2014-06-26 07:04:30

Upole na unyenyekevu wa moyo!


Leo tunaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, yaani, jamii yote ya waamini tunaungana katika kutafakari na kuadhimisha Upendo mkuu wa Mungu uliojidhihirisha katika Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo. Tunapoimba masifu ya Moyo huu wa mwokozi katika orodha iliyomo katika Litania ya Moyo wa Yesu kwa hakika tunakutana na tunu mbalimbali ambazo kwazo ni chachu kwetu katika kuelekea maisha ya ukamilifu. RealAudioMP3


Kristo anawekwa kwetu kama dira ya maisha ya kikristo, kwa njia yake, tunafanywa tena upya na kuwa watoto wa Mungu kadiri anavyofafanua mtume Paulo: “kwa kuwa alitangulia kutuchagua ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo sawasawa na Uradhi wa mapenzi yake” (Ef 1:5) na Mtume Paulo anaendelea kufafanua kuwa “yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote” (Kol 1:15). Hivyo, tunavyotafakari Upendo wa kimungu uliojifunua katika Moyo huu mtakatifu wa mwokozi tunapaswa kujiuliza tangu mwangu mwanzo juu ya sifa za moyo huo wa Kristo.


Injili ya leo inapambanua kwa uwazi kabisa sifa hizo zilizoupamba Moyo mtakatifu wa mwokozi kwa kuzijumuisha katika fadhila kuu mbili, upole na unyenyekevu. “Jitieni nira yangu mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11:29a). Injili inaendelea kutumbia kwamba kwa kutekeleza agizo hilo la kimungu la kuifanya mioyo yetu kuwa na umiliki wa upole na unyenyekevu wa kimungu tumeahidiwa raha: “nanyi mtapata raha nafsini mwenu, kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi” (Mt 11:29b). Ni juhudi ya mwanadamu kila wakati maishani mwake kutafuta raha katika nafsi, sasa kama tunaahidiwa raha kama hii, tena katika wepesi na urahisi, Mungu atupatie nini tena?


Lakini changamoto inaweza kujitokeza mbele yetu kwamba ni jinsi gani tunaweza kuuelewa na kuupokea huo upole na unyenyekevu wa Kristo. Sehemu hiyo ya Injili inamepatia mfano wa kawaida kabisa wa maisha ya kila siku ya mwanadamu, mfano wa kujifunza na kuchota maana ya kuwa wapole na wanyenyekevu: “kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga” (Mt 11:25).


Ni jibu jepesi kabisa ambalo kwa kumweka mtoto mbele yako na kutafakari maisha yake utafanikiwa kuona kwa wazo kabisa upole na unyenyekevu huo wa kimungu. Kwa mtoto mdogo tunajifunza unyoofu, msamaha, mahusiano yasiyo na hila, umoja, utayari wa kupokea mapya kutoka kwa wengine, utayari wa kusikiliza wengine na fadhila nyingine nyingi mno. Kwa maneno mafupi kabisa katika mtoto tunajifunza namna ya kupenda kadiri ya kipimo cha kimungu.


Somo la pili la leo linatupatia agizo hilo la kupendana sisi kwa sisi lakini pia linaainisha wazi kuwa kipimo cha upendo huo ni upendo wa kimungu kwa kuwa “Mungu ni Upendo” (1Yoh 4:8). Kipimo cha upendo wa kimungu kama alivyodokeza Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana siku ya Dominika ya Ekaristi Takatifu ni “kupenda bila kipimo”. Hatari ya kupenda kwa kipimo ni kuelekea katika kutenda kadiri utakavyofaidika.


