Bwana Maurizio Guizzardi mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Agostino Gemelli iliyoko
mjini Roma katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kitivo cha
tiba na upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, anasema,
wagonjwa wengi kutoka ndani na nje ya Italiwa wameendelea kupata huduma ya kinga na
tiba kwa kutumia teknolojia na utaalam wa kisasa kabisa katika kuwahudumia wagonjwa
kwa kuzingatia mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili.
Hospitali imekuwa ikiwahudumia
wagonjwa na ndugu zao katika mazingira ya upendo na mshikamano wa dhati kwa kutambua
kwamba, Kitivo hiki ni kati ya vitivo vinavyoongoza nchini Italia katika huduma za
kinga na tiba pamoja na tafiti za kisayansi. Hapa wanafundwa kitaaluma waganga, wauguzu
na wafanyakazi katika sekta ya afya katika ujumla wake.
Ni hospitali ambayo
inaongoza katika mkoa wa Lazio kuwa kulaza na kuwahudumia wagonjwa wengi. Ni hospitali
kubwa kitaifa inayotibu ugonjwa wa saratani na kwamba, hapa ni kimbilio kwa magonjwa
yaliyoshindikana sehemu mbali mbali za mkoa wa Lazio.
Bwana Guizzardi anasema,
athari za myumbo wa uchumi kimataifa hazipaswi kamwe kuathiri tija na huduma inayotolewa
hospitalini hapo na kwamba, hospitali itaendelea kuwafunda wafanyakazi wake, ili waweze
kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na jamaa zao.
Professa Franco Anelli,
mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu anasema, miaka 50 iliyopita,
ulikuwa ni mwanzo wa historia ya Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu,
kwa kuwaonjesha watu furaha wakati wa uzinduzi wake, simanzi na uchungu wakati watu
wanapolazwa, lakini daima watu wameendelea kuonesha matumaini kutokana na huduma bora
ya kinga na tiba inayotolewa hospitalini hapo, kwa kumpatia mgonjwa kipaumbele cha
kwanza.
Wafanyakazi hospitalini hapo ni watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili
ya huduma kwa wagonjwa. Hapa sayansi na imani vinakamilishana, kiasi kwamba, Chuo
kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kimeendelea kuwa aminifu kwa mwongozo
wa muasisi wake Padre Agostino Gemelli. Chuo kimeendelea kusoma alama za nyakati ili
kuhakikisha kwamba, kinatoa huduma makini kwa kuzingatia tafiti za kisayansi na teknlojia
iliyoko uwanjani. Hapa ni mahali pa kukinga na kutibu maradhi; majiundo makini na
tafiti za kisayansi.
Professa Rocco Bellantone, Mkuu wa kitivo cha tiba na
upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu anasema, kila siku
wako bega kwa bega na wagonjwa wanaosumbuka na kuteseka kama sehemu maalum ya utume
wao.
Wamejifunza kwamba, wao wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya kumhudumia
binadamu mzima: kiroho na kimwili. Wagonjwa wanapewa dawa na kuonjeshwa upendo wa
dhati unaojikita katika huduma makini. Katika shida na mahangaiko, wagonjwa wanapaswa
kuoneshwa mwanga wa imani kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayeponya na kufariji.
Kutokana
na changamoto hii, wahudumu wa sekta ya afya wataendelea kuchakarika ili kuhakikisha
kwamba, wanamhudumia mgonjwa kikamilifu na kamwe hawawezi kuridhika na kiwango cha
huduma wanachokitoa kwa sasa. Kila siku katika waganga na watafiti wanajikuta wakikabiliana
na changamoto mbali mbali kutoka kwa wagonjwa, changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa
kazi kwa ujasiri pasi na kukata tamaa.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1961
hadi mwaka 1964 Gemelli ikawa ni Hospitali kubwa inayotegemewa na wengi. Ni hsopitali
ambayo ni jukwaa la Chuo kikuu cha Kikatoliki. Hapa si mahali pa kujifunza peke yake,
kwani mganga anaishi kwa ajili ya kumhudumia mgonjwa. Hospitalini hapa mgonjwa anaheshimiwa
na kuthaminiwa kwa kuzingatia kanuni za ukweli, umakini na huruma.
Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.