2014-06-24 10:18:44

Sera na mikakati ya utunzaji wa misitu, binadamu apewe kipaumbele cha kwanza!


Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO limetoa taarifa ya hali ya misitu duniani kwa kuzitaka serikali mbali mbali kuhakikisha kwamba, katika sera na mikakati yake ya hifadhi ya misitu, zinatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, ili kusaidia mchakato wa kupambana na baa la umaskini duniani na kusaidia kukoleza maendeleo ya wananchi wengi wanaoishi vijijini.

Taarifa hii imetolewa na FAO wakati wa mkutano wa ishirini na mbili unaojadili taarifa ya Tume ya FAO kuhusu misitu, jambo ambalo linaonesha uhusiano mkubwa uliopo kati ya hali ya misitu na idadi ya watu wanaoendelea kutegemea mahitaji yao msingi katika mazao ya misitu, kama chanzo cha nishati, makazi na huduma za afya kwa kiwango kikubwa. Faida inayopatikana kutokana na misitu na mazao yake, ikiwa kama itatumika kama ilivyokusudiwa itachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza baa la umaskini duniani, kukuza maendeleo sanjari na uchumi wa kijani.

Bwana Jose Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO anasema, misitu ina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Hakuna uwezekano wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani, ikiwa kama misitu hitahifadhiwa vyema. Misitu ni chanzo kikuu cha nishati Barani Afrika kinachotegemewa na takribani nchi 22. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 90 ya wananchi wa Tanzania wanategemea nishati ya kuni. Kumbe, sera na mikakati makini ya utunzaji wa misitu inaweza kusaidia maboresho ya uhakika wa usalama wa chakula duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.