Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani, ILO hivi
karibuni, limejadili kuhusu ajira safi miongoni mwa vijana wa Misri, tukio ambalo
liliwajumuisha vijana kutoka dini ya Kiislam na Kikristo.
Tukio hili
lilipembua kwa kina na mapana kuhusu athari za ukosefu wa fursa za ajira nchini Misri
na mikakati inayoweza kutumika katika mchakato wa kutengeneza fursa za ajira zinazozingatia
ubora wa kazi kati ya vijana wa Misri, ili kutekeleza haki ya kufanya kazi, kuendeleza
ulinzi wa kijamii pamoja na kukuza majadiliano ya kijamii.
Takwimu zinaonesha
kwamba, vijana wanaunda asilimia 70% ya idadi ya watu ambao hawana ajira nchini Misri,
kati yao ni wale waliohitimu shule za sekondari, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu.
Tukio hili liliongozwa na viongozi wa kidini kutoka Kanisa la Kikoptik na Kiislam
kwa kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo ya vijana nchini Misri.
Shirika
la Kazi Duniani, ILO linaunga mkono juhudi za Jumuiya za Kidini katika kuhimiza tunu
msingi za maisha ya kijamii, maadili na utu wema. Kwa kushugulikia fursa za ajira,
ILO inapania pia kuchochea amani kwani Shirika hili lina amini kwamba, hakuna amani
pasi na haki jamii.
Kwa upande wao, viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
wanabainisha kwamba, majadiliano ya kijamii yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa
katika uzalishaji, tija na maendeleo katika nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu.
Kongamano hili ni sehemu ya hija iliyoamriwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika
mkutano wake mkuu wa kumi, uliofanyika mwishoni mwa Mwaka 2013.
Viongozi wa
Kanisa la Kikoptik wanasema kwamba, majadiliano ya kidini na kiekumene ni muhimu sana
katika ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kijamii, kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano
wa kitaifa, kwa kutambua kwamba, licha ya tofauti zao za kiimani, lakini wote ni ndugu
wamoja wanaounda taifa la Misri.
Maendeleo ya kweli yanayozingatia mahitaji
ya mtu mzima: kiroho na kimwili ni muhimu sana hata kwa waamini wa dini ya Kiislam,
wanapotekeleza mapenzi ya Mungu. Viongozi wa kidini wamekubaliana kimsingi kwamba,
wataendeleza juhudi hizi hata kwa siku za usoni kwa ajili ya maendeleo ya vijana wa
Misri.