2014-06-21 11:04:10

Andaeni sera na mikakati ya maendeleo inayotekelezeka!


Askofu mkuu Seraphin Rouamba, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger anaitaka familia ya Mungu katika nchi hizi mbili kujikita katika mikakati ya shughuli za kichungaji itakayojenga na kuimarisha utamaduni wa maendeleo endelevu ya binadamu, kwa kuzingatia mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Rouamba ameyasema hayo wakati alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu katoliki Burkina Faso na Niger, hivi karibuni, katika Kituo cha Kimataifa cha Kardinali Paul Zoungrana, kilichoko mjini Ouagadougou. Maaskofu wamepata fursa ya kusikiliza taarifa za shughuli mbali mbali zinazofanywa na Tume za Mabaraza ya Maaskofu huko Burkina Faso na Niger.

Askofu mkuu Rouamba anasema kuwa, huduma kwa Familia ya Mungu ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki, kwani linatumwa na Kristo kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kupembuana kubainisha miradi ya maendeleo endelevu inayotekelezeka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Barani Afrika.

Mwishoni, Maaskofu wamewaomba waamini na wananchi katika ujumla wao kuendelea kuombea amani na upatanisho wa kitaifa huko Burkina Faso na Niger.







All the contents on this site are copyrighted ©.