2014-06-21 10:45:55

Mawasiliano yawakumbatie maskini!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, Kanisa linapohimiza waamini kuwa kweli watangazaji wa Injili ya Furaha lina maanisha kuonesha mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili wao pia waweze kuonja, upendo, huruma, imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kwa ufupi haya ndiyo yaliyojiri katika mkutano wa wajumbe wa Tume za Mawasiliano kutoka katika Majimbo ya Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini, wakati wa kikao chake kilichohitimishwa hivi karibuni. Wajumbe wamekazia umuhimu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini kushirikiana kwa karibu zaidi pamoja na kubadilisha habari, ujuzi na mang'amuzi katika utekelezaji wa mchakato wa Utangazaji wa Injili ya Furaha kwa watu wa Mataifa.

Wajumbe wameangalia maeneo ya pamoja ambayo wanaweza kushirikiana kwa karibu zaid, ili kuimarisha huduma ya mawasiliano ya jamii inayotolewa na Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini. Wajumbe wanaendelea kuhimiza ushirikiano kati ya idara mbali mbali za Mabaraza ya Maaskofu, ili kwa pamoja, ziweze kujenga mtandao wa habari utakaowanufaisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Wamechambua pia ufanisi, fursa na changamoto zilizopo katika mtandao wa habari kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini.

Kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Novemba 2014 kutafanyika mkutano wa mtandao wa mawasiliano ya Jamii Amerika ya Kusini, huko Lima, nchini PerĂ¹. Licha ya kuwepo kwa maboresho makubwa ya uhuru wa vyombo vya habari Amerika ya Kusini, lakini CELAM inasema, bado kuna baadhi ya Serikali zinatoa vitisho kwa waandishi wa habari, kuna vizuizi vya kupata habari na kwamba, kuna haja ya kufanya maboresho makubwa katika njia za mawasiliano ya habari kwani hii ni sehemu ya watu kutekeleza uhuru wao wa kujieleza kadiri ya sheria zilizopo. Mitandao ya kijamii haina budi kutumika barabara ili kuhabarisha na kuwashirikisha watu mbali mbali Injili ya Furaha.







All the contents on this site are copyrighted ©.