2014-06-25 11:08:37

Yohana Mbatizaji kielelezo kwa Wakristo leo



(Vatican Radio) Yohana Mbatizaji ni mfano kwa Wakristo leo hii. Ni wito wa Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne asubuhi, wakati akiongoza Ibada ya Misa aliyoadhimisha katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta, mjini Vatican. Mahubiri yake yalilenga katika somo la Injili, ambalo mlikuwa na maelezo juu ya Siku Kuu ya kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji. Alimtaja Yohana Mbatizaji kuwa "Nabii Mkuu", akijumuisha misingi mitatu ya wito wa Yohana Mbatizaji kwamba ni kujiandaa , kung'amua na kujishusha.

Papa alianza kwa kueleza wito wa kwanza wa Yohana Mbatizaji kwamba, ni maandalizi. Yohana aliiandaa njia ya Yesu bila kutaka sifa yoyote kwake mwenyewe binafsi . Watu walimtafuta na kumfuata Yohana kwa sababu alikuwa na uwezo wa kuhubiri, na alikuwa mkweli na mtu wazi, kwani alipoulizwa kama yeye ndiye Kristo, alijibu kwamba, kamwe siye, ila yeye ni "sauti yake, na aliyetumwa kuandaa njia ya Bwana."

Wito wa Pili wa Yohana Mbatizaji, Papa Francis alisema, ni kuwa ni mang'amuzi. Kutambua mambo kwa kadiri yanavyopita. Yohana alimtambua Yesu kati ya watu waliokuwa wakipita na kumtambulisha kuwa ndiye Masiya wa kweli .Aliwaambia wafuasi wake , kwa sauti kuu , "Tazama huyu ndiye Mwana Kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu". Wanafunzi walitazama , lakini Yesu aliendelea kutembea , hivyo Yohana, kwa mara ingine alirudia kusema , “Tazama, huyu ndiye Mteule wa Mungu!" Yohana alimtambua Masiya na kumtambulisha kwa watu wengine.

Papa aliendelea kutaja wito wa tatu wa Yohana Mbatizaji, alijishusha, ili Bwana aweze pia kukua katika mioyo ya wengine. Alibainisha, hii hatua ya tatu ya wito wa Yohana, ni hatua moja ngumu sana, kwa sababu tabia ya Yesu ilikuwa tofauti na kile Yohana alichokuwa akifiri. Kabla ya kifo chake gerezani, Yohana alijawa na mashaka na kuwatuma wafuasi wake kwa Yesu kuuliza kama kweli yeye ndiye ni mteule. Yohana alijisikia kudhalilika kupitia kifo chake, lakini pia katika giza la mashaka yake, bado anabaki kuwa kielelezo kwa Wakristo leo hii.

Papa Francisko alihitimisha kwa kusema kuwa sisi Wakristo pia lazima kuandaa njia ya Bwana, ni lazima kupata mang'amuzi juu ya ukweli na sisi lazima kuwa kujishusha ili Bwana aweze kukua katika mioyo yetu na katika roho za watu wengine.







All the contents on this site are copyrighted ©.