Adhimisheni Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa Ibada, uchaji na nidhamu!
Askofu mstaafu Mathias Josefu Isuja wa Jimbo Katoliki Dodoma, katika maadhimisho ya
Siku kuu ya Ekaristi Takatifu Dekania ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jumapili tarehe
22 Juni 2014 amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kikamilifu ili waweze
kushiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha
na utume wa Kanisa.
Waamini wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri na kuungama
dhambi zao ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani kabla ya kushiriki
Mwili na Damu Azizi ya Kristo, chakula cha kiroho, mkate wa uzima wa milele ulioshuka
kutoka mbinguni. Kwa mtu anayeshiriki Sakramenti ya Ekaristi Takatifu bila ya kufanya
maandalizi ya kina anakula hukumu yake mwenyewe!
Siku kuu ya Ekaristi Takatifu
ni kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, mafumbo yanayoendelezwa
na Mama Kanisa, kila wakati waamini wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kumbe,
hili ni Fumbo la Imani, ambalo waamini wanaalikwa kuliadhimisha kwa Ibada, Uchaji
na Nidhamu. Ekaristi Takatifu ni kiini na chemchemi ya imani, changamoto kwa waamini
kutokubali kuyumbishwa hata kidogo. Waamini wawe tayari kumpokea Yesu wa Ekaristi
na tayari waoneshe ujasiri wa kumpeleka kwa wengine, wao wenyewe wakijitahidi kuwa
kweli ni Ekaristi kwa jirani zao.