona bado pamoja na hivi mnavyosema bado unasikia kwingine mtu ametenda kitu kibaya kingine tena, pengine kibaya zaidi kuliko walichotenda ninyi. Wale wote ambao tunafikiri tuna chuki, na chuki ambayo inaweza kusababisha kifo cha mtu mwingine ni wakati wa kuongoka sasa. Tutaulizwa na Mungu. Sisi sote ni mali yake Mungu na tutasimama mbele ya hukumu, mbele yake.

Ndugu zangu mliopo hapa waombolezaji, jambo kubwa la kuwambieni, pole! Pole Mapadre, na kwa Baba Padre Meneja wa miradi, Paroko, msaidizi wake, watawa, pole mkuu wa shule na timu yako, poleni sana wanafunzi mliokuwa mnahudumiwa na Sista, poleni Shirika, waamini wote wa Parokia hii, viongozi wetu wa serikali, wakuu wetu wa usalama, raia wa Tanzania, Poleni kwa msiba huu unaotupa aibu, unaotupa aibu na uchungu mkubwa. Poleni!

Njia za uovu zinakuwepo katika jamii, tusikate tamaa, wanafunzi msikate tamaa, walimu na walezi msikate tamaa, watawa msikate tamaa. Endeleeni kuwa na njaa na kiu ya haki kwani hiyo ni njaa na kiu ya kutamani kutenda anayotaka Mungu. Hiyo ndiyo hekima, endeleeni kuwa na njaa na kiu ya haki. Jambo ambalo analifahamu mtu kuwa ni la kweli hawezi kulikana kwa hiyo msianze kukana yaliyo ya kweli. Mtakatifu Karoli Lwanga alisema: “analofahamu mtu kuwa ni la kweli hawezi kulikana”. Na ninyi vilevile mnalojua kuwa ni la kweli msilikane.
Yawezekana tukapatwa mateso mengi zaidi, yawezekana tukapata hasara kubwa zaidi, lakini tukiishi au tunakufa tukumbuke tupo kwa ajili ya mapenzi ya Mungu. Msiogope!, msiogope! Kuweni watu wa rehema, samehe tu, samehe tu, kama Mungu angewasukuma wakaomba msamaha tungefurahi, tungegeuka na kusema Mungu mkubwa, lakini Shetani anapenda pia kuwa na raia wake, kwa hivyo hawezi kusema Mungu mkubwa, hivyo muwasamehe tu ..........AMINA.
Imeandaliwa na
Padre Joseph Peter Mosha,








All the contents on this site are copyrighted ©.