2014-06-25 10:37:19

Kanuni za utawala bora!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametaja misingi mikuu mitano ambayo utekelekezaji wake unathibitisha kushamiri kwa utawala bora nchini. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba utawala bora unaendelea kushamiri nchini, bado taasisi za usimamizi wa masuala ya utawala bora zina nafasi ya kuboresha kazi yao na kupanua kwa kiasi kikubwa zaidi utawala bora.

Rais Kikwete aliyasema hayo usiku wa Jumatatu, Juni 23, 2014, wakati alipozungumza baada ya kuwa ametunukiwa Tuzo ya Kutambua Mchango Wake wa Kuimarisha Utawala Bora nchini ambayo imetolewa na taasisi nane za usimamizi nchini. Taasisi hizo ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCB), Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA), Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali (ACCGen-D), Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (IAG-D) na Sekretarieti ya Tume ya Maadili.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Tuzo hiyo kutolewa nchini na ilikabidhiwa kwa Rais Kikwete wakati wa chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya wajumbe wa Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) mjini Dar Es salaam. Mkutano huo wa mwaka pia unahudhuriwa na wajumbe waalikwa kutoka nchi za Ujerumani, Afrika Kusini, Uganda, Sweden, Sierra Leone, Nigeria, Niger, Ghana, Kenya, Zambia, Rwanda, Burundi na Ethiopia.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bwana Ludovick Utoh, Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania ina utawala bora kwa sababu inadumisha misingi yote mikuu ya utawala bora. Aliitaja misingi hiyo kuwa ni kushamiri wa demokrasia, uhuru wa kutoa maoni na wa vyombo vya habari, haki ya kila Mtanzania kuishi, utawala wa sheria, kutoingiliana kwa mihimili mitatu ya Serikali.

Rais Kikwete ambaye amesema kuwa amepokea Tuzo hiyo kwa niaba ya viongozi wenzake katika Serikali – Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama –amesema kuwa utawala bora ni jambo muhimu na halina mbadala wake. “Tanzania tumeruhusu uhuru mkubwa kwa wananchi wetu kushiriki katika shughuli zao. Serikali yetu haitishi watu wake. Hatufanyi hivyo. Ziko nchi zinaishi kwa kutisha raia wake na nyie mnazijua, “ alisema Rais Kikwete.


Taarifa kwa vyombo vya habari zinasema Marekani imeipatia Tanzania vitabu vingine milioni 2.5 vya masomo ya sayansi kwa sekondari katika mwendelezo wa nchi hiyo kuisaidia Tanzania kukabiliana na uhaba wa vitabu na walimu wa masomo ya sayansi, Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania Mheshimiwa Mark Chilress amesema. Balozi Childress amezieleza habari hizo njema kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati walipokutana kwa mara ya kwanza tokea balozi huyo alipowasili nchini na kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais kikwete.

Wakati Rais Kikwete akimweleza hali ya utendaji wa sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii nchini na hasa jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto za elimu, Balozi Childress amemweleza Rais Kikwete kuwa uchapishaji wa vitabu hivyo umeanza kufuatia uidhinishwaji wa fedha za kuifanya kazi hiyo mwezi uliopita. “Mheshimiwa Rais ninayo furaha kukujulisha kuwa kazi hiyo imeidhinishwa ifanywe tokea mwezi Mei na kuwa vitabu vitawasili nchini mwanzoni mwa mwaka ujao,”Balozi Childress amemwambia Rais Kikwete ambaye ameshukuru kwa msaada huo mkubwa ambao ni mwendelezo wa misaada ya Marekani katika nyanja ya elimu.

Vitabu hivyo vya sayansi vinakadiriwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni tisa na vitasafirishwa na kuwasili nchini Januari mwakani kabla ya kufunguliwa kwa shule kwa mwaka mpya wa masomo. Kama ambavyo imekuwa kwa misaada ya vitabu kutoka Marekani, miswada ya vitabu hivyo vipya imeandaliwa na kuandikwa na wataalam wa taasisi ya Tanzania Institute of Education na kuhakikiwa na wataalam wa masomo hayo ya sayansi – fizikia, kemia na biolojia kabla ya kupelekwa Marekani kwa uchapishaji.

Tanzania ilianza kupata vitabu vya sayansi kwa mara ya kwanza tokea Rais Kikwete alipomwomba Rais wa 43 wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush kuisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto kubwa za ufundishaji masomo ya sayansi mwaka 2008. Vitabu hivyo ambavyo idadi yake ilikuwa milioni tatu viliwasili nchini mwaka 2010 na kugawiwa katika shule mbali mbali za sekondari.

Rais Barack Obama ameendeleza sera ya kutoa msaada wa vitabu vya sayansi kwa Tanzania na inakadiriwa kuwa vitabu vya sasa vitamaliza mahitaji yote ya vitabu vya masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari nchini kwa angalau miaka miwili ijayo. Tanzania ina kiasi cha wanafunzi milioni 1.8 katika shule za sekondari nchini kwa sasa na kati ya wanafunzi hao theluthi moja wanachukua masomo ya sayansi.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya Tanzania Railway Construction Corporation ya China, Bwana Zhang Zongyan pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation Bwana Lui Zhimng.


Naye Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania Mzee Kingunge Ngombale- Mwiru, ametoa changamoto kwa Watanzania kuwa wao ndio watakaojenga misingi ya maendeleo ya Ujamaa na Kujitegemea. Kauli hiyo ilitolewa na Mzee Ngombale- Mwiru, mara baada ya kutoka katika mkutano wa pamoja kati ya Makamu Wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Li Yuanchao, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti nchini China na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa Tanzania Bara Philip Mangula, uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dares Salaam.

Mkutano huo ambao ulikuwa ikijadili suala ya la ujenzi wa maendeleo ya Ujamaa na Kujitegemea ya jamii ya Watanzania ulioanzishwa na waasisi wa ujamaa huo,ambao ni Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse-tung . “Lazima uendelee mchakato wa ujamaa na kujitegemea. Kazi ya kujenga usawa ni ya kila mtu, watu hawajengewi ujamaa wanajenga wenyewe”, alisema huku akisisitiza kwamba wanatakiwa kushirikiana katika suala hilo. Aliongeza kuwa ikiwa Watanzania watapuuza hakuna mtu anyaeweza kuwajengea maendeleo ya ujamaa huo.

Mzee Ngombale- Mwiru aliongeza kwamba Watanzania wanapaswa kujenga uchumi wa kisasa wa kujitegemea mfano vile kwa kubadilisha kilimo, ufugaji na uvuvi kuwa wa kisasa. Aliwaasa vijana kuwa chachu ya mabadiliko hayo.

Kwa uapnde wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa Tanzania Bara Philip Mangula, alisema mkutano huo ulikuwa unazungumzia ujenzi wa ujamaa na maendeleo ya kujitegemea, uchambuzi wa tathimini ya ya maendeleo ya ujamaa na utaratibu wa utawala. Aliongeza kuwa siasa ya ujamaa na kujitegemea ndio iliyoifanya China kuwa ya pili duniani kiuchumi na hivi sasa ni ya kwanza kwa mujibu wa tathimini ya Juni mwaka 2014. Katika mkutano huo kulikuwepo kwa semina ambayo ilihusisha wasomi kutoka vyuo vikuu na baadhi ya viongozi wa chama hicho.








All the contents on this site are copyrighted ©.