Mawaziri wa afya kutoka Guinea, Sierra Leone, Liberia na Pwani ya Pembe, mwishoni
mwa juma walikutana mjini Conakry, Guinea, ili kubainisha mbinu mkakati utakaotumika
katika mchakato wa kudhibiti ugonjwa wa Ebola, ambao unaendelea kusababisha vifo katika
maeneo yaliyoko Afrika Magharibi. Guinea ni nchi ambayo imeshambuliwa sana na ugonjwa
huu tangu ulipojitokeza nchini humo, Januari 2014 na kufuatiwa na nchi za Liberia
na Sierra Leone.
Watu 528 wameshambuliwa homa ya Ebola na kwamba, hadi sasa
watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huu ni 337. Takwimu za Shirika la Afya
Duniani zinaonesha kwamba, idadi ya wagonjwa wa Ebola kutoka katika maeneo haya inazidi
kuongezeka maradufu, kiasi cha kutishia usalama wa maisha kwa wananchi wanaoishi Afrika
Magharibi.