Balozi wa Vatican nchini Sudan ya Kusini awasilisha hati za utambulisho!
Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini,
hivi karibuni aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Salva Kiir wa Sudan ya
Kusini, alipotembelea hivi karibuni Jimbo kuu la Juba.
Askofu mkuu Balvo anasema,
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi matukio mbali mbali
yanayotendeka nchini Sudan ya Kusini, hasa kutokana na mahangaiko ya watu wasiokuwa
na hatia; mambo ambayo yanasababishwa na machafuko ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini.
Askofu
mkuu Balvo anaendelea kuwahimiza wadau wakuu wa mkataba wa amani nchini Sudan ya Kusini,
kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana hii nyeti kwa ajili ya kulinda na kudumisha
amani na utulivu Sudan ya Kusini; mambo msingi katika kukoleza maendeleo endelevu
ya binadamu. Upatikanaji wa amani ya kudumu nchini Sudan ya Kusini utawasaidia wananchi
kurudi tena kwenye makazi yao na kuendelea na shughuli za kilimo na uzalishaji mali.
Askofu
mkuu Balvo amelitaka Kanisa pia kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, mshikamano, majadiliano na upatanisho wa
kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini.