Jubilee ya miaka 50 ya Kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Moyo Mtakatifu wa Yesu!
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa
kwa Kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa
Yesu kilichoko mjini Roma, sanjari na Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku ambayo
imetengwa maalum kwa ajili ya kuombea Utakatifu wa Mapadre, atatembelea na kusali
pamoja na Majaalimu, wafanyakazi, wanafunzi na wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali
ya Gemelli.
Kitivo cha Tiba na Upasuaji, kiko chini ya maombezi ya Moyo Mtakatifu
wa Yesu, Siku kuu ambayo itaadhimishwa Ijumaa, tarehe 27 Juni 2014. Baba Mtakatifu
Francisko alionesha nia hii na kuitangaza hadhari tarehe 4 Mei 2014 wakati wa maadhimisho
ya Siku ya 90 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Ratiba
elekezi kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha kwamba, atawasili Hospitalini
hapo majira ya Saa 9:30 Alasiri na kupokelewa na viongozi wakuu wa Hospitali. Atasalimiana
na wagonjwa watakaokuwepo kwenye Uwanja wa Hospitali na wale watakaokuwa wanaangalia
kupitia kwenye madirisha ya Wodi zao. Lakini atapata nafasi ya kuzungumza na baadhi
ya wagonjwa kwenye chumba maalum Hospitalini hapo.
Baba Mtakatifu baadaye,
atakwenda moja kwa moja kwenye Kikanisa cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kutoa heshima zake
za dhati kwa Masalia ya Watakatifu Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II. Hapa Baba Mtakatifu
anatarajiwa kutoa hotuba kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu
wa Yesu.
Majira ya saa 11: 30 Jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Baada ya Misa Takatifu,
Kardinali Angelo Scola, Rais wa Taasisi ya Toniolo pamoja na Professa Franco Anelli
mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu watatoa neno la shukrani.
Baba Mtakatifu atatembelea taasisi ya bayolojia na kuzungumza na wahusika na baadaye,
atahitimisha hija yake Chuoni hapo.