2014-06-20 10:38:02

Watumishi wa umma zingatieni maadili ya kazi!


Serikali ya Tanzania imewataka wananchi kuzingatia taratibu za kimsingi zinazopaswa kufuatwa na mteja wakati wa ufuatiaji na utoaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa na watoa huduma katika sekta ya Utumishi wa Umma nchini. Rai hiyo imetolewa tarehe 19. Juni, 2014 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia wakati alipokuwa akifungua kongamano la Wiki ya Utumishi wa Umma Jijini Dar es Salaam.


Waziri Ghasia alisema katika utoaji wa huduma za umma, mwananchi ambaye ndiye mteja mkuu katika utumishi wa umma ana wajibu wa kuwasilisha taarifa muhimu zitakazoombwa na mtoa huduma wa sekta ya umma, na mwananchi atapaswa kuziwasilisha kama sehemu ya udhibitisho wa kutolewa kwa huduma husika. “Kwa mfano mwananchi anayehitaji huduma ya cheti cha kuzaliwa kwa mtoto wake atapaswa kuwasilisha kadi ya hospitali, ambayo itaombwa na mhudumu wa afya, hivyo ni wajibu wa wananchi kutimiza kigezo hicho kama sharti la msingi la kupatiwa huduma hiyo” alisema Waziri Ghasia.


Akifafanua zaidi alisema ni dhahiri zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya umma na zipo zinazofanyiwa kazi na baadhi yake zinazohitaji ushirikishwaji wa wadau na kwa kulitambua suala hilo Serikali iliandaa kongamano hilo ili kuisaidia kutekeleza mipango yake kwa ufanisi kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa. Aidha Waziri Ghasia alisema katika kipindi cha miaka 50 ya utumishi wa Muungano, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya utumishi wa umma ikiwemo ubunifu wa Sera mbalimbali zinazotekelezwa kupitia kamati za mashauriano baina ya pande mbili za Muungano.


Waziri Ghasia aliongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazolikabili taifa, ambapo kwa kiasi kikubwa utatuzi wake unategemea namna sekta ya utumishi wa umma ilivyojipanga na kutekeleza wajibu wake. “Sekta binafsi, Asasi za Kiraia na Sekta isiyo rasmi ni sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa kuweza kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na uzoefu katika maeneo yetu, na zote kwa pamoja zina mchango mkubwa kwa kuwa zinasaidia kuwasilisha mawazo ya jamii Serikalini” alisema Waziri Ghasia.


Aliongeza kuwa mwaka 2011 Serikali ilibuni sera ya ushirikiano baina yake na sekta binafsi yaani Private Partnership Policy iliyopitishwa mwaka 2010 na kufuatiwa na sheria ya kutekeleza sera hiyo na kwa upande wa Asasi za kiraia upo mwongozo wa kushirikiana na asasi hizo uliotolewa mwaka 2012. Akizungumzia suala la maadili katika utumishi wa Umma, Waziri Ghasia alisema wapo baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya kazi ingawa si wote, kwani kwa sasa Serikali inatafakari changamoto na mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 ya utumishi wa Umma nchini.


Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hab Mkwizu alisema maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni maonesho ya wazi na yanahudhuriwa na wananchi wote yanayotoa fursa kwa watoa huduma ambao ni taasisi za umma kukutana moja kwa moja na wateja na wananchi kwa upande mwingine. “Utaratibu huu unatumika kuelimisha na kuonesha aina ya huduma zinazotolewa na watumishi wa umma kwa wananchi” alisema Mkwizu.








All the contents on this site are copyrighted ©.