Upendo huu unaitwa upendo wa “nipe nikupe”. Ni sumu kali sana katika ufuasi na katika maisha ya kikristo. Kristo alipokuwa anawaita baadhi ya wafuasi wake alionesha hatari hii: “Mtu mwingine pia akamwambia, ‘Bwana nitakufuata; lakini nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu’. Yesu akamwambia, ‘Mtu atiaye mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu” (Lk 9:61 – 62). Kumbe basi tunaona kwamba Upendo wa kimungu unatudai kujitoa kabisa bila kuangalia nyuma, bila kutafuta kipimo. Ni upendo unaotudai kujitoa wazima wazima kwa ajili ya wengine.


Kristo anaendelea kuwa mfano wa namna hiyo ya kupenda na kwa namna ya pekee tunaweza kuuona Moyo wake Mtakatifu ulivyojazwa na upole na unyenyekevu, jinsi alivyo mkarimu na kuwafikiria wengine. Katika sala yake ya kikuhani Yeye aliomba kwa Baba kwa ajili ya watu wake aliowapenda upeo (rejea Yoh 17). Aliwaombea uzima wa milele, kinga dhidi ya uovu, wadumu katika ukweli na wawe na umoja, Upendo huu ndiyo unatufanya kupenda kwa kutumikia, kupenda kwa kuangaikia fanaka ya wengine, kupenda kwa kujali jirani yako.


Hivyo, katika adhimisho la Sherehe hii ya leo tulipokee agizo hili la kimungu tuliloagizwa katika somo la Injili “jitieni nira yangu mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11: 29). Kwa kutekeleza agizo hili, kwa kujifananisha mioyo yetu na moyo wa Mwokozi Familia zetu zitaishi katika namna njema kabisa ya kusaidiana, kusikilizana, kusameheana na kutiana moyo.


Kila mmoja ndani ya familia atakuwa na fursa na kupokea na kushirikisha chochote chema na kwa njia hiyo umoja na uelewano utazidi kuimarika. Zaidi ya hapo kwa kuwa familia zitaimarika kwa umoja na uelewano basi itakuwa ni chachu kwa umoja wa kijamii, amani na uelewano kati ya jamii ya watu. Leo hii tunashuhudia magomvi, kutoelewana, kutokuaminiana katika jamii ya wanadamu. Mambo haya yote si ya kufurahisha na kutia moyo na dawa yake ni hii moja “upole na unyenyekevu wa Moyo wa Kristo”.


Tuhitimishe tafakari yetu kwa kuangalia ni kwa nini tujikabidhishe katika Upendo huo wa kimungu. Ni nini ambacho kinatuthibitishia kuwa kweli upendo wake kwetu ni thabiti. Somo la kwanza la siku ya leo limetuthibitishia: “bali kwa sababu Bwana anawapenda” (Kumb 7:8) na wimbo wa zaburi unahitimisha kwa kusema kwamba “fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele” (Zab 103:17).


Mwenyezi Mungu hapendi kwa sababu ya kufaidika na sifa zetu na sauti zetu za kuabudu, mwenyezi Mungu hapendi kwa sababu ya ukuu wetu, au sababu tumemfanyia mambo makubwa. Yeye ni thabiti katika upendo wake kwetu sababu yeye mwenyewe ni upendo. Mema na baraka zake tunazoshuhudia kila siku ni uthibitisho tosha wa Upendo wake kwetu usio na kipimo: “Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu, Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu” (Kumb 7:9).


Katika Litania ya Moyo Mtakatifu wa Yesu huwa tunahitimisha kwa sala ya kiitikizano ambyo husema: “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ufanye mioyo yetu ifananae na moyo wako”. Basi tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie tunapoadhimisha Sherehe hii ya Mapendo yake wetu kuifanya mioyo yetu kufanana na Moyo Mtakatifu wa mwanae Bwana wetu Yesu Kristo.


Upole na unyenyekevu wa Kristo uwe chachu ya maisha ya umoja badala ya kutengana, maisha ya msamaha badala ya visasi, maisha ya kutakiana mema badala ya mabaya, maisha ya kupendana badala ya chuki na maisha ya utakatifu badala ya dhambi.

Tumsifu Yesu Kristo!

Imeandaliwa na
Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.