Wapendwa taifa la Mungu, Tumsifu Yesu Kristu. Leo Mama Kanisa anasherehekea sikukuu
ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Moyo uliochomwa
mkuki pale msalabani. Kumbe Mama kanisa anasherehekea chemchemi ya neema za Mungu.
Sherehe hii ni kati ya sherehe za Bwana kadiri ya mpango wa kilitrujia ambayo huja
kila Ijumaa ya pili baada ya sherehe ya Pentekoste.
Mara moja tunaposikia
neno Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunapaswa kukumbuka maneno ya Mt Yohane, asemaye “tazama
jinsi Mungu alivyoupenda ulimwengu”. Na hivi bila kubabaika tunatambua kuwa ni mapendo
ya Mungu kwa wanadamu wote na kwa vizazi vyote. Kanisa likitafakari zawadi hiyo kubwa
ya mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote, haliachi kutumia zawadi hiyo kusogeza karibu
neema za Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mapadre wake, ndiyo kusema leo pia ni sikukuu
ya kutakatifuzwa kwa mapadre.
Wapendwa taifa takatifu, tukiwa na nia njema
tumfuase Bwana tukitafakari Neno lake ambalo Mama Kanisa ametuwekea leo hii ili kwalo
tutambue mapendo ya Mungu yatokayo katika Moyo wake. Katika somo la kwanza Mungu anaongea
na Waisraeli kwa njia ya Musa. Anawaambia jinsi alivyowapenda, akisema sikulazimishwa
na awaye yote wala kitu chochote, wala wingi wenu, wala uzuri wenu katika kuwapenda
ninyi, bali uthabiti wa moyo wangu na makusudio makamilifu yaliyo katika moyo wangu
tangu milele.
Baada ya tangazo la mapendo ya Mungu kwa Waisraeli Musa anawaalika
wapokee mwaliko huo mtakatifu kwa kuishika sheria ya Mungu na hukumu zake. Wote twajua
kuwa "sheria ya Mwenyezi Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya…" Zab. 19:7 Huo ndio
mwitiko wa mkristo na awaye yote katika kupokea mapendo yatokayo katika Moyo Mtakatifu
wa Yesu.
Mwinjili Matayo anakazia mwaliko huo kwa kuonesha matokeo ya mapendo
ya Mungu kwetu. Akisema njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo
nami nitawapumzisha" Mt 11:28. Kumbe wale wote watakao itika mwaliko huu watapumzik
katika Moyo wa mapendo kwa kuondolewa mizigo yote yenye kuleta udhaifu wa roho na
mwili. Pamoja na hilo Mwinjili anakazia pia jambo la unyenyekevu na upole wa moyo
na anatualika kutambua kuwa mahali pekee pa kujifunza ni katika Moyo Mtakatifu wa
Yesu, ambaye amefunua pendo la Mungu.
Mwinjili Yohane katika kutangaza upendo
wa Mungu anafundisha akisema ili mmoja aweze kupokea mwaliko wa mapendo, yampasa kusadiki
kabisa katika Mwana wa Mungu aliye ndani ya Baba, na kwa namna hiyo Mungu atakuja
ndani yake. Anaweka wazi fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu, upendo halisi yaani
Mungu anapomtoa Mwanae wa pekee kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Kwa umwilisho,
Mungu anaitazama dunia katika mtazamo chanya, na anaingia katika historia ya maisha
ya watu aliowapenda milele.
Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican katika ile Hati
ya kichungaji juu ya Kanisa katika ulimwengu "Gaudium et Spes" unawaalika waamini
kuitazama dunia katika mtazamo chanya na kuweka chachu ya Injili kama Kristu alivyoweka
chachu ya mapendo kwa njia ya umwilisho wake. Kwa sababu hiyo, leo Kanisa linasali
kwa kuuelekea Moyo Mtakatifu wa Yesu ili mapendo ya moyo huo yakae ndani ya ulimwengu
na ulimwengu huu uwe ni mahali pema pa kuishi.
Baada ya tafakari toka Neno
la Mungu naomba tuchukue maneno machache katika lugha yetu ya kila siku yatusaidie
katika kutambua mwelekeo wa mwanadamu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Daima Nasikia watu
wakisema "Jamaa yule ana moyo" na labda nawe umesikia! Unalo swali juu ya hili? Mimi
nina swali “ mbona watu wote wana mioyo?
Kwa vyovyote vile hapa kuna jambo
la ziada ambalo haligusiki, natumai si moyo wa nyama bali moyo wa mahusiano mema na
watu wengine na hivi moyo wa mapendo ya kimungu. Katika kuendelea kufuatilia nimesikia
pia watu wakisema "jamaa yule ana moyo mkuu" ndiyo kusema anao moyo wa kustahimili,
kutafakari na kuvumilia mateso yampatayo katika maisha yake. Si hayo tu bali nimesikia
"jamaa yule ana moyo mpole" kwa jinsi hiyo jamaa huyu anao moyo wa mapendo yatokayo
katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, maana Bwana mwenyewe amesema "mimi ni mpole na mnyenyekevu
wa moyo”
Mpendwa msikilizaji, tokana na tafakari hii, kama mmoja atakuuliza
nini maana ya Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, mara moja sema sikukuu ya Mapendo
ya Mungu kwa Wanadamu wote, Sikukuu ya kuwatakatifuza mapadre. Ni sikukuu ya upendo
upeo utokao kwa Mwenyezi Mungu.
Mama Kanisa amechagua sikukuu hii iwe ni kwa
ajili ya kuwatakatifuza mapadre ili wajazwe neema na baraka tele kwa ajili ya kazi
yao ya kichungaji inayodai mapendo ya kimungu. Kwa neema na baraka hizi taifa lote
la Mungu litatakatifuzwe. Kumbe ni sikukuu ya kutakatifuzwa pia kwa waamini wote,
maana mapadre si kwa ajili yao wenyewe bali kwa ajili ya uchungaji uliojazwa nguvu
ya Kimungu.
Wanatakatifuzwa ili waweze kukaa katika kifua cha Bwana na wavumilie
utume wao mpaka wanapofikisha taifa la Mungu katika Yerusalem mpya. Wanatakatifuzwa
ili maisha yao yawe ni chachu kwa maisha ya watu, yawe ni ekaristia mkate umegwao
katika jumuiya kama asemavyo Mtakatifu Ursula.
Tunaalikwa basi leo kuwaombea
mapadre wote na Wanaushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulimwenguni kote, ili maisha
yao yawe changamoto kwa taifa zima la Mungu. Tunawatakieni heri na baraka tele zitokazo
katika Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.