2014-06-26 07:02:14

Jubilee ya miaka 50: Hospitali ya Gemelli ni nyumba ya afya na sayansi ya tiba!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, sanjari na siku ya kuombea utakatifu wa Mapadre hapo tarehe 27 Juni 2014, majira ya jioni anatarajiwa kutembelea, kuzungumza na kusali pamoja na Familia ya Mungu katika Hospitali ya Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma.

Hii ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kilipozinduliwa Kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kilichoko mjini Roma. Kitivo hiki kimeendelea kuwa ni nyumba ya afya na jukwaa la sayansi.

Jubilee ya miaka 50 ya Kitivo hiki ni matunda ya ukarimu yaliooneshwa kwa namna ya pekee na Papa Pio wa kumi na moja kunako mwaka 1934 alipowazawadia Wafranciskani eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kitivo cha Tiba ya Upasauaji kilichozinduliwa kunako Mwaka 1964 na tangu wakati huo, Kitivo hiki kimekuwa ni chemchemi ya matumaini, huruma na mapendo kwa wagonjwa na wafanyakazi Hospitalini hapo.

Hizi ni juhudi kubwa zilizofanywa na Padre Agostino Gemelli, daktari na mtawa wa Shirika la Wafranciskani aliyeanzisha hatua za mwanzo kabisa cha mchakato wa ujenzi, lakini akafariki dunia tarehe 15 Julai 1959 na ujenzi ukashika kasi rasmi kunako mwaka 1961. Kitivo hiki kinaendelea kujipambanua kutokana na huduma makini inayotolewa hospitalini hapo, majiundo ya kina kwa waganga na wafanyakazi katika sekta ya afya. Hapa kuna urithi mkubwa wa sayansi ya tiba ya mwanadamu, tafiti za kisayansi kuhusu magonjwa mbali mbali na tiba ya uhakika.

Ni Hospitali inayohudumia wagonjwa kutoka ndani na nje ya Italia. Kunako mwaka 1978 Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea hospitalini na kusalimiana na wagonjwa pamoja na wafanyakazi. Miaka mitatu baadaye, yaani mwaka 1981 akapelekwa hospitalini hapo akiwa mahututi baada ya kupigwa risasi alipokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kunako mwaka 1996 Papa Yohane Paulo II akalazwa tena hospitalini hapo na siku moja akawaambia watu akisema kwamba, kwake Hospitali ya Gemelli imekuwa kama Ikulu ndogo, baada ya Vatican na Castel Gandolfo, mahali ambapo Mapapa wengi walikuwa wanakwenda kujipumzisha wakati wa majira ya kiangazi.

Historia inaonesha kwamba, Mtakatifu Yohane XXIII alitembelea Hospitali ya Gemelli kunako mwaka 1961 na kuzindua kitivo cha tiba. Kunako mwaka 1976 Mtumishi wa Mungu Paulo VI alitembelea hospitalini hapo na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa hospitali ya Gemelli. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2006 alitembelea hospitalini hapo na kuzindua mwaka wa masomo.

Tarehe 27 Juni 2014 ni zamu ya Baba Mtakatifu Francisko kutembelea, kuzungumza na kusali pamoja na wagonjwa, wafanyakazi na wanafunzi wanaosoma katika Kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Hospitali hii imeendelea kutekeleza wajibu na utume wake kwa tija na ufanisi mkubwa licha ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ni hospitali inayotoa huduma bora na makini kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.