Kuporomoka kwa thamani ya Kwacha Zambia ni janga kwa wananchi!
Askofu mkuu Telesphore Mpundu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia anasema Kanisa litaendelea
kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapenda kuona kwamba, wananchi wote wa Zambia wanahudumiwa
barabara kadiri ya Katiba, sheria na kanuni za nchi bila upendeleo.
Ni dhamana
ya watunga sera na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanachukua hatua madhubuti katika
kupanga na kutekeleza sera ambazo zitawasaidia wananchi wa Zambia kuwa na nguvu ya
kiuchumi, kuliko ilivyo sasa kiasi kwamba, wananchi wengi wanaendelea kukata tamaa
kutokana na mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma baada ya thamani ya fedha ya Zambia
kuendelea kuporomoka katika soko la fedha.
Askofu mkuu Mpundu anasema, ikiwa
kama maskini wanaendelea kutumbukia katika umaskini, hapa kuna walakini katika utawala,
kwani sera na mikakati ya kiuchumi haina budi kuhakikisha kwamba, inawasaidia watu
kujikwamua kiuchumi, pale lengo hili linaposhindwa kufikiwa, Serikali haina budi kuketi
na kuangalia upya mikakati na sera zake za kiuchumi.
Askofu mkuu Mpundu ameyasema
haya hivi karibuni wakati wa mahojiano na gazeti moja nchini Zambia kuhusu hali ya
umaskini wa wananchi wa Zambia. Kanisa katika utume wake wa kinabii, linapenda kuishauri
Serikali ya Zambia kuangalia sera na mikakati yake ya kiuchumi ili iweze kusaidia
kuchangia mchakato wa maboresho ya wananchi wa Zambia. Imeandikwa kwamba, “mtawatambua
kwa matunda yao”.
Serikali ya Zambia haina budi kubuni mikakati ya kuimarisha
fedha yake, vinginevyo watu wataendelea kuteseka kutokana na kushuka kwa thamani ya
Kwacha ya Zambia. Kanisa litaendelea kutekeleza utume wake wa kinabii kwa kuishauri
Serikali pale inapoona inafaa, ili kukuza na kudumisha misingi ya utawala bora kwani
hapa Kanisa na Serikali linawahudumia Wazambia: kiroho na kimwili, kumbe kuna haja
ya kushauriana, kusikikizana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Zambia katika ujumla wao!.